SHURA ya Maimamu Tanzania imetangaza hatua za kuikwamisha Rasimu ya Katiba inayopendekezwa, kwa kwenda kuwaeleza waumini wa dini ya Kiislamu kupiga kura ya hapana.
Hatua hiyo imekuja baada ya Rasimu ya Katiba inayopendekezwa iliyowasilishwa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Andrew Chenge, kuiweka kando Mahakama ya Kadhi. Jana mara baada ya kumalizika kikao cha maimamu wanchi nzima, Msemaji wa Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Rajabu Katimba, alisema hatua ya kupiga kura ya hapana ni moja ya azimio lililoafikiwa na kikao hicho.
“Msimamo wetu kwa asilimia 100 ni hapana, hatuungi mkono, tunalaani vikali jinsi mchakato huu wa Katiba ulivyovurundwa kwa sababu maoni ya Waislamu hayakuzingatiwa.
“Leo (jana) tulikuwa na kikao kilichojumuisha maimamu wote kutoka Tanzania na msimamo wetu katika hilo ni hapana,” alisema Sheikh Katimba.
Mbali na msimamo huo, Sheikh Katimba alisema mkutano huo pia umejadili mambo mengine mazito ambayo yatawekwa wazi hivi karibuni.
Sheikh huyo alisema wiki hii watakutana na vyombo vya habari ili kutoa tamko lao rasmi kuhusu Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.
Juzi na jana kumekuwa na ujumbe mfupi wa maneno (sms) uliokuwa ukisambazwa ambao ulisomeka hivi; ‘Assalam Alaykum, ndugu Muislam baada ya kukataliwa Mahakama ya Kadhi katika mchakato wa Katiba Mpya, Umoja wa Maimamu Tanzania (SHURA) wanakutana ili kujadili msimamo wa Waislamu kuipigia kura ya Ndiyo au Hapana mapendekezo ya Katiba Mpya’.
Chanzo kutoka ndani ya kikao hicho ambacho hakikutaka kutajwa jina lake, kilieleza masuala mengine mbali na azimio hilo la kukwamisha rasimu hiyo ya Katiba inayopendekezwa.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, kila imamu katika mkutano huo amepewa jukumu la kwenda kuzungumza na waumini wa msikiti wake na kuwaeleza ukandamizaji wa Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.
“Pamoja na hali hii, lakini kila mmoja wetu sasa tunakwenda kuwasha moto mikoani maana hili Bunge la Katiba limebeba ajenda zote zenye masilahi yao kisiasa kuliko hali halisi.
“Kwa hali hii kuanzia sasa unyonge umefika mwisho, maana kila mara Serikali imekuwa ikitumia ngao ya Watanzania wanyonge hasa Waislamu kupitisha mambo yao…. Kwa sasa kwa Katiba hii tutaikwamisha tu,” kilisema chanzo hicho.
Via Habari5Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment