Katika hali inayoashiria ukubwa wa
tatizo la ajira katika sekta rasmi nchini, juzi wasomi wa ngazi ya Chuo Kikuu
10,500 walijitokeza jana (pichani) kwenye usaili wa Idara ya Uhamiaji nchini inayohitaji
kuajiri watu 70 tu.
Wengi wakiwa ni vijana wasomi wa
fani mbalimbali wenye umri wa kati ya miaka 22 na 30, walifurika kwenye uwanja
huo uliopo Kurasini, katika Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam kuanzia saa 12
asubuhi.
Idadi hiyo inahusisha waombaji wa
ajira walioitwa na idara hiyo kutoka kundi la waombaji 20,000.
Idadi ya waombaji hao walijiotokeza
katika usaili huo ilithibitishwa na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi, Isack Namtanga, aliyekiri ni usaili wa kihistoria kutokana na kuhusisha
waombaji wengi kwa wakati mmoja.
“Kwa kweli huu ni usaili wa
kihistoria, hatujawahi kupata maombi mengi kama haya, wote waliotuma ni wale
wenye sifa kielimu ambayo ni kuwa na shahada ya kwanza ya fani tulizozitaja
hapo awali,” alisema.
Alifafanua kuwa, Wizara kupitia
matangazo ya nafasi hizo za ajira katika vyombo vya habari yaliyotolewa mapema
mwanzoni wa mwaka huu, yaliainisha nafasi zinazohitaji watu na sifa zake ambapo
katika nafasi ya kwanza ni ya Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji iliyohitaji watu 70.
Sifa za nafasi hiyo ni pamoja na
waombaji kuwa na elimu ya Shahada ya Kwanza katika fani za Uchumi, Biashara,
Utawala, Uandishi wa Habari, Ualimu, Usafirishaji, Rasilimali Watu na Sayansi
ya Kompyuta.
Nyingine ni Habari na Mawasiliano,
Takwimu, Uchapaji, Uhandisi Majengo na Uhandisi Mitambo.
“Na masharti yalitaka waombaji hao
wawe na umri usiozidi miaka 35, jambo ambalo waombaji wote 20,000 waliotuma
maombi yao walikuwa na sifa hizo hivyo ikabidi wachujwe ili kupata waombaji
watakaoitwa kwenye usaili.
“Hii inaonesha kuna uhaba mkubwa wa
ajira, na waombaji wote wana sifa hiyo ya shahada na umri, sasa tulifanya
usaili kwa makini tukapata hao zaidi ya 15,000 tumejitahidi na tumewaita wengi
ili waje wachuane kwenye usaili tupate hao 70,” alisema Namtanga.
Akizungumzia jinsi watakavyopata
waombaji wenye sifa ikiwa wote waliotuma maombi wanasifa tajwa, Namtanga
alisema pamoja na kuangalia sifa ya elimu, lakini pia wataangalia na ufahamu wa
mambo mengine ya kijamii.
Alisema hiyo ni ili kupata
waombaji wenye upeo mkubwa hasa kwa kuwa wengi wao wana sifa kielimu, hivyo
kuitwa kwao kwa wingi ni kutoa mwanya kwa wao kuchuana kwa uwazi na kupata
waombaji kwa haki.
Kwa upande wa waombaji hao, baadhi
ya waliozungumza na gazeti hili baada ya kutoka kwenye usaili huo walisema, ni
usaili mgumu kwani una ushindani wa hali ya juu.
“Sijawahi kufanya usaili wa watu
wengi kama huu, nafasi zinazohitajika ni 70, ila tulikuwa zaidi ya 10,000 sasa
unaona wazi kwamba ni lazima ufanya kwa makini ili kushindania nafasi hizo”,
alisema mmoja wa waombaji hao ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.
Aliongeza, hali hiyo inaonesha jinsi
gani vijana wengi wana uhaba wa ajira, kwani kwa nafasi hizo 70, maombi ni
mengi na yanavunja historia ya usaili wa nafasi nyingine mbalimbali zilizowahi
kutangazwa.
Alisema katika usaili huo,
waliufanya kwa kugawanywa kwenye makundi mawili, ambapo walitumia Uwanja wa
Taifa kufanyia kwa kuketi kwenye viti vya watazamaji mithili ya waliokuwa
wanaangalia pambano la soka kwenye uwanja huo wa kisasa wa michezo nchini.
Kuhusu usimamizi na ulinzi wakati wa
usaili, mmoja wa wasaili hao alisema wasimamizi walikuwa wa kutosha wakiongozwa
na Maofisa kutoka Uhamiaji, Magereza na baadhi ya maofisa kutoka Utumishi.
“Usimamizi ulikuwa mzuri na
walikuwepo wasimamizi wa kutosha, tulifanya kwa makundi mawili moja lilikuwa
chini uwanjani na wengine walipanda juu kwenye jukwaa la watazamaji, tulifanya
mtihani wa kuandika, ulikuwa mzuri tu, ndio tusubiri tuone majibu,” alisema
mmoja wa waombaji hao aliyeshukuru magazeti na vyombo vya habari kwa ujumla kwa
mchango wao mkubwa katika kuihabarisha jamii juu ya masuala mbalimbali ikiwa
pamoja na nafasi za ajira zinazotangazwa.
Hata hivyo Namtanga alisema , baada
ya usaili huo kukamilika, watafanya uchambuzi na watachagua watu waliofanya
vizuri kwa ajili ya usaili wa pili wa kuzungumza.
“Tumejipanga vizuri, tunategemea
kazi hii itafanyika kwa utulivu na tutapata watu wenye sifa na ufahamu wa mambo
ya kijamii kwani ni moja ya sifa ya ziada,” alisema Namtanga.
Alisema watakaopata nafasi hizo
watakuwa na majukumu mbalimbali yakiwemo kusimamia doria sehemu za mipakani,
bandarini vituo vya mabasi, kusimamia shughuli za upelelezi, kuandaa hati za
mashtaka, kukagua na kusimamia hati za safari na majukumu mengineyo.
Wakati wasomi hao wakionesha kiu ya
ajira katika sekta rasmi, katika miaka ya hivi karibuni imekuwa ikisisitizwa
umuhimu wa wasomi kujiajiri kutokana na ajira rasmi kuwa na nafasi chache, si
kwa Serikali ya Tanzania pekee, bali kote duniani.
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment