HATUA ya mawakili wa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kutengeneza ubishi wa kisheria katika agizo la Polisi la kuwasilisha nyaraka za mali za Askofu huyo, imeelezwa kuwa ni ukaidi ambao hautamsaidia kisheria.
Badala yake, kwa hatua hiyo ya mawakili hao, Jeshi la Polisi limewekewa mazingira mazuri ya kuchukua hatua ya pili ya matumizi ya nguvu katika kutekeleza agizo lao, baada ya hatua ya hiyari kushindikana.
Wakizungumza na gazeti hili jana, wanasheria mbalimbali walishangazwa na ubishi wa juzi, uliotokana na barua ya mawakili wa Askofu Gwajima kwenda kwa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
Katika barua hiyo, mawakili hao walitaka Polisi itoe agizo la maandishi la kuwasilisha nyaraka hizo, litakaloeleza vifungu vya sheria vinavyomtaka mteja wao kuwasilisha nyaraka hizo.
Ukaidi wa Gwajima
Barua hiyo iliyosainiwa na Wakili Peter Kibatala, iliwasilishwa juzi mchana katika jeshi hilo ikiwa ni siku moja baada ya Askofu Gwajima kutakiwa kuwasilisha nyaraka 10 zinazohusu umiliki wa mali zake, Aprili 16 mwaka huu watakapoendelea na mahojiano.
Mawakili hao kwa niaba ya mteja wao wameliomba Jeshi la Polisi kumwandikia barua rasmi Gwajima, wakiainisha nyaraka wanazozihitaji, pamoja na vifungu vya sheria vinavyotumiwa na jeshi hilo kutaka nyaraka hizo.
Mawakili hao wanasema watashukuru kupata hati hiyo ambayo wamedai hawaijui jina, lakini wanaamini Jeshi la Polisi litafahamu jina la kisheria la nyaraka husika inayotumika kumtaka Gwajima, awasilishe nyaraka wanazozihitaji.
Aidha wanasema askofu Gwajima atakapopata nyaraka anayoihitaji, atatimiza mwito na kuchukua hatua stahiki za kisheria.
Nyaraka 10
Nyaraka hizo ni Hati ya Usajili wa Kanisa, Namba ya Usajili, majina ya Baraza la Wadhamini (Baraza la Kiroho), idadi ya makanisa (matawi) anayohudumia, nyaraka za helikopta ya Kanisa na muundo wa uongozi wa Kanisa.
Nyingine ni Waraka wa Maaskofu uliosomwa makanisa yote, nyaraka za nyumba na mali za Kanisa na nyaraka zinazoonesha taarifa za hesabu kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Hiari. Pia waliagizwa kufuatana na mtu anayepiga picha za video kanisani hapo.
Ushauri
Wakifafanua kuhusu ubishi huo wa kutaka sheria inayotumiwa na Polisi kuagiza nyaraka hizo, wanasheria waliozungumza na gazeti hili walisema hakuna sheria yoyote inayomzuia Polisi kudai umiliki halali wa mali au nyaraka endapo watazihitaji.
Mwanasheria Dk Damas Ndumbaro, alisema kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Jinai na ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, askari Polisi amepewa fursa ya kufanya ukaguzi wa mali na nyaraka zozote bila ya kuzuiwa na mtu.
‘’Polisi anaweza kufanya ukaguzi nyumbani kwako bila kuwa na hati ya ukaguzi na anaweza kuwa nayo. Lengo lao ni kukamilisha masuala yao ya kipolisi tu,’’ alisema mwanasheria huyo.
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment