Katika hali hisiyo ya kawaida, waganga wawili wanaounda kundi maarufu la Rambaramba walinusulika kupoteza maisha Jumamosi ya wiki iliyopita wakati wakitekeleza majukumu yao ya kuuondoa uchawi katika kitongoji cha Makulunge kijiji cha Kiluvya mkoani Pwani!
Tukio hilo ambalo lilishuhudia na mamia ya wakazi wa kijiji hicho, lilitokana na waganga hao kuitwa na wananchi wa kijiji hicho kwa lengo la kutoa uchawi katika shule ya msingi Makulunge A.
Awali, kwa mujibu wa baadhi ya wananchi waliozungumza na times fm walipasha kwamba kumekuwa na matukio ya ajabu ambayo yamekuwa yakiwatokea wanafunzi wanaosoma shuleni hapo ikiwa ni pamoja na kusikia sauti za ajabu ajabu zikilia hawa maeneo la msalani.
“Watoto wamekuwa wakisikia sauti za watoto wakilia mara wanasikia sauti za paka lakini wakienda kuangalia pale sauti inapotoka wala hawaoni hicho kinacholia! Wakati mwingine mtoto anakwenda msalani anaaza kusikia sauti ikiita jina lake wakati yupo mwenyewe msalani,” anasema mkazi mmoja wa kijiji hicho aliyejitambulisha kwa jina moja la Athuman.
Athumani akaongeza, “Hata ufauli ndugu mwandishi ni mdogo sana ukilinganisha na idadi kubwa ya wanafunzi wanaotahiniwa kila mwaka.”
Taarifa zinasema baada ya viongozi na baadhi ya kamati ya shule kukutana waliamua kwa pamoja kuita kundi hilo la waganga kwa ajili ya kuuondoa uchawi huo na mara baada ya kufika siku ya kwanza na kufanya uchunguzi waligundua eneo hilo linauchawi mkubwa na kuomba kurudi tena siku ya Alhamisi huku wakitoa agizo la kununuliwa mbuzi kwa ajili ya kufanikisha kazi hiyo.
Mmoja kati ya mjumbe wa kamati ya shule hiyo Bw. Mohammed Njami, alisema waliamua kwa pamoja kuita waganga hao baada ya kuona matatizo ya kishirikina kwa wanafunzi wao wanaosoma shuleni hapo kuzidi.
“Watoto wetu wanapata shida sana na ndio maana tukaona kuna haja ya kuita waganga kwa ajili ya kutuondolea vitu hivyo….nadhani hata mwandishi mwenyewe umeona vitu jinsi vilivyotolea,” alisema.
Njami alipouliza kama shule hiyo inamatatizo mengine zaidi ya uchawi ambao kwa pamoja walichangishana pesa na kununuliwa mbuzi ili kuuondia, alisema shule hiyo inamatatizo ya madawati na watoto wao wengi wanakaa chini.
“Lakini kuhusu tatizo la madawati kuna mkutano wa wazazi na walimu utafanyika tarehe 18/11/2014 kwa lengo la kutatua kero ya madawati kwa shule yetu,” alibainisha.
Baadhi ya wanafunzi wanaosoma shuleni hapo waliozungumza na gazeti hili hawakuonyesha kukataa wala kukubali uwepo wa matukio ya ajabu kutokana na kila aliyezungumza kuonekama kuwa katikati ya jambo hilo.
Mtangazaji wetu, Edson Mkisi Jr alishuhudia waganga wakizimia wakati kazi hiyo ikiendelea kiasi cha kuanza kutia hofu kwa wananchi na hatimaye kuacha kuimba na kupiga makofi kama walivyotakiwa kufanya na waganga hao.
“Mwenzangu wasije wakafu tukaingia matatizoni hapa….kama wameshindwa bora waseme kuliko kutufia hapa….,” alisikika mwanakijiji mmoja akisema kwa sauti ya chini.
Hata hivyo, baada ya hali kuzidi kuwa tete kwa waganga hao walilazimika kuachana na kazi ya kuondoa ucahwi na kuanza kuwasaidiana ili kuwaopoa waliopoteza ‘neteweki’.
Mkisi Jr alishuhudia ndoo za maji zenye ujazo tofauti zikimwagwa kwa waganga wale huku wakikamulia na dawa mbalimbali lakini bado iliendelea kuwa mbaya kwa waganga walipozimia.
Hata walipozinduka baada ya kazi ya ziada kufanyika, waganga hao waliopoteza fahamu walikwenda kukaa pembeni kwa ajili ya kutafakari kilichotokea.
Times fm ilipotaka kujua nini kiliwatokea kiasi cha kupoteza fahamu na kuanza kuzua hofu kwa wananchi, mmoja ya waganga hao alisema matatizo ni sehemu ya kazi zao na kama pale angepoteza maisha hakuna mtu ambaye angeingia matatizoni.
“Wakati naingia kwenye kazi hii nilikula kuiapo kwa hiyo kama lolote lingetokea wala hakuna mtu ambaye angesumbuliwa na polisi maana ni sehemu ya kazi,” alisema.
Alipotafutwa kwa njia ya simu mwenyekiti wa kijiji hicho aliyetajwa kwa majina la Ade Mbruno kwa lengo la kutolea ufafanuzi uwepo wa uchawi katika moja ya shule zake, mwenyekiti hiyo alisema ni kweli alipata nakala ya barua ya uwepo wa waganga hao kijijini kwake lakini yeye hakuhusika katika kuwaita waganga hao.
“Kwa sasa nipo kanisani lakini naomba kukuhakikishia kwamba sijui na wala sihusiki na uwepo wa hao waganga. Hao wameletwa na kikundi cha watu kati ya 20 au 25 lakini mimi sijui lolote kuhusu uwepo wa hao waganga maana mimi siamini hayo mambo,” alisema mwenyekiti huyo.
Aidha, kwa upande wa Mkuu wa shule ya Msingi Makulunge A aliyetajwa kwa jina moja la Mwele, alisema yeye hajui na wala hajabariki uwepo wa waganga hao shuleni haijarishi mjumbe wa kamati ya shule kuthibitisha kufanyika vikao kadhaa kwa ajili ya ujio wa waganga hao.
“Sijui kabisa kuhusiana na ujio wa waganga hao kwanza hayo ni mambo ya kiimani ambayo mimi wala siyaamini kwa hiyo kama kuna kitu kama hicho Jumatatu nikifika shuleni nitahoji ujio wa hao waganga lakini mimi wala sijui ujio wao,” alijitetea mkuu huyo.
Siku moja baada ya kuzungumza na mwenyekiti pamojna na mkuu wa shule hiyo, kituo hiki kilipokea taarifa toka kwa baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wakisema kwamba baadhi ya wazee wamechukizwa na waganga hao kuondoa uchawi katika kijiji hicho na wametoa saa 24 waondoke.
“Kuna wazee hawawataki waganga wetu wamewapa saa 24 waondoke hivi sasa tunaandamana kwenda kwa mwenyekiti wa kijiji kupinga amri hiyo,” alisema mwanakijiji mmoja kwa njia ya simu.
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment