Kinyang’anyiro cha ubunge wa viti maalum katika mkoa wa Singida kimeibua mapya, baada ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Ikungi, Christina Hamis, kutishia kususia kuingia kwenye ofisi za jumuiya hiyo na kuhama chama.
Mwenyekiti huyo anakusudia kuchukua uamuzi huo kwa madai kuwa Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Aluu Segamba, anamlazimisha amuunge mkono mgombea ubunge wa Viti Maalumu (CCM), Wema Sepetu.
Christina alisema pamoja na kwamba yeye ni Mwenyekiti wa UWT wilaya, jambo linalomshangaza ni kuona mambo yasiyoridhisha yakifanyika ndani ya nyumba za mawakala wa mgombea ubunge huyo.
Alisema tangu mchakato umeanza amekuwa akipokea kauli za kashfa na matusi kutoka kwa watu wa karibu wa Wema akiwamo mama yake, Mariam Sepetu, kutokana na kutomuunga mkono mtoto wake.
Mariam Sepetu alipoulizwa kuhusu kutoa maneno ya kashfa kwa Mwenyekiti wa UWT, alisema hawezi kujibu mambo yoyote kuhusu kiongozi huyo.
Christina alisema kwa mara kadhaa amewasilisha malalamiko yake kwa Katibu wa CCM wilaya ya Ikungi, Segamba kuhusu matusi, kashfa na vitisho anavyopata, lakini hapewi ushirikiano.
“Nimemweleza Katibu wa Wilaya mambo nayofanyiwa, lakini niliishiwa kuambiwa siwezi kupata msaada wowote kwenye ofisi hiyo na kwamba niachane na Wema kwa sababu ameletwa na kiongozi mmoja mkubwa wa serikali, mawaziri na mtoto wa kigogo agombee ubunge,” alisema.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, maamuzi ya kugombea ubunge kwa Wema kumetokana na kushawishiwa na vigogo wa serikali na kwamba viongozi waliopo mkoani hapa wanatakiwa kumuunga mkono.
Christina alisema baada ya kuona hasaidiwi, aliwasilisha malalamiko kwa Katibu wa UWT Mkoa wa Singida, Anjela Mirembe, lakini jibu alilopatiwa ni kwamba Wema ameletwa na wakubwa na hivyo aachane naye.
Alipotakiwa kuzungumzia malalamiko ya mwenyekiti huyo wa UWT wilaya ya Ikungi, Mirembe alithibitisha kupokea malalamiko hayo kwa maneno, badala ya maandishi kama taratibu za kiutendaji wa kazi za kiofisi zinavyoelekeza na hivyo kushindwa kuyafanyia kazi.
Katibu wa UWT wilaya ya Ikungi, Yagi Kyaratu, alisema alipokea malalamiko hayo kutoka kwa mwenyekiti wake na kuyawasilisha kwa Katibu wa UWT mkoa wa Singida.
Katibu wa CCM wilaya ya Ikungi ambaye pia ni kaimu katibu wa CCM Mkoa wa Singida, Segamba, alipotafutwa ili aweze kujibu tuhuma zilizoelekezwa kwake alijibu kuwa yupo kwenye kikao.
Kwa upande wake, Wema alipotafutwa jana, simu yake hukupatikana na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi, hakujibu hadi tunakwenda mitamboni.
CHANZO: NIPASHE
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment