Mahakama
ya hakimu mkazi Kinondoni jijini Dar es salaam imesitisha kwa muda
shughuli zake baada ya zomeazomea iliyosababishwa na umati mkubwa wa
watu waliofika mahakamani hapo kushuhudia kesi inayomkabili Amina Maige
aliyeshitakiwa kwa kosa la kumjeruhi binti kwa kumng'ata na kumuunguza
kwa pasi.Ndivyo hali ilivyokuwa katika mahakama hiyo mara
baada ya mtuhumiwa huyo kufikishwa mahakamani hapo akiwa chini ya ulinzi
mkali wa polisi ambapo kabla ya kuteremka kutoka ndani ya gari
alifunika uso wake na mtandio hali iliyosababisha umati huo kuanza
kupiga kelele wakitaka afunuliwe ili aonekane.
Hata mara
baada ya kuhifadhiwa katika chumba cha maabusu ya mahakama hiyo wakati
akisubiri kupandishwa kizimbani baadhi ya wanaharakati waliofika
mahakamani hapo nao walisikika wakilaani kitendo cha polisi kumsaidia
kufunika uso.
Zoezi
la kuwatuliza wananchi hao lilionekana kuwashinda askari wa jeshi la
polisi hali iliyowalazimu askari magereza kuingilia kati na kusaidiana
nao ili shughuli za mahakama ziweze kuendelea kama askari Mmoja
alivyosikika akiwaomba waondoke katika eneo hilo.
Akisoma
shitaka linalomkabili mtuhumiwa huyo wakili wa serikali Mohamed Salum
mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya Kinondoni Yohana Yongolo amesema
mtuhumiwa Amina Maige anakabiliwa na kosa la kumjeruhi vibaya Binti
Eusta Hashim kinyume na kifungu kidogo cha sheria 225, kosa
alililolitenda huko eneo la Mwananyamala Manjunju.
Wakili
Mohamed amesema upelelezi umekamilika ambapo mshitakiwa amekana shitaka
hilo na kurudishwa rumande baada ya mwendesha mashitaka huyo kumuomba
hakimu asimpatie dhamana kwa ajili ya usalama wake, ombi ambalo hakimu
alikubaliana nalo ambapo mtuhumiwa amerudishwa rumande hadi June 26
mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa kwa ajili ya masikilizo ya awali.
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment