NYUMBA ya Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), John Heche, iliyopo Mabibo Loyola,
jijini Dar es Salaam, imevamiwa na watu wasiojulikana, ambapo vitu
vyenye thamani ya zaidi ya sh milioni 10 vimeibwa.
Tukio hilo limetokea wiki iliyopita muda mfupi baada ya Heche kutoka
nyumbani kwake alfajiri kwenda katika kituo cha mabasi ya mikoani cha
Ubungo, kuwahi usafiri wa kwenda jijini Mwanza.
Tayari tukio hilo limeripotiwa katika Kituo cha Polisi Mabibo Mwisho
na kupewa kumbukumbu namba MAB/RB/225/2014, kabla ya kuhamishiwa
katika Kituo cha Polisi Urafiki na kupewa namba URP/RB/2785/2014.
Hata hivyo tukio hilo limeanza kuhusishwa na masuala ya kisiasa
hususan katika vitu vinavyodaiwa kuibwa na namna Jeshi la Polisi Kituo
cha Urafiki wanavyolishughulikia.
Vitu vilivyoibwa ni pamoja na Friji, radio, TV, Decoder ya Dstv, jezi
za mpira jozi 32, mipira 56, magodoro, meza ya TV na music system
inayotumika kwenye mikutano ya hadhara.
Hadi sasa tayari mtuhumiwa mmoja anayedaiwa kuhusika na tukio hilo
amekamatwa na kukiri kuhusika na tukio hilo pamoja na wenzake ambao bado
wanaendelea kusakwa.
“Yule aliyekamatwa amekiri mbele ya Polisi kuhusika na tukio na
akawataja wengine sasa tunashangaa kigugumizi cha Polisi katika hili ni
nini mpaka wanashindwa kuwafuatilia na kubaini sababu zilizowafanya
waibe hapa,” alisema mmoja wa majirani wa Heche.
Kauli ya Heche
Heche ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA alipoulizwa iwapo
anaweza kulihusisha tukio hilo na shughuli zake za kisiasa, alisema ni
mapema kuhusisha tukio hilo na siasa moja kwa moja.
“Silihusishi moja kwa moja na siasa lakini namna askari wa Kituo cha
Polisi Urafiki wanavyolichukulia kiwepesi ndiyo inanipa shaka,” alisema
Heche
Kauli ya RPC Wambura
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP Camilius Wambura,
alipoulizwa kama analijua tukio hilo alisema hana taarifa nalo na kwamba
atafuatilia kujua kama lipo.
>>>>>Tanzania daima
Hifadhi blog hii kwenye simu yako ili upate habari zote kwa urahisi zaidi
Post a Comment
Post a Comment