MARA nyingi manesi wamekuwa wakishiriki katika matukio mbalimbali ya kuua watoto wachanga na kutegemea kulipwa ujira kutokana na kazi hiyo.
Matukio
mengi ya aina hiyo yamekuwa hayaripotiwi kutokana na usiri wa wahusika
kutaka mambo yao yasiwekwe hadharani lakini Oparesheni Fichua Maovu
(OFM), inaendelea kufichua unyama huo na kuumwaga hadharani.
Mara
kadhaa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, chini ya Waziri
Sophia Simba imekuwa ikikemea tabia mbaya ya baadhi ya manesi kutumia
vibaya taaluma yao na kuendeleza mauaji hayo.
SAFARI HII NI MBAGALA
Baadhi ya wazazi wanaoishi Mbagala
Kizuiani jijini Dar waliochoshwa na tabia ya manesi kuua vichanga,
walipiga simu OFM na kulalamikia vitendo vilivyokithiri vya utoaji mimba
katika dispensari iliyopo maeneo yao.
Nesi Maria akiwa katika harakati za kuandaa sindano ya ganzi na vifaa vingine kufanikisha zoezi la kutoa mimba.
OFM iliambiwa
kuwa dispensari hiyo ina manesi wengi wenye ujuzi na fani yao lakini
shughuli kubwa wanayoifanya ni kutoa mimba ili kujipatia fedha kwa njia
haramu.
“Manesi
wa kike wanafanya shughuli za kuua vichanga ambavyo bado havijapata
ruhusa ya kuingia duniani, kwa kweli inauma sana,” alisema mmoja wa
wazazi hao.
Taarifa zikasema kwamba manesi hao wapo
wengi lakini anayefahamika zaidi ni Maria ambaye amejizolea umaarufu kwa
kazi hiyo katika eneo lote la Mbagala.
“Ni
muda mrefu amekuwa akifanya mchezo huo, tena anafanya shughuli zake
bila ya hofu utadhani vitendo hivyo vimeruhusiwa na mamlaka husika,”
aliongeza mzazi mwingine.
OFM IMEJENGA HESHIMA
Wazazi hao wamesema kuwa wanaamini kuwa
Maria atanaswa kama alivyonaswa Dokta Mambo wa Kawe jijini Dar ambaye
naye alikuwa maarufu kwa shughuli kama hizo lakini OFM ikamshikisha
adabu.
Baada ya kutoa maelezo hayo, mmoja wa wazazi hao alitoa namba ya simu ya Maria kwa kamanda mkuu wa OFM.
MTEGO WAANDALIWA
Kamanda Mkuu wa OFM alimpigia simu Maria
na kumwambia kuwa alikuwa akitaka huduma ya kumtoa mimba mke wa mtu
aliyempa kwa bahati mbaya kabla mumewe hajarudi kutoka safarini.
Maria: Hakuna shaka wee njoo tu dispensari kwetu, si umeelekezwa?
Kamanda: Ndiyo.
Maria: Njoo basi tumalize kazi leoleo.
Kamanda: Hiyo kazi inaweza kufanyika kwa ufasaha?
Maria: Miye huwa sishindwi na chochote, wee njoo utafurahi kwa huduma yangu lakini wahi kwani namaliza shifti jioni.
OFM YAJIPANGA
Baada ya maelezo hayo, kamanda wa OFM
akaanza kuwapanga vijana wake kwa ajili ya kumnasa Maria katika mtego
huo siku hiyohiyo ya Machi 15, mwaka huu.
Mmoja
kati ya vijana waliopangwa katika zoezi hilo ni mwanamke mjazito ambaye
alitolewa hofu kwamba mimba yake haitatolewa na OFM watakuwa
wameshavamia katika chumba cha utoaji mimba.
Pia, OFM iliwasiliana na polisi wa Kituo cha Mbagala Kizuiani kwa lengo la kumkamata Maria.
MCHEZO MZIMA
Saa tisa mchana, OFM walikuwa wametanda katika dispensari husika wakiwa na askari waliokuwa wamevaa nguo za kiraia.
KAMANDA ATINGA FRONTI
Baada ya kupeana ishara za kikazi, OFM
na baadhi ya polisi waliingia ndani ya dispensari hiyo kwa nyakati
tofauti huku wakijifanya ni wagonjwa.
Baadhi
yao walijidai wamefika hapo kwa ajili ya kupima malaria huku wakimuacha
kamanda mkuu wa OFM akisonga fronti akiongozana na binti anayetakiwa
kutolewa mimba.
NESI MARIA AITWA MAPOKEZI
Kamanda wa OFM alipofika mapokezi ya dispensari hiyo, alipokewa na kusema shida yake ilikuwa ni kuonana na nesi Maria.
Bila
ya kinyongo wafanyakazi wa mapokezi waliwasiliana na Maria ambaye naye
alimtuma msaidizi wake aitwaye Maimuna kuwapokea wageni hao kisha
kuwapeleka katika chumba maalum.
Maimuna alizungumza na kamanda na kuanza kuelewana kuhusu malipo ya kazi hiyo ya utoaji mimba.
Maimuna: Huwa tunatoa huduma hiyo kwa shilingi 80,000.
Kamanda: Dah! Miye nina shilingi 50,000.
Maimuna: Ongeza kidogo maana ni kazi ngumu sana.
Kamanda: Naomba mnisaidie tafadhali.
Baada
ya maongezi ya muda mrefu, Maimuna alikubali kupokea shilingi 50,000 na
kuanza kumpima mjamzito baada ya kumuelekeza kupanda kitandani kwa
ajili ya maandalizi ya zoezi zima la utoaji mimba.
MIMBA YA MIEZI MIWILI
Vipimo vya dispensari hiyo vilionesha
kuwa ujauzito ulikuwa na umri wa miezi miwili, Maimuna akatoka na kwenda
kuchemsha vifaa vya kazi.
SINDANO TATU ZAANDALIWA
Katika chumba maalum cha kutolea mimba,
Maimuna aliweka vifaa vyote zikiwemo sindano tatu za ganzi alizokuwa
achomwe mjamzito huyo ili asisikie maumivu.
MARIA AINGIA MZIMAMZIMA
Baada ya Maimuna kukamilisha kazi yake,
aliendelea kubaki kwenye chumba maalum, ndipo Maria akaingia chumbani
humo mzimazima akitaka kukamilisha kazi yake.
Kamanda
wa OFM alipiga hesabu zake na kutoa ishara maalum kwa wenzake waliokuwa
nje ili wavamie kwa kuwa mtego ulikuwa umeshakamilika.
MARIA APIGWA NA BUTWAA
Akiwa haelewi kilichokuwa kikiendelea, Maria alipigwa na butwaa alipoona amevamiwa chumbani humo na watu asiowajua.
Taharuki yake ikamfanya ahisi kuwa alikuwa amenasa kwenye mikono ya OFM baada ya kuona kamera zikifanya kazi yake.
ALIJUA ATANASWA
OFM na askari walijitambulisha lakini Maria aliomba sana asitolewe gazetini.
“Chondechonde msinitoe gazetini kwani yatakuwa ni kama yale ya Dokta Mambo,” alisema akiwa ametahayari.
Alipoulizwa
kama alikuwa akifahamu kilichomkuta Dokta Mambo, Maria alisema
aliposoma habari ya dokta huyo alijua kuwa naye kuna siku angenasa ila
hakujua ni lini.
Ama
kweli nimepatikana, yaani kama mlivyomnasa Dokta Mambo, nilijua tu
kwamba lazima siku moja na mimi nitanaswa na OFM, kweli sitarudia tena,”
alisema Maria akiomba mambo yaishe palepale.
Baada ya OFM kumaliza kazi yao, waliwaachia polisi ambao waliwachukua Maria na Maimuna na kuwapeleka kituoni.
DAKTARI WA MUHIMBILI ATAJWA
Hata hivyo, Maria alimtaja daktari mmoja
wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (jina tunalo) kuwa ndiye anayehusika
na dispensari hiyo.
Alipotakiwa
kumpigia simu na kumtaka afike dispensari hapo, daktari huyo alikubali
kufika kabla ya saa 11 jioni lakini hadi saa mbili usiku hakuwa ametia
mguu wake.
Uchunguzi umebaini kuwa huenda alipenyezewa taarifa za kilichotokea na kushauriwa kutofika kwenye dispensari kukwepa msala huo.
Kamanda
wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Engelbert Kiondo hakupatikana
kuzungumzia tukio hilo, ingawa mmoja wa wasaidizi wake ambaye hakutaka
jina lake litajwe alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.
KUTOKA KWA MHARIRI
Bado OFM iko kazini na kamwe haitalala,
Maria alijua iko siku atanaswa ila hakujua siku wala saa, bado wewe
ambaye unadhani hatutakukamata! Itafika zamu yako, acha kufanya uovu na
mambo yasiyokubalika katika jamii.
-GPL
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment