Stori: Mwandishi Wetu, Iringa
KATIBU wa CCM wa Mkoa wa Iringa, Hassani Mtenga, mwishoni mwa wiki iliyopita alikiona cha moto baada ya kuzomewa na wananchi baada ya kuwataka wapiga kura hao wamshawishi Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa asichukue fomu za kugombea kiti hicho katika uchaguzi mkuu ujao kwa kuwa hatashinda.
Tukio hilo lililotokea katika Uwanja wa Mwembetogwa mjini hapa ni kama zengwe kwa Msigwa kwani katika mkutano ulioandaliwa na Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kwa ajili ya kutoa elimu ya Katiba Iliyopendekezwa nia ilikuwa siku ikifika wajitokeze kupiga kura ya Ndiyo.
Katika mkutano huo ambao baada ya matamshi hayo ya katibu wa CCM kulizuka vurugu na zomeazomea hiyo ndipo vijana wa CCM waliokuwa na sare za chama waliwafuata wazomeaji na kuwatolea maneno makali yaliyosababisha makundi hayo mawili kutaka kupigana.
Licha ya vurugu hizo Katibu Mtenga hakuishia hapo katika hotuba yake aliendelea kumshutumu Mbunge Mchungaji Msigwa kwa kudai kuwa kwa miaka minne aliyotumikia nafasi hiyo hakuna alichokifanya.
“Tulikuwa na viongozi wengi waliotufanyia makubwa yanayoendelea kukumbwa. Alikuwepo Chifu Adam Sapi Mkwawa, Jackson Makweta na wengine, walifanya kazi kwa uadilifu mkubwa na hawakuthubutu kujilimbikizia mali,” alisema.
Akaongeza: “Lakini Mbunge Msigwa kafanya kazi kwa miaka minne tayari ana yadi ya magari mtaji huo ameupata wapi?”
Kauli hiyo ilichochea baadhi ya vijana waliokuwa wanasikiliza hotuba yake kwa kuanza tena kusomea huku wakionesha vidole viwili alama ya V kama inavyotumika na Chadema ndipo Mtenga akadai vijana hao ni wa Chadema.
Akizungumzia vurugu za vijana hao na madai kuwa ni wa Chadema, mwenyekiti wa chama hicho (Chadema) wa Iringa Mjini, Frank Nyalusi alikana kuwa si wa chama chao kama alivyodai Mtenga.
“Suala la kuzomewa ukiongea pumba lipo duniani kote, mtu akizungumza jambo la uongo na lisiloeleweka ni lazima azomewe,” alisema Nyalusi.
Credit: Uwazi/Gpl
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment