PIPI 60 za madawa ya kulevya aina ya heroine
yanayokadiriwa kuwa na thamani ya shilingi milioni 60 yanadaiwa
kukamatwa ndani ya Gereza la Keko jijni Dar es Salaam baada ya mtu mmoja
kuingia nayo akiwa ameyameza.
Kwa mujibu wa chanzo, mtu mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Mashujaa
Udugu Matata, aliingia gerezani humo Machi 21, mwaka huu akitokea
kusomewa shitaka la kukutwa na madawa ya kulevya katika Mahakama ya
Kisutu jijini Dar es Salaam.
Inadaiwa Matata alikamatwa na polisi katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere, Machi 17, mwaka huu, saa 8.25 usiku
akitokea nchini Brazil.
Baada ya kukamatwa alitoa pipi 102 za madawa hayo. Alipofikishwa
gerezani hapo, inasemekana mtuhumiwa huyo hakuwa na hali nzuri kiafya,
jambo lililofanya awekwe chumba cha mahabusu wagonjwa ili aweze
kufuatiliwa kwa karibu na madaktari.
“Kesho yake asubuhi kuna mfungwa alikwenda kufanya usafi katika
chumba hicho, wakati anachukua takataka, akaitwa na Matata na kumuomba
achukue mzigo uliofungwa kwenye karatasi ambao ulikuwa unanuka kinyesi,
akamweleza ampelekee mahabusu mwenzake anayeitwa Abbas Gede,” kilisema
chanzo chetu.
Inasemekana Gede ni rafiki wa Matata ambaye naye ana kesi ya ‘unga’ na kwamba awali waliwahi kuishi pamoja Brazil.
Kutokana na sheria kutoruhusu mfungwa kuonana na mahabusu,
alilazimika kumpatia mahabusu mwingine ili aufikishe mzigo huo, lakini
badala ya kuufikisha, mahabusu huyo aliambiwa na rafiki zake kuwa unga
huo ni wa mamilioni ya shilingi, hivyo asubiri awape ndugu zake wakija
kumpelekea chakula.
Hata hivyo, akiwa katika harakati za kutaka kuwapa ndugu zake, askari
wa magereza walimkamata na alipoulizwa alikoyatoa, alimtaja Matata na
hivyo kufanikisha kukamatwa kwa wote waliohusika na mzigo huo.
Mkuu wa gereza hilo, Sena Shida amethibitisha kutokea kwa tukio hilo
na kusema kuwa watu wote waliohusika wataadhibiwa. “Kwa upande wake,
Matata ataadhibiwa mara atakapopata nafuu kulingana na sheria ya mwaka
1967, huo unga tumeuchoma moto,” alisema Shida.
Naye Kamanda wa Kikosi cha Kupambana na Kudhibiti Madawa ya Kulevya
Tanzania, SACP Godfrey Nzowa alipoulizwa alikiri kukamatwa kwa Matata na
kwamba alitoa pipi 102.
Awali walijua kuwa zimeisha hata hivyo, Nzowa alisema alimwagiza mkuu
huyo kuyapeleka madawa hayo ofisini kwake, akashangaa kusikia
yalichomwa. Aidha, alisema aliwasiliana na mkuu huyo wa gareza ambaye
alikiri kutokea kwa tukio hilo ingawa hakuweza kutoa ripoti kituo cha
polisi kama ilivyo taratibu.
Taarifa zilizopatikana ndani ya jeshi la polisi zinadai kuwa, Matata
aliwahi kukamatwa mwala 2007 kwa tuhuma ya kusafirisha madawa ya kulevya
na kufikishwa mahakamani na alikuwa chini ya uangalizi wa jeshi hilo na
wakati huo alikuwa hajabadili jina, aliitwa Abdallah Mauri Kaikai.
Kamishina Mkuu wa Jeshi la Magereza Tanzania, John Minja aliwahi
kuufumua uongozi wa Gereza la Keko kutokana na tuhuma za kuwepo biashara
ya madawa ya kulevya ndani ya gereza hilo.
>>>>>GPL
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro










Post a Comment
Post a Comment