Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Kwako mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Najua hunifahamu na hakuna mazingira yanayoweza kunikutanisha na wewe na ndiyo maana nimeamua kutumia ukurasa huu kufikisha ujumbe wangu kwako, ambao najua hutaufurahia.
Najua hunifahamu na hakuna mazingira yanayoweza kunikutanisha na wewe na ndiyo maana nimeamua kutumia ukurasa huu kufikisha ujumbe wangu kwako, ambao najua hutaufurahia.
Mheshimiwa, mimi sikuzaliwa Juni 25, 1954 huko Musoma kama wewe. Mimi
si msomi mwenye ‘CV’ ya nguvu na kubobea kwenye sayansi ya miamba na
madini kama wewe. Sijawahi kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wala
sijawahi kujiunga na chama au taasisi yoyote ya kisayansi duniani kama
wewe.
Sijawahi kufanya kazi kama mtafiti kwenye Chuo Kikuu cha Mainz,
Ujerumani kama wewe wala mimi sijawahi kuteuliwa kuwania ukurugenzi wa
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco).
Mimi si mbunge wa kuteuliwa wala waziri mwenye dhamana kubwa kama wewe.
Mimi ni kilaza tu, nisiyekuwa na elimu yoyote kichwani, niponipo tu
mjini naganga njaa kuhakikisha mkono unaenda kinywani.Hata hivyo, pamoja
na ukilaza wangu, ningekuwa mimi katika nafasi yako, kwa hii kashfa
kubwa ya mabilioni ya fedha yaliyochotwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow
inayoendelea kuitafuna nchi, nakuapia kuwa tayari ningeshang’atuka
madarakani.
Nisingesubiri sijui ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali
(CAG), uamuzi wa bunge wala mahakama, dhamira yangu ingenisuta kwamba
madudu haya yamefanyika kwenye wizara yangu kwa kuhusisha Benki Kuu ya
Tanzania (BoT).
Ningeona aibu kwamba dhamana kubwa niliyopewa na mheshimiwa Rais
Jakaya Kikwete kwa niaba ya Watanzania, ya kuhakikisha rasilimali zao
zinawanufaisha wazawa, imenishinda.
Nasikiasikia kwamba eti na wewe ni miongoni mwa vibosile waliochota
zile shilingi bilioni 306 na kuzitia mfukoni, sina uhakika wala siwezi
kuthibitisha hilo kwa kuwa mimi siyo mahakama lakini ile kutajwatajwa
tu, hata kama si kweli, kungetosha kukufanya uachie madaraka na kupisha
uchunguzi.
Ndiyo! Unawezaje kuingia ofisini kwa kujiamini na mwisho wa mwezi
ukaenda kukinga mshahara mnono wakati kazi uliyopewa imekushinda?
Mahakama ilipoamuru kwamba fedha (service charge) zilizokuwa zinalipwa
na Tanesco kwa IPTL, zipelekwe kwenye akaunti maalum, Tegeta Escrow
mpaka muafaka utakapofikiwa kati ya wabia waliokuwa wanahusika katika
kesi hiyo, ilikuwa na lengo zuri la kunusuru fedha za umma.
Sasa iweje hata hukumu bado haijatolewa, watu ‘wajisevie’ mabilioni
ya fedha chini ya wizara yako na BoT, huku wewe uliyepewa dhamana ya juu
kabisa katika wizara, ukilifumbia macho suala hili?
Najua wewe ni msomi ambaye elimu yako imekukomboa ipasavyo. Naamini
kwamba wewe si mwanasiasa bali mtendaji ndiyo maana mheshimiwa rais
alikupa nafasi hiyo nzito ili kuwatumikia Watanzania lakini mbona mambo
yamekuwa ndivyo sivyo?
Nilisikia kauli yako uliyoitoa wakati ukihutubia kwenye mkutano wa
wawekezaji zaidi ya 170 kutoka nchi mbalimbali duniani hivi karibuni
kujadili kuhusu mbinu za kulipatia Bara la Afrika umeme wa uhakika.
Ukasikika ukisema eti fedha zilizokuwa katika akaunti ya Tegeta
Escrow siyo za umma bali ni za Kampuni ya IPTL na ukawataka ‘akina
yakhe’ kuacha kuzikomalia kwani siyo zao, ukadiriki kuwaita majina
mabaya wote wanaolishupalia suala hilo na kutaka wapuuzwe.
Sawa, uelewa wako ni mkubwa na unajua mambo mengi zaidi makubwa
lakini kama kweli wewe ni muungwana, kubali kuwajibika kwanza. Acha
kuleta siasa mheshimiwa, ndugu zetu wanakufa Muhimbili kwa kukosa dawa
wakati mabilioni yamechotwa chini ya wizara yako.
Nguo ikimvuka, muungwana huchutama. Ningekuwa mimi katika nafasi
yako, tayari ningeshang’atuka ili kulinda heshima yangu, kupisha
uchunguzi na kuwaachia wenye uchungu na nchi hii walinde rasilimali
zetu.
Wasalaam.
Wasalaam.
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment