April 29, 2025 07:34:39 PM Menu
 

Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This
Askofu Method Kilaini.

Salaam baba Askofu Method Kilaini.
Ni matumaini yangu kwamba unaendelea vyema na majukumu yako ya kuchunga kondoo wa Bwana. Najua itakuwa vigumu kwa mimi kuonana na wewe kutokana na umbali uliopo kati ya Dar es Salaam na Bukoba lakini hilo halinizuii kukufikishia ujumbe wangu.

Baba askofu, mimi sikuzaliwa Machi 30, 1948 kwenye kijiji kilichozungukwa na migomba cha Katoma, Bukoba kama wewe. Sikusomea hukohuko Bukoba na baadaye kusomea falsafa kabla ya kwenda kusomea dini (Teolojia) katika Chuo cha Urban University of Propaganda Fide, Rome jijini Italia na kuhitimu mwaka 1972.
Sikupewa upadrisho mwaka 1972 na Kardinali Angelo Rossi jijini Rome na kurudi Bukoba kuendelea na kazi ya kumtumikia Mungu kama wewe. Mimi sikuwekwa wakfu mwaka 2000 na kuteuliwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Baadaye sikuhamishiwa Bukoba kuendelea na wadhifa wa askofu msaidizi wa jimbo hilo kama wewe.
Sijui chochote kuhusu dini wala falsafa, mimi ni mkosefu ambaye maisha yangu yametawaliwa na dhambi kwa kipindi kirefu! Mungu ananiadhibu kwa kunipa maisha magumu kutokana na utitiri wa dhambi nilizonazo.
Hata hivyo, ningekuwa mimi katika nafasi yako, baba askofu, kwa hili sakata la kudaiwa kushiriki kwenye ‘karamu ya wenye dhambi’ na kumegewa zaidi ya milioni 80 kwenye mgawo wa mabilioni ya Escrow, hakika ningeachia wadhifa wangu.
Baba askofu, mbona utaratibu unajulikana kwamba sadaka za kanisa zinapelekwa kanisani? Kwa nini hizo milioni 80, kama kweli waliokupa walikuwa na lengo la kutoa sadaka au michango ya kulisaidia kanisa, hawakuielekeza moja kwa moja kanisani na badala yake ukaingiziwa kwenye akaunti yako binafsi?
Na kama kweli kanisa lilikuwa linajua, kwa nini mpaka leo halijatoa tamko lolote la kukusafisha? Jamii yetu ya Kitanzania, imejengwa kuwa na imani kubwa kwa viongozi wa dini kama wewe. Ni kawaida kwa wanasiasa kuiingiza nchi katika matatizo makubwa ya ufisadi kama ule wa Richmond, Epa, Escrow na mingine mingi! Tumeshazoea.

Hata kama watu wanashtuka, lakini moyoni wanajua kuwa ni kawaida ya wanasiasa lakini mbona sasa mambo yanabadilika? Kwa nini na nyie viongozi wa dini ambao kwa kipindi kirefu tumekuwa tukiwategemea kukemea maovu leo mnadaiwa kushiriki kwenye karamu za wenye dhambi?
Baba askofu, kama ulikuwa unajua au ulikuwa hujui kama fedha ulizopewa ni haramu, bado suala la msingi linabaki palepale, na wewe umeshiriki kumtafuna ‘ndafu’ wa Escrow hivyo inabidi uwajibike! Ndiyo, utaendeleaje kuwaungamisha wenye dhambi wakati na wewe tayari unatajwa kuwa miongoni mwa wakosefu?
Najua kwamba unaijua vyema lugha ya Kilatini, kuna msemo uliokaa kisheria zaidi usemao: Ignorantia juris non excusat (kutokujua sheria hakukupi msamaha). Yawezekana wakati ukimtafuna ndafu huyo, hukuwa ukijua kwamba ni wa wizi na kwamba ulikuwa ukivunja sheria lakini hiyo haikuondolei hatia!
Kamati ya kudumu ya hesabu za serikali ya bunge, ilipendekeza kuwa wote walioshiriki kutafuna mabilioni ya Escrow kama mchwa, washughulikiwe ipasavyo lakini katika ripoti yake, kamati hiyo haikuwagusa ninyi viongozi wa dini.
Basi kwa nia njema kabisa, nakushauri baba askofu, kubali kuwajibika, achia ngazi wakae wengine ili uendelee kulinda heshima yako ambayo umekuwa nayo kwa kipindi kirefu pamoja na heshima ya kanisa.
Hutakuwa kiongozi wa kwanza wa dini kuachia ngazi, wapo wengi tu, tena wengine wenye nyadhifa za juu kuliko wewe duniani, ambao japokuwa wengine hawakuwa na hatia lakini jamii ilipoanza kuwasakama kwa kashfa moja au nyingine, waliamua kumuandikia barua Papa na kuachia madaraka.
Wasalaam.
Ungana nasi katika  Facebook na Umechekeshwa

Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala,

Hifadhi blog hii kwenye simu yako ili upate habari zote kwa urahisi zaidi

Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
http://www.facebook.com/kibonajoro
13 Dec 2014

Post a Comment

 
Top