Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This
    Mh.Bernard Membe
KATIKA mfululizo wa makala hizi zinazochambua wasifu wa wanasiasa wanaotarajiwa kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu 2015, leo ‘tunammulika’ Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Camillius Membe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi, Kusini mwa nchi yetu.
Kama tutakavyoona katika uchambuzi huu, huyu ni mgombea mwenye historia fupi lakini yenye kujaa weledi katika siasa za Tanzania na kimataifa, hii ni kwa sababu alikuwa shushushu, hivyo mambo yake mengi kuwa ya siri.
Alizaliwa wapi na lini?
Bernard Camillius Membe alizaliwa Novemba 9, 1953 katika Kijiji cha Rondo Chiponda, Wilaya ya Lindi Vijijini, akiwa ni mtoto wa pili katika familia ya watoto saba wa mzee Camillius Anton Ntanchile na mama Cecilia John Membe.
Membe alifunga ndoa ya Kikristo na Dorcas Richard Masanche mwaka 1986  na Mungu amewajalia watoto watatu, wawili wa kiume na mmoja wa kike.
Kimaisha Membe hakukulia mjini, alizaliwa na kukua akiwa kijijini kama Watanzania wengi waliokulia huko walivyo, hivyo anajua tabu wanayopata wanavijiji kwa sababu alizaliwa katika kijiji ambacho hakikuwa na zahanati na maji yalikuwa shida, alilazimika kutembea kilometa nyingi kuyafuata.
Baba yake alikuwa mwindaji aliyelazimika kuwa hivyo akiwa bado mtoto mdogo miaka kama mitano hivi, wakiwa shambani, Camillius Anton Ntanchile alishuhudia simba akimnyatia na kisha kumdaka mama yake (Bibi yake Bernard) na kutokomea naye, na walikuja kupata baadhi tu ya viungo vya mwili wake.
Kitendo hicho kibaya kilimfanya Camillius akawa na ndoto ya kumiliki bunduki na kuwa mwindaji na akafanikiwa alipokua mkubwa hivyo basi kama wanasiasa wengine wanavyoitwa ‘Mtoto wa Mkulima’, Membe anaweza kupachikwa jina la Mtoto wa Mwindaji!
Baba yake alifariki dunia mwaka 1987 kwa ajali ya kulipukiwa na bunduki pajani baada ya kuvuja damu nyingi akiwa porini. Kwa maelezo ya Membe, hii ndiyo hali iliyomchochea kupigania uwepo wa hospitali ya wilaya katika jimbo lake la uchaguzi.
USOMI NA REKODI ZITAMSAIDIA KUWA RAIS 2015?
Kwa kiasi kikubwa, Membe amefuata mtiririko wa kawaida katika kusoma kwake, elimu ya msingi aliipata katika Shule ya Msingi Rondo Chiponda mwaka 1962 hadi 1968.
Shule ya sekondari alisomea katika Seminari ya Namupa  (1969 hadi 1972), akajiunga na Itaga Seminari Tabora kwa kidato cha tano na sita (1973 hadi 1974.)
 Maandiko mbalimbali niliyowahi kuyasoma yanaeleza kwamba Membe aliwahi kusomea upadri kwa miezi kadhaa.
Baada ya kumaliza kidato cha sita mwaka 1974, Membe alijiunga kwa mujibu wa sheria mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa muda wa mwaka mmoja.
 Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (1981/82), alisomea shahada ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma akitokea Ofisi ya Rais alipokuwa ameajiriwa.
KUMBE NI ‘KICHWA’
Matokeo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yanaonyesha kwamba Membe alifaulu vizuri kwa kiwango cha kupata GPA ya 4.1, huu ni ufaulu wa juu sana,  alipewa barua ya ajira ya uhadhiri wa chuo kikuu hicho katika ngazi ya uhadhiri msaidizi (tutorial assistant), alishindwa kujiunga kwa sababu mwajiri wake, ikulu, alikataa.
Bernard Camillius Membe anayo pia shahada ya uzamili katika Uhusiano wa Kimataifa aliyoipata kutoka Chuo Kikuu cha Johns Hopkins nchini Marekani mwaka 1992.
MSAIDIZI WA MKURUGENZI
Akiwa kachero ikulu alipanda ngazi kadhaa na hata kuwa msaidizi wa waliopata kuwa wakurugenzi wakuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Dk. Hans Kitine na Apson Mwang’onda.
Baadaye Membe alipelekwa ubalozi wa Tanzania nchini Canada kama Mwambata wa Ubalozi (Minister Plenipotentiary), alidumu katika nafasi hiyo hadi mwaka 2,000 alipoamua kugombea ubunge, akashinda na kuwa mbunge wa pili wa Jimbo jipya la Mtama, Lindi akimrithi Masoud Ally Chitende.
ALIVYOMKAMPENIA JK
Katika kampeni za urais za mwaka 2005 ndani na nje ya CCM, Membe alifanya kazi kwa karibu na akina Edward Lowassa na Apson katika kuhakikisha kwamba Rais Jakaya Mrisho Kikwete anapitishwa kuwa mgombea na hatimaye kushinda katika uchaguzi wa urais.
Baada ya Rais Kikwete kushinda uchaguzi wa mwaka 2005 alimteua Membe kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini nafasi aliyoshikilia kati ya Oktoba 2006 na Januari 2007, na baadaye Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani kati ya Januari 2006 na Oktoba 2006.
Baada ya kuteuliwa kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Asha-Rose Migiro kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Rais Kikwete alimteua Membe kuchukua nafasi yake na anaishikilia hadi leo
UTATA WAKE
Membe aliitangazia dunia kupitia Bunge letu Mei 27, 2014 kwamba waasi wa kikundi cha M 23 huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuwa walikuwa ni raia wa Rwanda na walikuwa wakifadhiliwa na Serikali ya Rwanda. Hii ilileta shida kidiplomasia. Pia alilaumiwa kuhusiana na matakwa yake ya kuruhusu uraia pacha na aliungwa mkono na Rais Kikwete, jambo ambalo Baba wa Taifa, mwalimu Julius Nyerere alilipinga.
 UADILIFU WAKE
Bernard Membe ni kati ya viongozi wachache katika serikali ya CCM wanaotajwa kwamba ni waadilifu.
Mapema katika Bunge la mwaka 2001/2002, paliibuka kashfa kubwa ikimhusisha aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, Dk. Hans Kitine. Katika kashfa hiyo ilidaiwa kwamba Dk. Kitine alikuwa ametumia fedha za serikali kwa kumtibu mke wake, Saada Mkwawa Kitine, nje ya nchi kwa kiwango cha dola za Kimarekani 63,000. 
Ni katika hatua hii ambapo Bernard Membe alisimama Bungeni akamwaga nyaraka zinazoonyesha jinsi fedha zilivyotumwa kwenye akaunti binafsi ya mama Kitine badala ya kutumwa katika akaunti ya ubalozi. Dk Kitine ilibidi aachie ngazi serikalini.
Membe ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM aliyeshinda mwaka 2012 na hivi karibuni amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Nchi za Jumuiya ya Madola (CMAG).
Kiongozi huyu anajitambulisha kwa taswira ya uadilifu na kwa kweli ni vigumu kumhusisha na kashfa yoyote iliyotokea hapa nchini, anajivunia rekodi ya kuipaisha Tanzania katika anga za kimataifa kidiplomasia hivyo ukilinganisha na wagombea wengine, huyu anaweza ‘kupeta’ ikiwa turufu yake itakubaliwa na vikao vya juu vya CCM awanie urais.

Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala,

Hifadhi blog hii kwenye simu yako ili upate habari zote kwa urahisi zaidi

Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
http://www.facebook.com/kibonajoro

Post a Comment

 
Top