WATU 3 wamekufa kwa nyakati tofauti kufuatia kuzuka kwa mapigano ya kugombea ardhi kati ya Wafugaji na Wakulima katika Kijiji cha Kinyinya, Kata ya Nyamtukuza Wilayani Kakonko Mkoani Kigoma.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kinyinya, Justine Kilegea, alisema kuwa tukio hilo limetokea jana usiku baada ya Wafugaji wanaoishi mashambani kuvamia nyumba za Wakulima na kuua watu wawili kisha kuchoma moto miili yao.
Waliokufa katika tukio la juzi, wametajwa kuwa ni Kachila Kahegelu (48) na Lameck Kachila (26), ambao ni ndugu.
Alisema mauaji hayo yanahusisha jamii ya wakulima wenyeji wa kabila la Waha na jamii ya Wafugaji wa kabila la Wasukuma, na yalikuwa ni ya kulipiza kisasi baada ya mfugaji kuuawa na ng’ombe wake kukatwa katwa kwa mapanga Octoba 15 mwaka huu.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Venance Mwamoto, alifika eneo la tukio na kushuhudia miili ya watu waliokufa ambapo alikemea vikali tukio hilo na kusema kuwa ni la uvunjifu wa amani hivyo kuitaka Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Kijiji kukaa na kuzungumzia suala hilo.
“Msigombane kwa ajili ya ardhi, alisema Mwamoto, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kibondo. “Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inasema mwananchi wa Tanzania anaruhusiwa kwenda sehemu yoyote ile ili mradi asivunje sheria.”
Aidha aliwataka wananchi wa Kijiji hicho kuacha mara moja mauaji ya kulipizana visasi na kuongeza kuwa wote waliofanya mauaji hayo watahakikisha wanakamatwa ili sheria ifuate mkondo wake.
Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Kinyinya akiwemo Silas Kabebela na Daniel Paul, walisema kuwa wafugaji wamekuwa ni kero kwa wananchi wakulima wa kijiji hicho kwa kuharibu mashamba yao huku wakiutupia lawama uongozi wa kijiji kuwa unasababisha mgogoro kuwa mkubwa kwa kugawa ardhi bila utaratibu.
Alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo, Mwenyekiti huyo (Kilegea), alisema kuwa yeye wakati anaingia madarakani alikuta wafugaji hao tayari wanaishi mashambani na kwamba hajui utaratibu uliotumika kuwakaribisha kijijini hapo.
Credit kigomapressclub
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro








Post a Comment
Post a Comment