Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Na Makongoro  Oging’
Kuna taarifa kwamba kumbe askari magereza mstaafu wa Gereza la Dondwe,Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani (jina linahifadhiwa) anadaiwa kuhusika katika zoezi nzima la utoaji wa mafunzo ya kijeshi kwa watu waliovamia Kituo cha Polisi Stakishari jijini Dar es Salaam Julai 12,mwaka huu.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili unaonesha kwamba askari huyo anatajwa kuhusika kutoa mafunzo ya kijeshi na mbinu za medani kwa watu walioshiriki kitendo cha kinyama cha kuvamia kituo, kuiba silaha na kuua raia na askari.

Mwandishi wetu alielezwa na vyanzo makini vya habari kwamba askari huyo alikuwa akitoka kijijini kwao ambacho kipo mbali na makazi ya wanaodaiwa wahalifu wa tukio hilo na kuja kwenye ngome hiyo kwa ajili ya kutoa mafunzo.

“Alikuwa akijidai kuja kwenye ibada lakini alikuwa akipita   nyumba nyingi za ibada, kitu kilitotushangaza wengi kwani hata kama mvua ikinyesha, hakukosa kwenda kwenye ngome ya wahalifu wale.
Imeelezwa kwamba askari huyo alikuwa akiwatembelea watuhumiwa hao huko porini kwenye ngome yao bila vikwazo lakini  raia wa kawaida hawakuruhusiwa kwenda au kupita maeneo hayo jambo liliokuwa likileta maswali mengi juu ya uhusiano wa askari huyo na watuhumiwa hao.
Hivi karibuni wananchi wa Kijiji cha Mandikongo, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani walipokuwa wakiishi watuhumiwa hao wa mauaji wa Polisi wa Kituo cha Stakishari walikaa katika mkutano kujadili  kuhusu suala la ulinzi na usalama, wakakubaliana kwa pamoja kushirikiana na polisi na vyombo vyote vya usalama kuwasaka waliohusika na tukio hilo waliokuwa wakiishi katika pori la kijiji hicho.

Hata hivyo,  wananchi hao walisema askari huyo mstaafu wa magereza lazima asakwe na kukamatwa ili ahojiwe na vyombo vya serikali kuhusu urafiki wake na watuhumiwa hao ambao kwa sasa wamekimbia na familia zao na hawajulikani walipo.

“Unajua huyu askari tuna wasiwasi naye maana angekuwa mtu mzuri angeweza kutoa taarifa kwa vyombo vya dola kuhusu kikundi hicho hatari,” alisema mwanakijiji mmoja wa kijij hicho ambaye hakupenda kuandikwa jina gazetini.
Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mandikongo, Issa Said Mchalaganga alisema kwamba kamati ya ulinzi na usalam  kijijini hapo wamedhamiria
 watuhumiwa wote wanapatikana pamoja na silaha nzito za kivita walizokimbia nazo.
Watuhumiwa saba wanaosadikiwa kuhusika katika uhalifu mbalimbali likiwemo tukio la Stakishari hawajapatikana na vyombo vya dola vinaendelea kuwasaka.

Polisi hivi karibuni walisambaratisha kambi ya kikundi hicho na kufanikiwa kumkamata mtu mmoja, bunduki 15 na fedha shilingi milioni 170 zilizochimbiwa chini katika kambi ya watuhumiwa hao.
Polisi wanne na raia watatu waliuawa katika uvamizi wa Kituo Kikuu cha Polisi Stakishari cha Wilaya ya Kipolisi Ukonga, Julai 12, mwaka huu na watuhumiwa hao wanadaiwa kuhusika na uvamizi huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, SACP Lucas Mkondya alipohojiwa alisema anaendelea kuwasaka watuhumiwa.

“Nawaomba wananchi kutoa taarifa kituo chochote cha polisi, vyombo vya usalama au kwa wenyeviti wa serikali ya mitaa wakiwaona watu wanaowatilia shaka,” alisema.

Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala,

Hifadhi blog hii kwenye simu yako ili upate habari zote kwa urahisi zaidi

Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
http://www.facebook.com/kibonajoro

Post a Comment

 
Top