Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Matokeo  ya ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusiana na kuchotwa kwa Sh. bilioni 306 kifisadi kwenye akaunti ya Tegeta Escrow ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) umeiweka matatani Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), huku yakizitambua fedha hizo kuwa ni za umma.

Ofisi ya AG inadaiwa kuingia matatani, baada ya ripoti ya ukaguzi huo iliyovuja kubaini kwamba, inahusika moja kwa moja katika kuisababishia serikali hasara ya jumla ya Sh. bilioni 321 katika kashfa hiyo.

Pia Wizara ya Nishati na Madini, nayo inatajwa na ripoti hiyo kuhusika katika kuisababishia serikali hasara hiyo.

Vilevile, Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) nayo pia imeingia matatani, baada ya kuhusishwa na ripoti hiyo kwa tuhuma za kulikosesha shirika hilo kiasi hicho cha fedha.

Ripoti hiyo imo kwenye vitabu vitatu, ambavyo kila kimoja kina kurasa zaidi ya 300. Kitabu cha kwanza ni muhtasari wa ripoti na cha pili na tatu ni nyaraka za ushahidi. Ofisi ya AG inahusishwa na kashfa hiyo, baada ya ripoti hiyo kueleza kuwa ilivunja sheria makusudi kwa kuelekeza kuwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye gharama za uendeshaji (capacity charges), ambazo Tanesco walilipishwa na IPTL, isilipwe.

Maelekezo hayo ya ofisi ya AG yanadaiwa kusababisha serikali kupoteza mapato ya Sh. bilioni 21.

Aidha, Wizara ya Nishati na Madini inaguswa na taarifa hiyo kwamba ilisaini nyaraka kuidhinisha kutolewa fedha hizo kwenye akaunti hiyo bila kuhakikisha fedha za Tanesco zinarudi.

Hatua hiyo ya wizara hiyo inadaiwa kuipotezea Tanesco kiasi hicho cha fedha.

Nayo Bodi ya Tanesco inaguswa katika kashfa hiyo kwa madai kwamba, haikutimiza wajibu wake kwa kugeuza maamuzi yake na hivyo kulikosesha shirika kiasi hicho cha fedha.

Ripoti ya CAG inaigusa Bodi hiyo ikisema kwamba iligeuza maamuzi yake ama kwa kushinikizwa na wizara au kwa rushwa.

Ripoti hiyo imebainisha pia kuwa Wizara ya Nishati na Madini haikujiridhisha kuhusu uhalali wa umiliki wa IPTL.

Pia imebaini kuwa kampuni ya PAP haikununua kihalali asilimia 70 ya hisa za kampuni ya Mechmar katika IPTL kwa madai kwamba, zilizuiwa na mahakama.


Vilevile, imebaini kuwa kampuni hiyo (Mechmar) hawana hati halisi za hisa (share certificates).

Ripoti hiyo imebainisha pia kuwa PAP ilifanya udanganyifu mkubwa katika malipo ya kodi kwa kutoa nyaraka za uongo kuwa walionunua hisa kwa Sh. milioni sita, badala ya Dola za Marekani milioni 20 na kuikosesha serikali mapato ya Sh. bilioni 8.7.

Inabainisha kuwa fedha zilizokuwamo kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, ambazo ni jumla ya Sh. bilioni 306 ni matokeo ya Tanesco kulipishwa gharama za uendeshaji zaidi ya kiwango kinachotakiwa kulipwa.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa Tanesco walipaswa kurejeshewa Sh. bilioni 321 zilizolipwa ziada kwa IPTL kati ya mwaka 2002-2012.

Hivyo, fedha za akaunti ya Tegeta Escrow ni fedha za umma na kwamba, yote ilipaswa kurudi Tanesco na shirika kuendelea kuwadai IPTL Sh. bilioni 15.

Ripoti hiyo, ambayo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliikabidhi kwa Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, Ijumaa iliyopita, tayari imekwishakabidhiwa kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kwa ajili ya kuipitia.

Itawasilishwa bungeni Novemba 26, mwaka huu, ili kutoa fursa kwa wabunge kuijadili na kupitisha azimio juu ya yaliyomo.

KAULI YA ZITTO
Alipoulizwa jana, Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, alithibitisha kamati yake kukabidhiwa ripoti hiyo ya CAG na kusema bado anaisoma, kwani ina kurasa zaidi ya 1,000.

“Bado naisoma. Namshukuru sana CAG kumaliza kazi hii na kujibu hadidu rejea zote. Ni taarifa kubwa yenye majuzuu matatu (vitabu) kila juzuu ina kurasa zaidi ya 300,” alisema Zitto, ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini.

Kashfa ya Tegeta Escrow iliibuliwa bungeni na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila ambaye alisisitiza kwamba fedha hizo ni za umma na kwamba ziliondolewa na wezi kwa njia za utata. Kuibuliwa kwa kashfa hiyo, kulisababisha Kafulila kuingia kwenye malumbano makali katika kutoleana maneno ya dharau na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, bungeni.

Maneno hayo ya dharau yalihusisha Jaji Werema kumwita Kafulila kuwa ni tumbili na Kafulila kumwita Jaji Werema mwizi.Baadhi ya wabunge wamekuwa wakishinikiza wakitaka ripoti hiyo pamoja na ile ya uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) ziwasilishwe bungeni ili zikajadiliwe na wabunge ili ukweli ujulikane.

Tayari nchi wahisani zimetangaza kuikatia misaada serikali ya zaidi ya Sh. trilioni moja kutokana na kashfa hiyo.Hatua hiyo imeshaanza kulalamikiwa na baadhi ya viongozi wa serikali akiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye kwa nyakati tofauti amekuwa akieleza kuwa wahisani hawakufanya maamuzi sahihi kwa kuwa wamewaadhibu watu wengi wasiohusika.

Akaunti ya Tegeta Escrow ilifunguliwa kutokana na kutoelewana kuhusu gharama halisi na halali za umeme unaozalishwa na IPTL na kuuzwa Tanesco.

Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa (ICSID), katika uamuzi wake wa Februari 2014, ilitoa hukumu kuonyesha kwamba Tanesco walitozwa kiwango cha juu zaidi ya kilichopaswa kulipwa kwa IPTL.


Kwa uamuzi huo, ni dhahiri kwamba fedha zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye akaunti ya Escrow zilipaswa kugawanywa kwa IPTL na Tanesco baada ya hesabu kufanyiwa marekebisho upya kwa viwango halali, lakini badala yake fedha hizo zilitoweka ghafla kwenye akaunti hiyo.

Mjadala wa ripoti hiyo unatarajiwa kuwa mkali kutokana na wabunge wengi kulichukulia suala hizo kuwa ni kashfa kubwa ya upotevu wa fedha nyingi za walipakodi huku ukiwapo uwezekano wa baadhi ya vigogo kung’olewa katika nafasi zao kama njia ya kuwajibika ama kuwajibishwa.

Tangu suala hilo lilipoibuliwa na Kafulila, Serikali imekuwa ikitoa maelezo kupitia kwa viongozi wake wakuu akiwamo Waziri Mkuu Pinda, Jaji Werema; Waziri wa Nishati na Madini. Prof. Sospeter Muhongo, kuwa fedha hizo siyo za umma bali za wanahisa katika IPTL ambao fedha zao zilifunguliwa akaunti ya Escrow baada ya kuingia katika mgogoro.


Credit: Nipashe

Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala,

Hifadhi blog hii kwenye simu yako ili upate habari zote kwa urahisi zaidi

Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
http://www.facebook.com/kibonajoro

Post a Comment

 
Top