Stori: WAANDISHI WETU
NI kweli Dar si salama tena! Lile sakata la utekaji na mauaji ya watoto, sasa limechukua sura mpya na kulifanya Jiji la Dar kuwa mahali salama kwa kuishi kufuatia kutekwa na kuuawa kwa wasichana wawili na mfanyabiashara mmoja huku watoto wawili wakiwa hawajulikani walipo, Uwazi lina data za kutosha.
Kwa nyakati tofauti, gazeti hili limewahi kuripoti mara kadhaa juu ya utekeji wa watoto wadogo hususan wanafunzi ambao baadaye hupatikana wakiwa wameuawa na baadhi yao wakikatwa viungo vyao nyeti hali inayoonesha kuwa ni mambo ya kishirikina. Lakini safari hii, inaonekana kuwepo mtandao wenye malengo maalum.
WATOTO WAWILI WATEKWA, HAWAJAPATIKANA
Watoto wawili ambao ni majirani wanaoishi Mbagala Kipati, Kuluthumu Selemani (14) na Aisha Muhidin (13), Novemba 10, mwaka huu walitoweka baada ya kuaga majumbani mwao wanakwenda madrasa kwa Ustaadh Hafidhi Sharahani Rashid, lakini tangu siku hiyo hawajaonekana tena.
Kwa mujibu wa chanzo, siku chache kabla ya watoto hao kutoweka, inadaiwa ustaadh huyo aliwanunulia vitambaa vinavyotumiwa na wanawake kujisitiri kichwa (hijabu) ambavyo walivivaa siku ya kutekwa kwao.
Iliendelea kudaiwa kuwa watoto hao baada ya kutekwa, walichukuliwa na kwenda kuhifadhiwa katika nyumba ya bibi mmoja ambaye jina halikupatikana mara moja wa maeneo hayo hayo ya Mbagala, anayetajwa kushirikiana na ustaadhi huyo.
Baada ya kukaa siku kadhaa za ukimya huku kukiwepo na uvumi wa watoto hao kuhifadhiwa nyumbani kwa bibi huyo, wazazi wa watoto hao walikwenda kwa bibi huyo kumtaka awatoe watoto wao, lakini alikataa kuwa nao ndani mwake.
Kuona hivyo, wazazi hao waliwaacha nje watoto wadogo wawili ili waangalie watoto hao wasitoroshwe wakati wao wakienda kutoa taarifa Kituo cha Polisi cha Mbagala Kizuiani, Dar lakini nyuma, inasemekana watoto wawili waliovaa kininja na mtu mzima mmoja naye alivaa kininja walitoka na kutokomea kusikojulikana.
Watoto walioachwa kulinda walibaini kuwa waliotoka ni Kuluthumu na mwenzake, wakatimua mbio kuwafuata wazazi wao na kuwaeleza juu ya jambo hilo, lakini waliporudi wakiwa na askari, hawakufanikiwa kupata chochote kwani bibi huyo aliendelea kukataa kuwepo wala kutoka kwa mtu yeyote ndani kwake.
Baada ya kushindwa kuwaona watoto hao, wazazi wa watoto hao walikwenda nyumbani kwa ustaadh na kumkaba koo wakimtaka kuwatoa watoto wao, lakini alikataa katakata kuhusika na lolote juu ya upoteaji wao.
WAZAZI WAZUNGUMZA
Mama wa Kuluthumu, Mwanahawa Kadala na baba wa Aisha, Muhidin walisema wanashangazwa na jeshi la polisi kukaa kimya badala ya kuwahoji watu hao wawili ambao wanaamini wanajua kinachoendelea.
“Haya mambo ya utekaji nilikuwa nayasikia huko Nigeria sasa yamekuja Tanzania, tunaiomba serikali ifanye uchunguzi sambamba na kumhoji Ustaadh Hafidh ambaye ni mwalimu wao wa madrasa juu ya walipo watoto wetu,” alisema Mwanahawa.
Taarifa ya watoto hao kutoweka ilitolewa katika Kituo cha Polisi Mbagala na kufunguliwa jalada la taarifa lenye namba MBL/RB/2975/2014 kisha jalada la uchunguzi namba MBL/RB/13029/2014.
MSIKIE USTAADH MWENYEWE
Lakini hata hivyo, ustaadh huyo aliliambia gazeti hili kuwa hausiki na suala hilo na kwamba hata yeye linamnyima raha.
“Ni kweli hao watoto ni wanafunzi wangu, lakini sihusiki na kutoweka kwao, natupiwa lawama na wazazi, wengine kudiriki kunikaba na kunipiga.
“Nimekosa usalama, ni bora kama wananihisi polisi waje wanichukue ili nikahojiwe kuliko kunisonga kila kukicha, na mimi nina uchungu kwa upoteaji wa watoto hao, hata sipati usingizi, nimekuwa nikiwatafuta kama wao wazazi wanavyofanya lakini sijafanikiwa,”alisema ustaadh.
KUHUSU BIBI
Juu ya uhusiano wake na bibi anayetiliwa shaka, ustaadh huyo alikiri kumfahamu, lakini alisema ni kwa vile hapo nyuma aliwahi kuolewa katika nyumba yake na kwamba watoto wake pia ni baadhi ya wanafunzi wake wa madrasa.
MFANYABIASHARA NDANI YA NOAH
Katika tukio jingine, Ibrahim Twambile, mfanyabiashara katika Soko la Ilala jijini Dar akiwa kazini kwake Tabata, alitokewa na watu wawili waliojitambulisha kuwa ni askari wa Kituo cha Polisi Tabata hivyo wanamuhitaji kituoni.
Alipokubali, walimchukua na kupanda naye kwenye gari aina ya Toyota Noah. Baada ya kutembea na kufika maeneo ya Tabata, mtu mmoja aliyekuwa katika gari lililokuwa nyuma ya Noah hiyo aliitilia shaka baada ya kuona inayumbayumba, hivyo aliifuata kwa karibu ili ajue kinachoendelea.
WATEKAJI WASHTUKA, WAKIMBIA
Inadaiwa kuwa, watekaji hao ambao hawakufahamika idadi yao ndani ya Noah hiyo, nao walilishtukia gari lililo nyuma yao, hivyo kuongeza mwendo ingawa baadaye iligundulika kuwa kulikuwa na kipigo kikubwa kilichokuwa kikitolewa kwa mtu aliye ndani ya gari hilo.
BODABODA
Baada ya kufika Tabata Segerea, dereva wa gari la nyuma aliwaambia vijana wa bodaboda juu ya wasiwasi wake kwa Noah iliyokuwa mbele yake.
Ndipo bodaboda hao, kama jeshi la sisimizi, waliwasha pikipiki zao na kuanza kuifukuza Noah hiyo ambayo baada ya kuikimbiza kwa muda, walipolivuka daraja la Segerea, mbele kidogo waliona mtu akitupwa nje ya gari hilo karibu na njia panda ya Kinyerezi na Stakishari.
Baada ya kumtupa mtu huyo, watu hao walikwenda Kituo cha Polisi Stakishari na kujisalimisha wakidai kuwa walikuwa wamemuua mtu kwa kumgonga na gari barabarani.
Hata hivyo, wakati polisi wakiweka mafaili sawa kwa kuchukua maelezo, bodaboda walifika kituoni hapo na kuwaeleza polisi ukweli kuhusu watu hao wenye Noah, wakatiwa mbaroni.Taarifa kutoka ndani ya jeshi la polisi zinasema watu wanne wanashikiliwa hadi sasa kuhusiana na tukio hilo ambalo gazeti hili limedokezwa kuwa ni ulipizaji wa visasi.Mwili wa marehemu Ibrahim alisafirishwa mkoani Mbeya kwa mazishi.
WAREMBO WAWILI WATEKWA, WAUAWA
Wanze Makongoro (23) msichana aliyekuwa akisoma Chuo cha Kutunza Kumbukumbu (Ukutubi) Bagamoyo, Pwani, mwili wake ulikutwa ukiwa umetupwa pembezoni mwa bonde la Mto Msimbazi jijini Dar baada ya kutafutwa kwa zaidi ya wiki moja.
Akizungumza na Uwazi Novemba 22, mwaka huu kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar ambako mwili wa Wanze ulikuwa ukiagwa, mama mkubwa wa marehemu, Mgeni Msafiri alisema mwanaye aliondoka chuoni Novemba 13, mwaka huu asubuhi akiwaaga wanafunzi wanzake kwamba anakwenda Mlimani City jijini Dar kutengeneza simu yake.“Kesho yake alituma ujumbe wa simu (SMS) kwa mdogo wake, Hamisa akamwambia ametekwa na watu asiowafahamu,” alisema mama huyo.
Alisema baada ya kupewa taarifa hizo walitoa taarifa chuoni kwake ambao nao waliwaeleza polisi na baadaye vituo vyote vikubwa vya polisi vya jijini Dar es Salaam na msako ukaanza mara moja.
Baada ya uchunguzi kufanywa, iligundulika kuwa marehemu Wanze aliondoka na rafiki yake aliyemtaja kwa jina la Salha, jina alilokuwa akitumia katika mtandao wa Facebook ingawa jina lake halisi ni Jacqueline Clement Masanja.
Inadaiwa kuwa baada ya Wanze kufika Mlimani City, Salha alimuunganisha kwa wanaume wawili ambao ndiyo wanasemekana kumteka na ambao walikuwa wakiitumia simu yake kuwasiliana na ndugu zake akiwaambia wasiwe na wasiwasi kwani yupo salama akiwa na shoga yake huyo.
Wazazi na polisi walimtafuta Salha ili awaeleze alipo mwenzake lakini hakuatikana hadi walipokuja kuuona mwili wa marehemu Bonde la Msimbazi.
Wanze ni mpwa wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadick na mwili wake ulisafirishwa kwenda Mwanza kwa mazishi.
JACK NAYE ATOWEKA, AKUTWA AMEKUFA
Wakati msako wa kujua wapi alipo rafiki wa marehemu Wanze, Salha ukiendelea, taarifa za kusikitisha zilidai kuwa mwili wa msichana huyo nao uliokotwa wilayani Temeke akiwa ameuawa kikatili.
Habari kutoka kwa watu wa karibu na Jack zinasema wauaji wa Wanze walitambua kuwa ni mtu mmoja tu anayejua kuwa wao ndiyo walimuua Wenze na mtu huyo alikuwa Salha hivyo ili wabaki salama ilikuwa ni lazima wamuue pia Jack.
Uwazi lilipozungumza na Mecky Sadick ambaye alisema yeye ni mmoja wa familia ya wafiwa hawezi kuzungumzia chochote ila atakaporudi kazini ataliongelea suala hili.
MAREHEMU WALIKUTANAJE?
Marehemu Wanze na Jack walifahamiana kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook na baada ya urafiki wao kukolea, Jack alikuwa akimtembelea Wanze chuoni na alimtambulisha kwa wanachuo wenzake kama dada yake wa hiari ingawa wazazi wake hawakuwahi kumfahamu rafiki huyo.
Chanzo Global
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment