Mbunge wa Mbinga Kusini, Kapteni John Komba, kwa mara nyingine amemshambulia aliyekuwa Mweyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, kwa ‘kuwaingilia’ na amemuomba Rais Jakaya Kikwete, amuite na kumkanya.
Katika mchango wake bungeni jana, Komba alianza kwa kusema, “Ninalo moja kubwa la kuchangia hapa, juzi nilizungumza habari hapa, jamani eh..., mtu akishazikwa, akifufuka ni tatizo kubwa katika kijiji kile, kazi haziendi…sasa jana (juzi) mmeona.?”
“Mimi nasema ukweli kabisa, huyu mzee ana nini, ana kitu gani na sisi, mbona anatuingilia sana,” alisema.
Komba alisema anamwomba Rais amwite Jaji Warioba na kumweleza hakumtuma kufanya hivyo isipokuwa kukusanya maoni basi, na inatosha hapo alipofikia.
Alisema, Jaji Warioba alipoteuliwa na Rais kuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo, kitu cha kwanza alinukuliwa akisema, “mmenichagua mimi na wenzangu sasa naomba mtuache msituingilie, na kweli hakuingiliwa na alifanya kazi na kumaliza vizuri bila kuingiliwa.”
“Lakini anatuingilia sisi, mkuki kwa nguruwe? Yeye amekuwa refarii?
Anatufuatilia kila tunachofanya, sasa na yeye anasema atapambana na sisi, ataingia mitaani, anapambana na sisi, yeye upande mwingine na sisi upande mwingine, haya, njoo Warioba kwetu, tutaonana,” alisema.
Alisema Jaji Warioba anafanya kinyume na alivyoagizwa, kwani wakati wa kuunda tume yake, Rais alimwambia akusanye maoni basi, na amekusanya mengi.
Alisema Jaji Nyalali alipokuwa anakusanya maoni kuhusu mfumo wa demokrasia ya vyama vingi maoni yalionyesha asilimia 80 ya watu walipenda mfumo wa chama kimoja uendelee na asilimia 20 walipenda mfumo wa vyama vingi, jambo ambalo lilikuja kuheshimwa.
Hata hivyo, alisema anashangaa kuona kila wanachokifanya wajumbe wa BMK, Jaji Warioba kazi yake ni kuzungumzia tunu tu.
“Baba baba huyu kila kitu tunachokifanya yeye tunu tunu tunu tunu tunu tuuu basi,” alisema.
Kuhusu uhalali wa BMK, Komba alisema anashangaa kumwona Warioba ambaye ni Jaji anashindwa kuheshimu uamuzi wa majaji wenzake.
“Majaji wenzake wamesema bunge hili ni halali, sasa Warioba ni jaji gani ambaye hataki kuheshimu hata wenzake, jamani?
Shutuma za Komba dhidi ya Jaji Warioba zinafuatia ushiriki wake katika adhimisho la miaka 19 tangu kuanzishwa kwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) jijini Da es Saam juzi.
Adhimisho hilo pia lilitumika kumkumbuka muasisi wa LHRC, marehemu Dk. Sengondo Mvungi ambaye aliwahi kuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Akizungumzia adhimisho la juzi, Komba alisema wakati Jaji Warioba anazungumza kulikuwa na wazungu wengi, na akaonyesha wasiwasi wake kuwa huenda (Jaji Warioba) amepewa kitu na wazungu hao au ameahidiwa kitu hivyo akataka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufuatilia.
Alisema jambo la ajabu ni kwamba, “baba huyu kila siku (anatuingilia) anatufuatilia kila tunachofanya.”
Alimtuhumu Jaji Warioba ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu kuwa hana maadili lakini Makamu Mwenyekiti wa BMK, Samia Hassan Suluhu, alimtaka Komba kufuta maneno aliyomtuhumu (Warioba) kuwa hana maadili, naye akasema, “hana maadili ya kujali wenzake kama wanafanya mambo mazuri, isipokuwa anayo maadili ya mambo mengine.”
Kwa upande wake Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo, alizungumza kwa kifupi kuwa anamshauri Jaji Warioba apumzike baada ya kufanya kazi nzuri ya kukusanya maoni ambayo ndiyo yametumika kama msingi wa Katiba.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Andrew Chenge alisema kuwa anawaheshimu baadhi ya viongozi wanaoendelea kutoa maoni yao ya kuiponda Rasimu ya Katiba inayopendekezwa hivyo hapendi kabisa kulumbana nao.
Aliwataka Watanzania kuzisoma Rasimu zote mbili (ile ya Jaji Warioba na inayopendekezwa na BMK) ili wapime kuona ni ipi iliyo bora.
Alisisitiza kuwa msingi wa Rasimu ya Katiba inayopendekezwa na BMK ni Rasimu ya Jaji Warioba hivyo madai ya kwamba maoni ya wananchi hayakuzingatiwa hayana ukweli wowote.
Source:Nipashe
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment