Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imebaini taarifa mbalimbali zinazozungumzwa na ambazo zimetolewa katika baadhi ya vyombo vya habari kuhusu zoezi la usaili wa nafasi ya Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji lililofanywa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi tarehe 13 katika Uwanja mpya wa Taifa, Dar es Salaam.
Wizara ingependa kutoa ufafanuzi kuhusu baadhi ya tuhuma zilizotolewa na baadhi ya wadau kama ifuatavyo:
1. RUSHWA
Tuhuma
za rushwa zinazoambatanishwa na zoezi hili ni hisia tu za wahusika
kwani, kwanza hazina ushahidi, na pia usaili ulifanywa kufuatana na
kanuni na sheria zinazosimamia ajira za watumishi wa Umma.
2. ULINZI
Katika
Uwanja wa Taifa kulikuwa na Maafisa mbalimbali toka Taasisi za Wizara
ya Mambo ya Ndani ya nchi ambao walikuwepo kuhakikisha kuwa zoezi hilo
linafanyika kwa usalama.
3. WINGI WA WASAILIWA
Nafasi
za Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji zilitangazwa katika magazeti na Tovuti
ya Wizara na Idara ya Uhamiaji kufuatana na taratibu Serikali
zinazosimamia ujazaji wa nafasi za kazi katika utumishi wa umma kwa
lengo la kuiweka wazi kwa umma wa Watanzania na matokeo yake wahitimu
zaidi ya 20,000 walitumia haki yao ya msingi kuomba nafasi hizo.
Kufuatana
na wingi wa waombaji, Wizara ilifanya zoezi la mchujo wa awali ambao
hatimaye ulibakiza kiasi cha maombi 10,000 yenye waombaji wenye sifa
zinazohitajika.
Aidha
kutokana na wingi huo, na haki ya kila muombaji ya kupatiwa nafasi ya
kushindania nafasi hizo, ilibidi Wizara ifanye utaratibu wa kutafuta
eneo lenye nafasi ya kutosha ya kuweza kuwapokea wasailiwa, ambalo
hatimaye ilionekana iwe Uwanja mpya wa Taifa.
Wingi
wa wasailiwa ni matokeo ya kidemokrasia ya kutoa nafasi kwa kila raia
kushindania nafasi za ajira zinazotolewa nchini ili mradi awe na sifa.
4. BAADHI YA WASAILIWA KUTOKUWA NA KALAMU
Maandalizi
ya usaili ni pamoja na kuwa na vifaa vya kawaida vya kushiriki usaili
hivyo msailiwa aliyefika katika eneo la usaili akiwa mikono mitupu ni
yule ambaye hakujiandaa, wala kuwa na kalamu haihitaji kutangaziwa.
5. UFINYU WA ENEO
Uwanja
mpya wa Taifa Dar es Salaam una uwezo wa kukaliwa na watu 60,000 hivyo
idadi ya wasailiwa 10,000 waliokuwapo uwanjani hapo haikuwa tishio kwa
usalama wao.
MWISHO
Nia
ya Wizara haikuwa kuleta usumbufu kwa mtu yeyote ila kutoa nafasi sawa
kwa walioleta maombi kushindania nafasi zilizotangazwa.
Imetolewa na:
Sgn
Isaac J. Nantanga
MSEMAJI WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
14 JUNI, 2014
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment