Stori: Na Dustan Shekidele, Morogoro
MTOTO mmoja wa miaka 9 (jina linahifadhiwa) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Manda iliyopo Kijiji cha Mtimbira, wilayani Ulanga, Morogoro wiki iliyopita usiku wa manane anadaiwa kukutwa darasani akiwa na hirizi kubwa kiunoni.
Mwananchi akionesha Hirizi iliyofungwa kiunoni mwa mtoto wa miaka tisa (jina linahifadhiwa).
Tukio hilo lilitokea katika moja ya majengo ya Shule ya Msingi Mazoezi Kigurunyembe ya mjini humo.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo lililoshuhudiwa pia na mwandishi wetu, lilijiri Alhamisi iliyopita ambapo mara baada ya kuonekana darasani humo, baadhi ya wananchi walianza kumpa kichapo wakidai kuwa yeye ni mwanga.
Dogo huyo alinusurika kifo kutoka kwa wananchi hao wa Kigurunyembe waliokuwa na hasira kali baada ya mmoja wa walimu kuwatuliza na kufanikiwa kumuokoa mwanafunzi huyo na kwenda kumficha kwenye ofisi ya walimu ya shule hiyo.
Hirizi nyekundu ikiwa kiunoni mwa mtoto huyo.
Akihojiwa na Uwazi mwalimu huyo aliyejitambulishwa kwa jina la Zuhura Khatibu alikuwa na haya ya kusema:
“ Wiki hii mimi ni mwalimu wa zamu nilipofika shuleni nikawashuhudiwa wananchi wakimshushia kichapo mtoto huyo, kama mzazi niliumia sana nikawauliza kwa nini wanampiga wakadai eti ni mwanga ameanguka hapa shule usiku, sisi tulipigwa butwaa. Nilimuoka na kumficha ofisini,” alisema Zuhura.
Mtoto huyo akiwa na mwalimu wa zamu, Bi. Zuhura Khatibu.
Akizungumza na mwandishi wetu, mwanafunzi huyo alidai kuwa alitokea Mtimbira kwa ndege ya kichawi, anatumiwa na wanga na kwamba alipofika pale shuleni wenzake walimdondosha akaamua kuingia darasani.
Alipoulizwa alikuwa anaelekea wapi usiku huo, alidai walikuwa wakienda Kihonda kwa baba yake anayefanya biashara ya mbogamboga. Alipopekuliwa alikutwa na hirizi kubwa yenye rangi nyekundu kwenye mkanda wa suruali yake, alipoulizwa ilikuwa ya nini alisema alifungwa ili kumlinda.
Mwalimu Zuhura Khatibu akimpeleka mtoto huyo kituoni.
Baada ya mahojiano hayo,walimu hao walimkabidhi mwandishi wetu mwanafunzi huyo ambapo waliongozana na Mwalimu Zuhura hadi Kituo cha Polisi Morogoro kwenye dawati la jinsia na watoto.
Mkaguzi Msaidizi wa Polisi wa Dawati la Jinsia na Watoto, Sophia Ngosso alimpokea mtoto huyo na kufungua taarifa kwenye kitabu cha kumbukumbu cha polisi jalada namba MOR/RB/12659/014.
Baadaye iligundulika kuwa mtoto huyo alikuwa anatafutwa na baba yake aitwaye Clarence Kandira ambaye alifika pale polisi baada ya kupigiwa simu ambapo alimtambua mwanaye na kuangua kilio na kusema:
Baba wa mtoto huyo kushoto, Clarence Kandira akimshukuru msamaria mwema (Zuhura Khatibu).
“Huyu mtoto anasoma darasa la pili Mtimbira na ana matatizo ya ugonjwa, (hakuutaja), tukiwa nyumbani Kihonga alipotea katika mazingira ya kutatanisha na hii ni mara ya pili, mara ya kwanza alipotea hivihivi na kuokotwa kwenye Mto Kilombero akiwa ndani ya mtumbwi.”
Alipoulizwa kwa nini amemfunga hirizi, Kandira alidai kuwa haikuwa hirizi bali ni alama yake inayomsaidia kuonekana kirahisi anapopotea. Afande Sophia alimsainisha Kandira na kumkabidhi mtoto wake akaondoka naye.
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment