Hatua hiyo inatokana na mbio za kutaka kumrithi Rais Jakaya Kikwete kabla ya chama kupuliza kipenga.
Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amepongeza uamuzi wa
Kamati Kuu ya CCM kwa kuwapa adhabu ya onyo kali wanachama wake sita
akiwamo mwenyewe kwa kosa la kuanza kampeni za urais mwaka 2015 mapema
kabla ya muda.
Waziri Membe ni miongoni mwa wanachama sita
waliohojiwa na kupewa onyo kali kwa kuanza kampeni mapema. Hata hivyo,
kwenye mkutano wake na waandishi wa habari jana, alikataa kuulizwa
maswali.
Vigogo wengine waliopewa onyo ni Mawaziri wakuu
wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira.
Wengine ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini,
William Ngeleja.
“Napongeza kwa hatua iliyochukuliwa na Kamati Kuu,
kila chama lazima kifuate utaratibu wa kupata viongozi wake,” alisema
Waziri Membe.
Alisema utaratibu wa kuwapata viongozi
usipofuatwa, utaiingiza nchi kwenye vurugu na kusababisha machafuko.
Alisema uamuzi huo umeonyesha kwamba CCM ina utaratibu wake wa kupata
viongozi na kwamba, adhabu hiyo inaonyesha baadhi ya wanachama akiwamo
yeye (Membe) walikuwa wamekiuka.
Akitoa mfano, Waziri Membe alisema Kanisa Katoliki lina utaratibu mzuri wa kumpata kiongozi wake mkuu ambaye ni Papa.
“Mataifa mengi yameiga mambo mbalimbali
yanayofanywa na Kanisa Katoliki kama vile mavazi ya mapadri yameigwa na
yanavaliwa na majaji, maspika na hata wanafunzi wanasherehekea kumaliza
vyuo kwa kuvaa mavazi hayo,” alisema Waziri Membe.
Hata hivyo, Waziri Membe alisema hakuna taifa lolote lililoiga utaratibu wa Wakatoliki kumchagua Papa ili kupata viongozi wao.
“Mataifa mengi yameiga mavazi ya Wakatoliki, lakini hayataki kuiga jinsi wanavyomchagua kiongozi wao mkuu,” alisema.
Alisema uchaguzi wa Papa huwa ni wa haki na kwamba, hakuna mtu anayeweza kutoa rushwa ili achaguliwe.
“Pamoja na uchaguzi kuwa wa haki, lakini mataifa
hayaigi utaratibu huo ili kupata viongozi wao, ndiyo maana kwenye
chaguzi mara kwa mara kunakuwa na vurugu na machafuko,” alisema.
Alisema kila chama lazima kiweke utaratibu wa haki wa kupata viongozi, ili kuepusha taifa kupata rais ambaye ni fisadi.
Wiki iliyopita Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM,
iliwahoji viongozi hao wakituhumiwa kukiuka taratibu za chama hicho kwa
kuanza mapema kampeni kuwania urais. Baada ya kamati hiyo kumaliza,
ilipeleka taarifa kwenye Kamati ya Maadili ya CCM ililipeleka suala hilo
kwa Kamati Kuu, ambayo iliwapa karipio kali na kuwafungia kutogombea
uongozi wowote ndani ya chama kwa mwaka mmoja.
>>>>NIPASHE
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro







Post a Comment
Post a Comment