TUKIO la mtoto Nasra Mvungi kuteswa kwa kufungiwa katika boksi ndani ya
nyumba kwa zaidi ya miaka mitatu na kufariki dunia baada ya kuokolewa na
wasamaria, limefanikisha kupatikana kwa mtoto mwingine mwenye matatizo
ya kiafya ambaye licha ya kuzaliwa miaka 18 iliyopita, inaelezwa
hajawahi kulia, kuongea, kukaa wala kutembea.
Mtoto huyo mwenye mwonekano kama wa mtoto mwenye umri wa miaka mitano,
amepatikana baada ya wasamaria kutoa taarifa Dawati la Jinsia katika
Jeshi la Polisi wilayani hapa, wakiarifu kuwapo kwa mtoto mlemavu
anayenyanyaswa kama ilivyokuwa kwa mtoto Nasra `Mtoto wa Boksi’.
Katibu wa Dawati la Jinsia, Koplo Janeth Maeda amethibitisha kuwapo kwa
tukio hilo, akisema walipokea taarifa za kuwapo kwa mtoto
anayenyanyaswa, hivyo kukimbilia eneo la tukio ili kumwokoa mtoto
aliyedaiwa kuwapo katika mateso ikiwa pamoja na kunyimwa huduma muhimu.
Hata hivyo, anasema walichokishuhudia si mateso, bali ni hali duni ya
kimaisha ya wazazi wake, hivyo kulilazimu Jeshi la Polisi kwa
kushirikiana na Ustawi wa Jamii kumwokoa kwa kumkimbiza hospitali kwa
uchunguzi zaidi wa afya yake.
Anasema: “Kwa kweli tulipopata taarifa hizo tulishtuka sana tukaamua
kuwasha gari na kuelekea eneo la Lukobe ambako ndiko tuliambiwa kuwa
kuna mtoto huyo na kumkuta mtoto huyo, lakini tofauti na tulivyoambiwa,
tulimkuta akiwa katika mazingira mazuri.
“Labda kilichoonekana kwa wengine kama ni mateso ni kwa sababu wazazi
wake kutokuwa na uwezo wa kumudu matibabu tumeamua kusaidiana na ofisi
ya Ustawi wa Jamii Mkoa kumsaidia mtoto huyo kwa kuhakikisha anapatiwa
huduma ya matibabu anayostahili.”
Kwa mujibu wa wazazi wa mtoto huyo wa kike aitwaye Farida, baba Abdallah
Kipingu na mkewe, Mwajuma Abdallah, wakazi wa Lukobe katika Manispaa ya
Morogoro, binti yao huyo alizaliwa mwaka 1996 na kwamba tangu azaliwe
hajawahi kulia.
Mama wa mtoto, Mwajuma akiwa sambamba na mumewe alisema walimzaa Farida
huko Muheza mkoani Tanga na kwamba walimzalia nyumbani, lakini kutokana
na kushindwa kulia, wiki moja baadaye walikwenda Hospitali ya Wilaya ya
Muheza ili kujua kilichomsibu mtoto wao.
“Hatukupata msaada, tukaendelea kumlea alipofikisha miezi minne ambao
mara nyingi ni muda wa kukaa, tulijaribisha kumkalisha, lakini hakukaa
hivyo kwa mara nyingine tukaenda hospitali, safari hii ya Mkoa wa
Morogoro ambako tumekuwa tunaishi, tukaambiwa mtoto ahudhurie mazoezi ya
viungo.
“Tulihudhuria mazoezi kwa muda mrefu hatukuona mabadiliko baadaye
tukaamua kuhamia kwenye kituo cha kulea watoto walemavu cha Amani
Center, tukaambiwa tuendelee ingawa hakukuwa na mabadiliko, tulipohamia
Lukobe mwaka jana hatukuweza tena kumpeleka kwenye mazoezi kutokana na
kukosa uwezo wa kifedha za kufanya mizunguko,” anasema.
Anasema wamekuwa wakiendesha maisha kwa kutegemea biashara ya bidhaa
ndogondogo katika genge lao, msimamizi mkuu akiwa mumewe na kwamba yeye
huhangaika zaidi na mtoto.
“Hayo ndiyo yamekuwa maisha yetu hadi kufikia wakati huu tulipopata
msaada wa Polisi na Ustawi wa Jamii,” anasema mama huyo aliyeiomba jamii
kuwaombea na kuwapa msaada wa hali na mali katika kufanikisha matibabu
na malezi ya binti yao ambaye kwa sasa amefikishwa katika Hospitali ya
Mkoa wa Morogoro kwa uchunguzi zaidi.
Naye Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Morogoro, Oswin Ngungamtitu
aliwashukuru wananchi kwa kuitikia mwito wa kutoa taarifa za matukio
kama ya mtoto Nasra, kwani imewafanya wafumbue macho na kutoa taarifa
mbalimbali.
Alisema taarifa zao zinaweza kuwa faraja kwa watoto na wazazi wengi
wasiojua cha kufanya baada ya kuelemewa na majukumu ya kutunza watoto
wenye uhitaji maalumu.
Hata hivyo, aliitaka jamii kuwapeleka watoto wenye ulemavu na wenye
matatizo katika sehemu zinazohusika ili watoto hao waweze kupatiwa
msaada na hatimaye kuweza kuimarisha afya zao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mganga Mkuu Mfawidhi, Dk Rita
Lyamuya alisema baada ya kupata taarifa hizo taratibu za kumfanyia
uchunguzi zinaendelea ikiwa ni pamoja na kumpatia virutubisho.
Chanzo Habarileo
BOFYA HAPAChanzo Habarileo
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment