Wenyeviti
wa vyama vya Upinzani vya Chadema, Chama cha Wananchi (CUF) na Chama
cha NCCR-Mageuzi, jana usiku walikutana ili kutoa kauli ya pamoja,
kutokana na hotuba ya ufunguzi wa Bunge kwa maelezo kuwa tayari Rais
amevuruga mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya.
Wakati viongozi hao wakikutana, Mwenyekiti wa Chama cha DP Mchungaji,
Christopher Mtikila alisema, Rais ameingilia mchakato na kutoa maelezo
jinsi ya kuandika Katiba.
Wakizungumza na gazeti hili jana mara baada ya hotuba hiyo, Freeman
Mbowe, James Mbatia na Profesa Ibrahim Lipumba, walisema wameipokea kwa
masikitiko makubwa hotuba hiyo.
Awali Katibu wa muda wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Julius
Mtatiro alisema Rais Jakaya Kikwete amevuruga mchakato wa Katiba, kwani
walitarajia angetumia mamlaka yake kama Rais kuwaunganisha.
“Rais tulitarajia angeongea kama mkuu wa nchi, lakini amezungumza
kama Mwenyekiti wa CCM na kutoa msimamo juu ya muundo wa Muungano jambo
ambalo hatukulitegemea,” alisema Mtatiro.
Alisema kwa Rais kutoa msimamo ni sawa na mwongozo jambo ambalo limevuruga mchakato mzima.
Hofu ya kuvunjika Bunge
Wakizungumza nje ya Bunge, baadhi ya wajumbe wameeleza kuwa hotuba ya
Rais Kikwete kama ikitekelezwa uwezekano wa kupata Katiba Mpya utakuwa
mgumu.
Mjumbe Luhaga Mpina alisema kwa jinsi rasimu ilivyoandikiwa na kama
muundo wa serikali mbili ukipita basi rasimu ya Katiba itabidi iandikwe
upya.
“Rasimu yote imetengenezwa kwa mfumo wa serikali tatu sasa hapa kuna hatari ya Bunge kukwama ,” alisema.
Mtatiro kwa upande wake alisema sasa kuna hofu ya kushindwa
kupatikana Katiba Mpya kwani Rais amewachanganya wajumbe na kama
watapitisha maoni yake itabidi rasimu kuandikwa upya.
Mjumbe Mustapha Akoonay, alisema upatikanaji wa katiba upo shakani kwani sasa upinzani utakuwa mkubwa juu ya muundo wa muungano.
“Kwa sasa nadhani itabidi turudi upya kwa wananchi kupata kura ya maoni juu ya muundo wa muungano,” alisema.
Lucy Owenya alisema Rais amegeuza mkutano wa Bunge kuwa ni mkutano
wa Chama Cha Mapinduzi, kwani ameshindwa kabisa kutoa mwelekeo wa nchi
na badala yake ametoa msimamo wa CCM.
“Kutokana na hili, naamini kabisa Bunge halitakuwapo na ni bora iwe
hivyo kwa kuwa amejibu hotuba ya Warioba na kwa maana hiyo amepingana na
mawazo ya wananchi.”
Godbles Lema alisema kuwa Rais hakuja kuhutubia taifa bali alikuja kufanya semina na kujibu hotuba ya Warioba.
Mjumbe huyo ambaye ni mbunge wa Arusha Mjini alionyesha shaka kuwa
baada ya muda wa wiki tatu hakutakuwa na Bunge la Katiba kwa kuwa wako
baadhi ya watu ambao hawatakubali kilichofanywa na Rais Kikwete.
“Waliochukua fedha ni vyema wakaenda kumalizia nyumba zao kwa kuwa
kiongozi wetu amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwafurahisha wanaCCM lakini
kwa Watanzania hatutakubali,” alisema Lema.
John Cheyo alisema, “Mimi ninachokiona ni maridhiano tu, suala la
kufumua rasimu halinipi shida kwa kuwa vitu vyote vinavyoletwa bungeni
huwa ni mali ya Bunge na hivyo tutafanya tunavyoona sisi inafaa.”
Mchungaji Peter Msigwa, alisema kuwa kosa kubwa ambalo lilifanywa na
upinzani ni kukubali na kuruhusu Jaji Warioba atangulie kuwasilisha
rasimu yake akasema hilo ndilo lililowagharimu.
Alitaka Bunge livunjwe mara moja ili warudi kwa wananchi wakaamue na
kuwahukumu kutokana na kile ambacho walikifanya katika Bunge ambalo kwa
maoni yake wamekula fedha za walipa kodi bure.
Naye Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa aliipongeza hutuba ya Rais Jakaya Kikwete ya uzinduzi wa Bunge la Katiba.
Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge la Katiba, alisema kwa kifupi
hotuba ya Rais Kikwete ni nzuri. Lowassa alitoa kauli hiyo, wakati
akitoka nje ya Bunge, muda mfupi baada ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza
hotuba ya uzinduzi wa Bunge hilo.
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment