MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Chalinze kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ridhiwani Kikwete amewataka wakazi wa Chalinze kupuuza hoja inayotolewa na mgombea wa Chadema kuwa yeye si mkazi wa Chalinze.
Ridhwani alisema hayo jana wakati
akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kurejesha fomu za
kugombea Ubunge wa jimbo hilo. Mgombea Ubunge wa Jimbo la Chalinze kwa
tiketi ya Chadema, Matayo Torongey, alinukuliwa akisema kuwa Ridhwani
hawezi kugombea Ubunge Chalinze kwa kuwa si mkazi wa jimbo hilo.
Katika mazungumzo yake na waandishi wa
habari, Ridhwani alionesha kushangazwa kuwa iweje akashifiwe kuwa yeye
si mkazi wa Chalinze.
“Yani (Torongey) anaweza kuniambia kuwa
mimi sio mkazi wa Chalinze? Hii inachekesha sana kwa kuwa kwanza ni nani
asiyejua kuwa mimi mzaliwa kabisa wa huku?” Alihoji Ridhwani.
Aliongeza kuwa ili kuwahakikishia wakazi
wa Chalinze maendeleo, wagombea wanatakiwa kutangaza sera
zinazotekelezeka na kuacha kutoa kauli zenye nia ya kuwapumbaza wakazi
wa Chalinze.
Alisema kuwa hatotaka kutumia muda wake
kufanya kampeni za kiubabaishaji kuanza kulumbana na kukejeli, kwa kuwa
amekuwa katika misingi mizuri ya kisiasa.
Alisema hajatokea chumbani kugombania
Ubunge, badala yake amekuwa katika misingi ya kisiasa tangu mdogo na
amechukua uamuzi wa kuingia katika siasa kwa lengo la kusaidia wananchi.
“Najua awali wakazi wa eneo la Chalinze walikuwa wachache sana na kwa sasa kuna ongezeko kubwa la wakazi wa Chalinze hivyo hata mahitaji nayo yanaongezeka,” alisema Ridhwani.
Aliongeza kuwa ongezeko hilo
limesababisha kuongezeka kwa mahitaji ya huduma mbalimbali kama hizo za
kijamii na kuongeza kuwa akiwa Mbunge atatatua kero hizo.
“Watu wanadhania kuwa mimi nimetokea
chumbani kuja kwenye siasa… hapana yaani tena hata sio kwa sababu ya
kuwa mimi ni mtoto wa Rais ndio nimeona ngoja nije kuuza sura huku, sio
ila ni kwa sababu nimekulia katika mazingira haya na ninaona kuwa ni
wakati wa kutatua kero za wakazi wenzangu wa huku,” alisema Ridhiwani.
Kuhusu tatizo la migogoro katika jimbo
hilo, alisema anaona kuwa analo jukumu kubwa la kuendelea kushiriki
katika kutatua kero zao ambazo CCM kwa muda mrefu imekuwa ikifanya
hivyo.
Alisema atakuwa na haki ya kupata mikosi iwapo akipuuzia kutatua kero ya muda mrefu ya wafugaji na wakulima.
Ridhwani anatarajia kuzindua rasmi
kampeni zake Jumamosi ijayo katika jimbo la Chalinze lililoachwa wazi
kutokana na kifo cha aliekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Said Bwamdogo.
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment