BAADHI ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wamewaonya wenzao ambao wamepanga kumzomea Rais Jakaya Kikwete wakati akitarajiwa kulihutubia bunge hilo kesho.
Onyo
hilo walilitoa jana mjini Dodoma wakati wa semina maalum ya kupitia
kanuni za bunge hilo, iliyofanyikia katika ukumbi wa Bunge.
Akichangia
katika semina hiyo mmoja wa wajumbe hao, James Mbatia, alionya taarifa
za kuwepo kwa mkakati wa kupanga kumzomea Rais Kikwete, atakapolihutubia
Bunge kesho.
Mbatia alisema, Rais anaongoza watu wote, ingawa ana chama cha siasa kwa mujibu wa sheria hivyo ni lazima asikilizwe.
“Tumesikia wapo wenye mkakati wa kumzomea Rais atakapokuja hapa,” alisema Mbatia.
Aliwataka
wajumbe wenzake waache fitina, kuzomeazomea na badala yake wavumiliane
ili waweze kuvuka salama huku akisisitiza kuwa, kauli ya umma ni kauli
ya Mungu.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, alionya vinara wa
fujo na kusisitiza kuwa hawataachwa salama kwani kuna kamera maalumu
ambazo zitatumika kukusanya ushahidi.
“Kamati ya Kanuni Madhubuti zitafanyakazi na hatutakubali kuahirisha Bunge huku watu wakilipwa posho,” alisema Mwenyekiti huyo.
Alisema,
ndani ya Bunge hilo kuna kamera 12 ambazo zinanasa kila tukio, hivyo
ushahidi huo utakusanywa na kuupeleka kamati ya maadili kwa ajili ya
uamuzi.
Mbali
na hayo Mwenyekiti huyo hakusita kutamka wazi kuwa ndani ya Bunge hilo
kuna vinara wa vurugu ambao watahakikisha wanashughulikiwa pindi
watakapojitokeza wakati Rais Kikwete akihutubia.
Naye
Julius Mtatiro ambaye ni miongoni mwa wajumbe wa bunge hilo alisema,
hatarajii kama kuna mtu yeyote anayetaka kufanya jambo lolote.
Alisema,
Rais ana dhamira nzuri na mchakato wa kuwapatia Watanzania Katiba Mpya,
hivyo hatarajii jambo jingine lolote zaidi ya kumsikiliza Rais Kikwete.
Wakati huo huo, Mtatiro alitolea mfano alivyotukanwa matusi mabaya na mmoja wa wajumbe pale alipokuwa akisimama na kupiga meza.
Alisisitiza
kwamba, kila mmoja aelewe kuwa wapo bungeni hapo kwa ajili ya kutunga
Katiba ambayo ni tendo la maridhiano na maelewano na wajumbe waweke hilo
mbele.
Akijibu
hilo, Mwenyekiti wa bunge hilo, Sitta alisema kusimama na kupiga meza
huo nao ni udikteta, kwani mjumbe haruhusiwi kusimama bila kuruhusiwa.
Sitta, alisema hatavumilia udikteta wa aina yoyote uwe wa wengi au wachache.
Wakati
huo huo, Kada wa siku nyingi wa CCM na Mjumbe wa Bunge la Katiba,
Kingunge Ngombale Mwiru, amesema Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, imeshindwa kuweka misingi ya
kujenga muungano badala yake inataka kuuvunja.
Kingunge
ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja baada ya Jaji Warioba kuwasilisha
Rasimu ya Pili ya Katiba katika Bunge la Katiba Mjini Dodoma, huku
akiendelea kutetea msimamo wa Tume yake wa kupendekeza muundo wa
Serikali tatu.
Akihojiwa
jana katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Kituo cha
Utangazaji cha Televisheni ya Taifa (TBC1) Kingunge, alisema mahali
popote alipo binadamu lazima kuwepo kero na changamoto.
Hata
hivyo alisema changamoto hizo haziwezi kuvunja muungano. Alitoa mfano
akisema kwa nchi za Afrika, Tanzania ni nchi ya kuigwa kutokana na kuwa
kisiwa cha amani.
Kingunge
alisema ameshangazwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoa mapendekezo
bila kuangalia matokeo ya muundo ambao utasambaratisha uzalendo.
"Tume
wao wamemaliza kazi yao wameandika maandishi mengi, lakini Bunge Maalum
la Katiba ndilo linalochagua Katiba ambayo itapendekezwa na wananchi,"
alisisitiza Kingunge.
Aliwataka
wajumbe wa Bunge hilo kutuliza vichwa vyao, kwani rasimu hiyo
haiandikwi na wajumbe wala chama chochote na kwamba hakuna mtu anayeweza
kwenda Ikulu bila kuchaguliwa na wananchi.
Kada
huyo wa CCM aliwataka Watanzania kuwa makini na watulivu na kuliachia
Bunge tukufu kazi ya kutunga katiba kwani ndilo linawakilisha wananchi
na Serikali.
Alishauri
Watanzania watulie na kuangalia Katiba ambayo imeachwa na waasisi kwa
miaka 50 imeleta mafanikio gani. Alisema Tanzania ni Taifa kubwa na
lengo la kupigania uhuru ni kuungana kumuondoa mkoloni.
"Katiba
mpya kwanza tukubaliane si mradi kupata katiba, tuwe na lengo la kupata
katiba iliyo bora na kabla ya kupata hiyo mpya tuangalie katika miaka
ya 50 tumeweza kupata mafanikio makubwa kiasi gani kwa Katiba ya zamani
chini ya mwasisi Mwalimu Julius Nyerere," alisema.
Kwa
upande wake Mjumbe wa Bunge la Katiba kutoka Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar, Pandu Amir Kificho, alisema kama mwakilishi wa Serikali ya
Zanzibar wanapendekeza Serikali mbili.
Kificho
alisema jambo la Muungano limedumu ndani ya miaka 50 na lengo kuweka
muungano uliyo bora zaidi, lakini changamoto zilizokuwepo ingetumika
utaratibu wa kuziondoa kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano.
"Mimi
kama mwakilishi kutoka Zanzibar tunachagua Serikali mbili na katika
Bunge hili kuna Wawakilishi kutoka Zanzibar wa CCM na CUF wanataka
Serikali mbili ziweze kuendelea kama msimamo wao wa Baraza la
Wawakilishi wa CCM," alisema.
Alisema
kuundwa Serikali tatu ni mzigo na zitaleta machafuko hatimaye kuyumba.
Alisema katika nchi tatu moja ikiyumba, lazima idondoshwe.
"Naitupia
lawama Tume ya Rasimu ya Katiba kwa kupendekeza na kuchagua Serikali
tatu halafu katika rasimu yao hawajaelezea faida ya kuchagua Serikali
tatu au Serikali mbili, jicho lao alijaangalia mbele,"alisema
Wakati
huo huo, Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini imeunga mkono muundo wa
Serikali tatu zilizopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba katika Katiba
mpya.
Akizungumza
na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam jana, Msemaji Mkuu wa
Taasisi hiyo, Rajabu Katumba, alisema ni vyema zikawepo Serikali tatu ya
Tanganyika, Zanzibar na Serikali ya Muungano.
Alisema
kuwepo kwa Serikali hizo kutatatua kero nyingi zinazojitokeza katika
kipindi hiki cha uwepo wa Serikali mbili. Alisema Serikali ya Tanganyika
na Zanzibar zijitegemee wakati ile ya Muungano iwe na Rais wa Muungano
atakayeratibu na kusimamia makubaliano ya muungano huo.
Aidha alisema Katiba Mpya ya Serikali tatu ni muhimu pia izingatie kero za waislamu zilizodumu kwa miaka 50.
Alisema
kama Waislamu walipendekeza Katiba Mpya ya Serikali tatu, itambue uwepo
wa Mahakama ya Kadhi ili kusimamia kwa mujibu wa sheria za Kiislamu
mambo yanayohusu Waislamu kama ilivyo nchi zingine za Afrika, Asia na
Ulaya.
Pia
alisema walipendekeza rasimu hiyo itambue rasmi siku ya Ijumaa kwamba
wafanyakazi na wanafunzi wapewe fursa ya kutosha kufanya ibada kama
ilivyo kwa Wakristo.
"Tulipendekeza
kwamba baada ya Serikali kutambua uwepo wa muumba, isiegemee upande
wowote wa dini bali iwepo kwa ajili ya kulinda maslahi ya wenye dini,"
alisema Katumba.
Alisema
wanaikumbusha Serikali kwamba Waislamu ni wapenda amani na wapo tayari
kusaidia kama wadau wakuu wa amani, lakini wanatahadharisha kwamba amani
ya kweli itapatikana tu pale ambapo haki ya wote itapatikana.
"Ni muhimu kwa Serikali kuyatafakari kwa kina mapendekezo yetu yakiwemo ya Katiba Mpya ya Serikali tatu," alisema.
CHANZO >> Majira
CHANZO >> Majira
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment