Vijana 65 wa
Tanzania wamehukumiwa adhabu ya kifo nchini China baada ya kupatikana
na hatia ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya. Vijana
hao ni kati ya zaidi ya 403 wa Tanzania wanaoshikiliwa katika nchi
mbalimbali duniani kwa tuhuma ya kujihusisha na biashara hizo.
Hayo
yalisemwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu
na Bunge), William Lukuvi(pichani), mjini Dodoma wakati akizungumzia
Maadhimisho ya Siku Dawa za Kulevya Duniani yanayofanyika Juni 26 kila
mwaka.
Lukuvi
alisema kuwa kwa mwaka huu maadhimisho hayo ya kesho, kitaifa
yatafanyika katika viwanja vya shule ya msingi Nzovwe jijini Mbeya na
Makamu wa Rais, Dk. Gharib Bilal, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
“Tangu mwaka
2008 kumekuwa na wimbi kubwa la vijana wenye asili ya Kitanzania
kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi,
mpaka hivi sasa idadi yao ni kubwa kiasi cha kufikia zaidi ya 400, na
wanashikiliwa katika nchi mbalimbali ambazo pia adhabu zao
zinatofautiana kulingana na sheria za nchi hizo,” alisema Lukuvi.
NCHI WANAKOSHIKILIWA
Alizitaja
baadhi ya nchi ambako vijana hao wanashikiliwa kuwa ni Brazil (108),
Hong Kong (118), Kenya (34), Pakistan (16) na China 65. Nyingine ni Japan (7), Malawi (5), Uganda (3), Uswisi (2), Marekani (2), Uturuki (1), Botswana (5) na Msumbiji (1). “Orodha ya nchi waliko vijana hao ni defu zaidi,” alisema.
Akizungumzia
maadhimisho hayo kwa nchini, Lukuvi alisema kauli mbiu yake kwa mwaka
huu ni ‘Uteja wa dawa za kulevya unazuilika na kutibika, chukua hatua'.
AlisemaTanzania
imeendelea kuwa miongoni mwa nchi zenye tatizo kubwa la dawa za kulevya
kulingana na takwimu za ukamataji wa dawa hizo.
Kwa mujibu
wa Lukuvi, kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu kiasi cha kilo 220 za
dawa hizo aina ya Heroine na watuhumwa 18 walikamatwa huku pia kilo
15.4 za Cocaine zilikamatwa na watuhumiwa saba.
Lukuvi
alisema kwa sasa dawa za kulevya ni tishio kubwa kwa maendeleo ya taifa
kwa sababu imethibitika kuwa matumizi yake hupunguza tija na ufanisi wa
nguvu kazi ya taifa.
SHERIA MPYA YAJA
Alisema
katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali imekamilisha muswada wa
sheria ya dawa za kulevya ambao kama utapitishwa bungeni na kuwa sheri
kama ulivyo, unaweza kusaidia kwa Kiwango kikubwa kupunguza tatizo hilo.
Lukuvi
alisema tofauti na jinsi ilivyo sheria ya sasa, sheria mpya itaondoa
adhabu ya faini na watuhumiwa kunyimwa dhamana wanapokamatwa, hali
ambayo itasaidia kukabiliana na wasafirishaji na wauzaji wa dawa hizo.
Kwa mujibu
wa Lukuvi, sheria hiyo itakwenda sambamba na uundaji wa chombo imara cha
kushughulikia dawa za kulevya ambacho kitakuwa na uwezo wa kupeleleza,
kukamata na kushitaki watuhumiwa wa dawa za kulevya kama ilivyo kwa
Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Alisema kuwa
muswada huo tayari umekamilika na kwamba wakati wowote unaweza
kuwasilishwa bungeni ili upitishwe hatimaye kuwa sheria.
Alisema
maadhimisho hayo pia yatafanyika katika ngazi ya mkoa nchini na kuwaomba
wananchi kujitokeza kushiriki ili waweze kupata elimu ya kutosha juu ya
madhara na vita dhidi ya dawa hizo.
KANDORO ANENA
Naye Mkuu wa
Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, amewataka wananchi mkoani mwake
walioathirika na dawa za kulevya kujitokeza kwa wingi kupima afya zao,
kupata tiba na ushauri katika maadhimisho hayo.
Kandoro
alifafanua kuwa maadhimisho hayo yanafanyika mkoani humo kutokana na
takwimu kuonyesha una kiwango kikubwa cha tatizo la dawa za kulevya
kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu na kutoa mfano wa bangi ambayo
inalimwa kwa wingi.
“Kama
mnavyojua, mkoa wetu upo mpakani hivyo tuna changamoto kubwa sana ya
uingizaji wa dawa hizi, mara nyingi watu hukamatwa katika mipaka ya
Tunduma na Kasumulo, hivyo ni budi elimu hii kutolewa kwa wananchi ili
tushirikiane wote katika kutokomeza vita hii tuliyonayo,” alisema
Kandoro.
Alisema kuwa
pombe aina ya viroba vya bei nafuu vitokavyo Malawi ni changamoto pia
kwani vijana wengi wanavitumia, hivyo kuathirika kwa kiasi kikubwa.
NA EMMANUEL LENGWA
CHANZO: NIPASHE
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro








Post a Comment
Post a Comment