Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This



KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, mama wa watoto watatu, mkazi wa wilayani hapa, mwanzoni mwa wiki hii aliwatekeleza porini watoto hao, akiwemo mwenye umri wa miezi mitatu.

Mama wa watoto hao amefahamika kuwa ni Wakuru Omar, mkazi wa kijiji cha Salama wilayani hapa. Tukio hilo limethibitishwa polisi wilayani Bunda, wanaoendelea kumtafuta mama huyo kuhusu ukatili dhidi ya watoto wake.

Limethibitishwa pia na msimamizi wa haki za binadamu na ukatili wa watoto katika Kata ya Salama, Lydia Kabaka aliyesema watoto hao walitelekezwa usiku wa Desemba 9, mwaka huu.

Alisema mwanamke huyo alitupa watoto hao, ambao mmoja anao umri wa miaka mitatu, mwingine miaka miwili na mdogo mwenye umri wa miezi mitatu, ambao wote ni wa kiume.

Alidai chanzo cha mama huyo kufanya ukatili dhidi ya watoto wake ni ugomvi wa kifamilia na ulevi wake wa kupindukia.

Alifafanua kuwa mwanamke huyo aliolewa na mume wake ambaye alikuwa na wanawake wengine wawili na alifanikiwa kuzaa watoto wanne na mmoja wao akafariki, lakini baadaye akawa mlevi wa pombe wa kupindukia na kuleta ugomvi ndani ya familia hiyo.

Alisema kutokana na tabia hiyo ya ulevi wa kila siku, mumewe aliamua kumtoa nyumbani hapo na kumpangishia nyumba sehemu nyingine kijijini hapo, ikiwa ni pamoja na kumpatia mahitaji yote muhimu ya kijamii na kifamilia.

Alidai kuwa siku ya tukio wakati wa usiku mwanamke huyo akiwa amelewa aliwachukua watoto wake wote watatu na kuwatelekeza porini na kutokomea kusikojulikana.

Alisema watoto hao waliokolewa na wapita njia baada ya kusikia wanalia, kutokana na kutaabika kwa kupigwa na baridi na njaa kali.

“Huo ni ukatili wa hali ya juu, aliwachukua watoto wake na kwenda kuwatupa porini kwenye katani, lakini waliokolewa na wapitanjia waliofika katika eneo hilo baada ya kusikia kelele za kulia kwa watoto hao,” alisema.

Aidha, alisema watoto hao walichukuliwa na kupelekwa kwa baba yao na tukio hilo kuripotiwa kituo cha polisi Nyamuswa. Polisi wilayani hapa walisema wanaendelea kumtafuta mwanamke huyo afikishwe mahakamani kwa kosa la kutesa na kutelekeza watoto wake porini.

Matukio ya wazazi kutelekeza watoto wao yamekuwa yakitokea mara kwa mara wilayani hapa na hivi karibuni mwanamke mwingine alitelekeza mtoto wake wa mwaka mmoja na kwenda kufanya kazi ya baa.
HABARI LEO

Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala,

Hifadhi blog hii kwenye simu yako ili upate habari zote kwa urahisi zaidi

Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
http://www.facebook.com/kibonajoro
12 Dec 2014

Post a Comment

 
Top