MBUNGE wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) jana alimgomea Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, Kapteni George Mkuchika ambaye alimtaka kufuta kauli yake ambayo alidai inamdhihaki rais wa nchi.
Mkosamali alibishana na waziri huyo katika mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2015/2016 mjini Dodoma jana.
Mkuchika aliomba mwongozo kwa Mwenyekiti wa Bunge, Lediana Mng’ongo kwa kutumia Kanuni ya 64 (d) ambayo inasema ‘wakati wa majadiliano, Mbunge hatatumia jina la rais kwa dhihaka katika mjadala kwa madhumuni ya kutaka kulishawishi Bunge kuamua jambo lolote ambalo kwa namna fulani linamdhalilisha rais’.
“Mheshimiwa Mwenyekiti nimesimama kwa kanuni na. 64 (d). Ndugu yangu Mkosamali namheshimu sana wakati anachangia ameeleza kwamba rais hana utashi wa siasa wa kupambana na rushwa, rais hana nia ya kupambana na rushwa”.
Hata hivyo, Mkosamali alikataa Mkuchika asipewe nafasi ya kuomba mwongozo huo akisema hata yeye jana alinyimwa nafasi ya kutoa taarifa wakati Mbunge wa Tarime, Chacha Nyangwine alipokuwa akichangia hoja yake.
Licha ya kutakiwa kuondoa maneno hayo, Mkosamali aligoma na kusema: “Nitafutaje wakati hiyo ndiyo hali halisi, yaani nifute wakati jambo liko hivyo, juzi tulisikia anasafisha watu wakati mambo yote yameanzia bungeni.”
Awali katika mchango wake, Mkosamali alihoji taasisi muhimu kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mfuko wa Maendelea wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na Mpango wa Kurasimisha Mali za wanyonge Tanzania (Mkurabita) kuwa chini ya ofisi ya rais na siyo waziri mkuu.
“Mheshimiwa mwenyekiti utashangaa, hizi ofisi zilizopo chini ya rais ndiyo zina njaa, njaa imeanzia Ikulu.
“Kwa mtazamo wangu ninaona kwamba tunaweka Takukuru Ikulu ili Rais awe na political will (utashi wa siasa), ataweza kupambana na rushwa katika maeneo mbalimbali.
“Hii maana yake ni kwamba ukiona Takukuru imefeli rais hana utashi wa siasa, ndiyo maana kila siku tunasema Takukuru iwe na meno lakini hawajawezeshwa hivyo.
“Kwa mfano mwaka huu DPP (Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai), amefuta kesi zote muhimu, kwa hiyo kwa Takukuru kufeli maana yake Serikali nzima imefeli. Miaka yenu 10 hamkuwa na nia ya kupambana na rushwa, rais hakuwa na nia ya kupambana rushwa.
“Hawa TASAF mwaka jana mliomba Sh bilioni 18 lakini walipewa tatu tu, chuo cha uongozi hamjawapelekea fedha hivi nyinyi mawaziri na CCM yenu mnataka hao wakurugenzi wa hiyo TASAF wawachukulieje?”alihoji Mkosamali.
Wabunge wengine waliochangia hoja hiyo ni Mbunge wa Manyoni, Kapteni John Chiligati (CCM), aliyeilalamikia serikali kushindwa kutoa fedha za bajeti ya Sh bilioni tatu za Mkurabita akisema haikuwatendea haki wananchi.
Pia aliitaka serikali kuandaa haraka sheria ya Uongozi na Utumishi wa Umma inayowakataza watumishi wa umma kuwa wafanyabiashara ili kuondoa mmomonyoko wa maadili uliokithiri nchini.
Mbunge wa Viti Maalum, Clara Mwatuka (CUF), alisema serikali iache kuwashangaa wapinzani wanaoikosoa kwa sababu hiyo ndiyo kazi yao.
“Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo ni wajibu na jukumu lake na wapinzani wanawakosoa msione kwamba ni vibaya kwa sababu wapinzani kazi yao ni kuisukuma serikali,” alisema Mwaituka.
Hotuba ya Mary Nagu
Awali akiwasilisha bungeni makadirio ya matumizi ya fedha za Ofisi ya rais, Tume ya Mipango kwa mwaka 2015/2016, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Mary Nagu alisema katika mwaka wa fedha 2014/2015 tume hiyo ilifuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo 52 katika mikoa kadhaa nchini.
Hata hivyo alisema miradi hiyo inakabiliwa na changamoto ya kutopata fedha za kutosha na kwa wakati, hali iliyosababisha utekelezaji kuwa nyuma ya ratiba.
“Utekelezaji wa baadhi ya miradi unasuasua au kusimama kutokana na malimbikizo ya madeni ya wakandarasi, lakini ili kukabiliana na changamoto hizo serikali inakusudia kuimarisha vyanzo vya mapato vya kodi na visivyo vya kodi,” alisema Nagu.
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment