Dar es Salaam. Kinyume na matarajio ya wananchi walio wengi ya kupata unafuu katika kodi za bidhaa mbalimbali, Bajeti ya Serikali iliyosomwa jana imekuwa ya maumivu kwao ikipendekeza wakamuliwe zaidi lakini ikaja na mikakati ya kudhibiti misamaha ya kodi na kupunguza matumizi.
Kinyume na bajeti ya mwaka jana
iliyoonekana ni ‘majanga’ kwa kila eneo, mwaka huu Serikali imetoa ahadi
za kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma katika ununuzi na
misamaha ya kodi ili kuhakikisha fedha hizo zinaelekezwa kwenye shughuli
muhimu za maendeleo na huduma za jamii.
Hayo yamo katika hotuba ya Bajeti iliyosomwa bungeni, Dodoma jana na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum.
Hata hivyo, uamuzi huo kama njia
ya kupate fedha zaidi umeelezwa kuwa ni ‘mzuri wenye tatizo la jinsi
gani ya kupima utekelezaji wake’.
Mhadhiri wa Shule ya Biashara ya
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Goodluck Urassa alisema kuna matatizo
makubwa ya uwajibikaji yanayoweza kuzorotesha nia njema ya kubana
matumizi na kudhibiti misamaha ya kodi.
Pia, katika hotuba hiyo kilio
cha muda mrefu cha wafanyakazi kutaka kupunguziwa kodi kwenye mshahara
hadi chini ya asilimia 10, kimeendelea kuwa kitendawili baada ya
Serikali kupunguza kwa asilimia moja tu, kutoka 13 hadi 12 huku Kima cha
Chini cha Mshahara (KCC), kikielezwa kwamba kitaongezwa lakini bila
kuwekwa wazi kwa kiwango gani.
Hotuba hiyo pia haikubainisha
vyanzo vipya vya mapato vilivyoainishwa, suala ambalo awali, lilizua
mvutano mkali kati ya Serikali na Kamati ya Bunge ya Bajeti.
Badala yake, imeendelea na utamaduni uleule wa kuzikamua kodi bidhaa zilezile zikiwamo soda, pombe, sigara na magari.
Hata hivyo, Waziri Mkuya alisema
Bajeti yake imelenga kupunguza gharama za maisha ya wananchi kwa
kuendelea na jitihada za kudhibiti na kupunguza mfumuko wa bei,
kuboresha huduma za jamii, miundombinu ya barabara, umeme na
umwagiliaji.
Kudhibiti matumizi
Mkakati kabambe aliokuja nao
Waziri Mkuya ni wa kuimarisha zaidi usimamizi na udhibiti wa matumizi ya
fedha za umma, kuongeza nidhamu ya matumizi na uwajibikaji kwa wadau
wote wanaotekeleza Bajeti ya Serikali.
Pengine jambo muhimu katika
mkakati huo ni kuunganisha matumizi yote ya Serikali, yaani wizara,
idara za Serikali zinazojitegemea, sekretarieti za mikoa, mamlaka za
Serikali za mitaa na wakala na taasisi za Serikali chini ya mfumo mmoja
wa udhibiti wa fedha za umma unaosimamiwa na Mlipaji Mkuu wa Serikali. Bonyeza hapa kuendelea kusoma
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment