Dar es Salaam. Homa
ya dengue inaendelea kushika kasi nchini baada ya takwimu za Januari
hadi juzi kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kuonyesha kuwa watu
376 wamekwishagundulika kuugua ugonjwa huo.
Mtaalamu wa Ufuatiliaji wa Magonjwa wa
wizara hiyo, Dk Janeth Mugamba alisema hadi jana watu wawili walikuwa
wamepoteza maisha, idadi ambayo alisema inaweza kuwa kubwa zaidi endapo
upimaji utafanyika katika kila wilaya. “Pengine idadi inaweza kuwa kubwa
zaidi kwa sababu wengi hawapimwi, Ijumaa (kesho) tutatoa, taarifa
zaidi,” alisema.
Alisema Wilaya ya Kinondoni ina wagonjwa
wengi zaidi, ikifuatiwa na Ilala na Temeke. Hata hivyo, alisema huenda
wilaya zenye idadi ndogo ya wagonjwa hazijaweza kupima na kubaini watu
wenye maradhi hayo ikilinganishwa na Kinondoni.
Juzi, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
Dk Seif Rashid alisema hali ni mbaya na wananchi wanatakiwa kuchukua
hadhari wasipate maambukizi ya ugonjwa huo.
Mtafiti wa malaria, tabia za mbu na
mazingira, wa Taasisi ya Afya ya Ifakara, Dk Nicholas Govela alisema
tayari wameshatuma maombi ya kufanya utafiti wa kina kuwajua mbu
wanaoeneza homa ya dengue nchini. “Utafiti huu utasaidia kujua ni mbu
kiasi gani wameathirika na virusi hivyo. Tukifanya hivyo tutajua ukubwa
wa tatizo, tutajua wanapatikana wapi zaidi na virusi vyao vimetokea
wapi,” alisema.
Dk Govela alisema ni lazima utafiti huo
ufanyike ili kudhibiti maambukizi zaidi ya homa hiyo akisema zipo sababu
kadhaa zinazohisiwa kusababisha maradhi hayo, ikiwamo ya wahamiaji
kuleta virusi hivyo vinavyosababisha homa hiyo na kuambukizwa kwa njia
ya kuumwa na mbu.
“Ugonjwa huu umeenea zaidi nchi za
Amerika ya Kusini na Kusini mwa Bara la Asia. Hapa kwetu mbu hawa
walikuwapo lakini ugonjwa wa dengue haukuwapo kwa kiasi hiki, ndiyo
maana sababu zinazohisiwa zaweza kuwa ni wahamiaji,” alisema.
Alisema maambukizi ya homa ya dengue
hutokea baada ya mtu mwenye ugonjwa huo kuumwa na mbu hao aina ya Aedes
Egyptiae na mbu hao wakichukua virusi, huvisambaza kwa watu wengine.
“Inawezekana tatizo ni kubwa zaidi ya hivi inavyofikiriwa kwa sababu
wanaokuja hospitali kupimwa na kugundulika ni wachache, wengi wasiofika
hawawezi kujulikana,” alisema.
Makazi duni hatarini zaidi
Daktari Kiongozi na Mtaalamu wa homa ya
dengue, Mrisho Rupinda alisema watu wanaoishi katika makazi duni wapo
hatarini kuathiriwa zaidi kwa sababu ya kuwapo kwa taka nyingi na
madimbwi.
Alitoa mfano wa wagonjwa wa kwanza
wilayani Kinondoni, akisema walitokea maeneo ya Kambangwa, Mwananyamala
Komakoma ambako kulikuwa na madimbwi na bwawa la maji.
“Wagonjwa wengi huonekana zaidi kwenye
makazi duni kwa sababu ya mpangilio mbovu na kuzagaa kwa taka. Lakini
pia maeneo mengine ambayo watu huhifadhi maji kwenye matenki au ndoo kwa
muda mrefu bila kuyafunika,” alisema.
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment