Viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam (JUMIKI)
wamefutiwa mashitaka na mahakama ya wilaya ya Mwanakwerekwe dhidi ya
kesi ya kufanya mkusanyiko bila ya kibali iliofunguliwa Mei mwaka jana
visiwani Zanzibar.
Uamuzi huo umetolewa na Hakim Ame Msaraka Pinja baada ya kukamilika
kusikilizwa kesi hiyo na washitakiwa kuonekana hawana hatia katika
mashitaka yaliokuwa yamefunguliwa na Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar,
mwezi Mei mwaka jana.
Hakimu Pinja amesema kwa kuzingatia mashahidi wanne upande wa mashitaka
pamoja na washitakiwa wenyewe waliithibitishia mahakama kwamba katika
mkusanyiko wao hawakuwa wakizungumzia mambo ya dini isipokuwa Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar.
Amesema kwa msingi huo washitakiwa hawakuhitaji kuwa na kibali chochote
cha kisheria kabla ya kuandaa mkusanyiko huo kwa vile walikuwa
wakizungumzia mambo ya Muungano na kwa msingi huo hakuna shitaka
linalowatia hatiani na mahakama imetupilia mbali dai hilo.
Amesema baada ya mahakama kupitia jalada la kesi hiyo, imeonekana
washitakiwa hawana hatia, “ninawaachia huru kwa sababu kosa
waliloshitakiwa halikuhitaji kibali cha Mufti kabla ya kuandaa
mkusanyiko huo,” alisema Hakimu Pinja.
Hata hivyo Hakimu huyo alisema upande wa mashitaka wa Serikali kama
haujaridhika na uamuzi wa mahakama hiyo unaweza kukata rufaa mahakama ya
mkoa ndani ya siku 30 tangu kutolewa kwa uamuzi huo.
Washitakiwa katika kesi hiyo ni Farid Hadiy Ahmed Mussa Juma Issa, Haji
Sadif Haji, Suleima Juma Suleiman, Fikirini Mjawaliwa Fikirini na
Abdallah Said Ali.
Washitakiwa walifunguliwa mashitaka kwa kufanya mihadhara ya Kiislam
bila kibali cha Mufti kinyume cha kifungu cha 6(1)(2) cha kanuni za
kuidhinisha na kuratibu mihadhara zinazotengenezwa chini ya kifungu
15(1) ya sheria Namba 9 ya mwaka 2001, kifungu cha 10(1)© na kifungu cha
14(2) ya sheria namba 9 ya mwaka 2001.
Ilidawa bila ya halali, Mei 26 mwaka jana majira ya saa 3:30 huko katika
viwanja vya Lumumba wilaya ya Mjini Unguja, washitakaiwa walifanya
mihadhara ya Kiislam bila ya kuomba kibali cha Mufti wa Zanzibar.
>>>>Zanzibar islamic news blog
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment