Licha ya Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kukanusha mara zote kwamba, hahusiki na kusambaratika kwa ndoa ya Mwimba Injili Flora Mbasha na mumewe, Emmanuel Mbasha, lakini mume huyo ambaye amekuwa akimshutumu Gwajima ameibuka na jipya.
Jipya aliloibuka nalo Mbasha ni kudai kuwa, msala uliompata Mchungaji Gwajima wa kumtolea maneno yenye kuudhi Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycap Kadinali Pendo na kisha kuhojiwa polisi na kupata mshtuko, kuzimia hadi kulazwa hospitali ni malipo ya Mungu kwake kutokana na kilio chake.
Akizungumza na Amani kwa njia ya simu kwa dakika 15 juzi, Mbasha alisema: “Ile hali (kupoteza fahamu) ya Gwajima ni malipo. Mimi nilishasema jamani, mtu akikutendea ubaya malipo ni hapahapa duniani, hakuna kwingine.
“Mimi ndoa yangu haipo, mke wangu anajua yeye anavyoishi. Kwa hivyo mimi nimekuwa nikiishi kwa manung’uniko kila siku, unadhani nini kitatokea kwake?”
Mbasha alikwenda mbele zaidi kwa kutoa tamko na agizo kwa mchungaji huyo kwa kusema:
“Tena namwomba Mungu ampe afya Gwajima, akitoka hospitali alikolazwa (TMJ, Dar) anitafute kuniomba msamaha.
“Ni vyema na itakuwa vyema zaidi akinitafuta na kuniomba msamaha ili kila mmoja aishi kwa amani. Mimi nisiwe na kinyongo na yeye na wala yeye asiwe na kinyongo na mimi.”
Mbasha hakumalizia hapo, alipoulizwa kama kauli ya Gwajima iliyosababisha mtafaruku ilikuwa sawasawa au la! Mbasha alisema:
“Hilo atajua yeye mwenyewe na Mungu wake, mimi sijui. Ila ninachojua mimi ni kitu kimoja tu, kwamba Mungu amenilipia basi, sasa aniombe msamaha.”
Naye mchungaji mmoja wa kanisa la Gwajima alipopatikana kwa simu na kuulizwa kuhusu madai ya Mbasha, alisema:
“Yule hajui maandiko sawasawa. Hakuna uhusiano wowote kati ya kilichompata mchungaji wangu na hisia zake kuhusu mkewe Flora.
“Yule hajui maandiko sawasawa. Hakuna uhusiano wowote kati ya kilichompata mchungaji wangu na hisia zake kuhusu mkewe Flora.
“Gwajima na Flora hawana uhusiano wowote usiofaa. Sasa yeye anaposema kalipiwa, kalipiwa kitu gani? Mungu anaweza kulipa jambo la hisia?”
Wiki mbili zilizopita, kwenye Viwanja vya Tanganyika Perkers ambako kuna kanisa, Gwajima alitoa mahubiri yaliyolenga kumshutumu Kadinali Pengo kwa kitendo chake cha kwenda kinyume na maazimio ya Baraza la Maaskofu Tanzania kuhusu msimamo wao wa Mahakama ya Kadhi nchini.
Hali hiyo ilimfanya Gwajima kuitwa Polisi Kituo cha Kati, Dar na kuhojiwa. Akiwa katika mahojiano, ghafla alisikia kizunguzungu, akaanguka na kupoteza fahamu. alikimbizwa katika Hospitali ya Polisi Baracks kisha Hospitali ya TMJ, Dar kwa matibabu zaidi.
Juzi, Gwajima aliruhusiwa kutoka hospitalini hapo lakini akachukuliwa hadi Kituo cha Polisi Oysterbay kwa mahojiano zaidi na kuachiwa kwa dhamana.
Credit: Amani/Gpl
Credit: Amani/Gpl
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment