ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mhandisi William Mhando, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kuwa mshitakiwa wa pili (Eva Mhando) katika kesi ya matumizi mabaya ya madaraka, si mke wake.
Mhandisi Mhando alitoa madai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Frank
Moshi, alipokuwa akisomewa maelezo ya awali katika kesi hiyo na Wakili
wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai.
Mhando alikiri maelezo kuwa alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco tangu
Juni 2010 hadi 2012, lakini alikana maelezo kuwa mshitakiwa wa pili (Eva
Stephen Mhando) ni mkewe ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya
Santa Clara Supply Limited.
Kwa upande wake, Eva alikubali kwamba aliwahi kuajiriwa na Tanesco
kuanzia mwaka 1982 hadi 2009, mshitakiwa wa tatu, France Mchalenge pia
alikubali kwamba alikuwa mwajiriwa wa shirika hilo, wakati uchunguzi
unafanyika alikuwa mhasibu mkuu na alikuwa mjumbe wa Kamati ya Tathimini
ya Zabuni namba Pa/001/11/HQ/G/011 ya vifaa vya ofisi, ikiwemo printa
na kompyuta.
Swai alidai mshitakiwa wa nne, Sophia Misidai aliajiriwa na Tanesco
na wakati uchunguzi unafanyika alikuwa mhasibu mkuu na mjumbe wa kamati
iliyofanya tathimini ya zabuni ya kusambaza vifaa vya ofisi katika
shirika hilo. Mshitakiwa alikubaliana na maelezo hayo.
Mshitakiwa wa tano, alikubali kwamba alikuwa mwajiriwa wa Tanesco na
kuwa wakati wa uchunguzi alikuwa ofisa usambazaji na alikuwa mjumbe wa
kamati iliyotathimini zabuni hiyo.
“Mheshimiwa Hakimu, Kampuni ya Santa Clara Supply Ltd inamilikiwa na
Eva Stephen William, Fred William na Veronica Stephen Mhando, ilipata
zabuni ya kusambaza vifaa vya ofisi yenye thamani ya sh milioni 884.5.
“Mhando akiwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo na Eva akiwa Mkurugenzi
Mkuu wa Santa Clara Supply Ltd alisaini barua ya kuipa zabuni huku
akijua wazi kwamba kampuni hiyo inamilikiwa na familia yake, pia
hakujitoa kuonyesha kwamba ana maslahi na kampuni hiyo,” alidai.
Wakili Swai aliendelea kueleza kuwa Mhando aliwapa zabuni hiyo
mshitakwa wa pili, Eva na watoto wake kinyume na utaratibu, walitaka
kuiuza kampuni hiyo kwa mtu mwingine wakati tayari walishapata zabuni ya
kusambaza vifaa hivyo vya ofisi, mshitakiwa wa kwanza (Mhando) alitumia
madaraka yake vibaya kwa kushindwa kuonyesha kwamba ana maslahi binafsi
na Kampuni ya Santa Clara,” alidai Swai.
Swai alidai kwamba Eva alighushi taarifa za ukaguzi wa hesabu za
Kampuni ya Santa Clara ya mwaka 2007/2008 akionyesha kuwa Kampuni ya
Finx Capital House ilifanya ukaguzi.
Pia mshitakiwa huyo alighushi taarifa ya kuhamisha hisa akionyesha
hisa 200 zenye thamani ya sh 10,000 zilihamishiwa kwa Eveta Shing’oma.
Eva alidaiwa kutoa taarifa ya ukaguzi wa fedha kwa Katibu wa Bodi ya
Zabuni wa Tanesco akionyesha zilifanyiwa ukaguzi Desemba, mwaka 2010,
akajipatia sh milioni 37.7 kutoka kwa shirika hilo.
Swai alidai Mchalange, Misidai na Naftali Kisinga walitoa taarifa
katika Bodi ya Zabuni kuonyesha kwamba Kampuni ya Santa Clara walikuwa
wana sifa ya kupata zabuni hiyo, walipata mkataba wa kusambaza vifaa vya
ofisini wenye thamani ya sh 884,550,000. Washitakiwa hao walikana
maeneo yote hayo.
Wakili Swai alieleza upande wa jamhuri unatarajia kuleta mashahidi 14 na wanawasilisha mahakamani vielelezo 18.
Hakimu Mushi aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 29 na 30 mwaka huu, itakapokuja kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment