
Kashfa ya
baadhi ya wabunge kukatisha safari za kikazi nje ya nchi baada ya
kuchukua fedha za safari na posho limewatia aibu na kutikisha bunge jana
asubuhi huku Bunge likisema suala hilo limefikishwa ngazi ya utawala na
kuwataka waliochukua posho hizo kuzirudisha. Sakata
hilo liliibuliwa bungeni na Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu
Nchemba, wakati akiomba mwongozo kwa mwenyekiti wa kikao hicho, Mussa
Zungu Azzan (Ilala – CCM) baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na
majibu.
Katika
mwongozo wake, Mwigulu alitaka kujua hatua ambazo bunge linachukua
dhidi ya wabunge wachache ambao wanachukua fedha bila kwenda safari za
kikazi suala ambalo alisema linawadhalilisha wabunge.
“Hivi karibuni kumekuwa na taarifa kwenye magazeti kwamba baadhi ya
wabunge waliopewa safari za kikazi nje ya nchi wamechukua fedha lakini
wameshindwa kwenda huko na wengine wamekatisha safari hizo.
“Magazeti yameandika kwamba wana mahusiano, mimi sipendi kwenda kwenye
uhusiano na badala yake nataka kwenda kwenye taswira ya Bunge na
Taifa,” alisema.
“Hili ni
suala binafsi, lakini linachafua taswira ya wabunge na kulidhalilisha
bunge. Hatua gani zinachukuliwa dhidi yao,” alisema na kuongeza:
“Jambo hili limechukua taswira kama ni bunge lote na limevunja heshima
ya Bunge na linatuvunjia heshima, hata watu ambao tuna maadili ya
uongozi tunaoliheshimu taifa letu.”
“Lakini mwongozo ninaotaka kuomba ni kwamba kiti chako kinachukua hatua
gani stahiki ya kupambanua kwamba mambo yaliyofanywa na mbunge binafsi
na yashughuhulikiwe kwa mbunge binafsi mwenyewe kuliko kupanga taswira
bunge zima tuonekane ni wa hovyo,” alisema.
Wakati Mwigulu akizungumza wabunge wengi wa CCM walionekana kupiga
makofi hali ambayo iliwamfanya Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema),
David Silinde, kusimama na kusema maelezo ya Mwigulu yanaonyesha kuwa
suala hilo ni la wapinzani peke yake, jambo ambalo siyo kweli.
Alisema wabunge wote wa CCM na Upinzani wanahusika katika kashfa hiyo.
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Mariam Msabaha, aliwaeleza wabunge
wenzake kwamba wakianza kutajana wapenzi humo bungeni hakuna
atakayesalimika kwani kila mmoja anaye wa kwake.
Alisema anashangaa kumsikia Mwigulu akisema amesoma kwenye magazeti
kashfa ya wabunge kuchukua posho na kutokwenda safari wakati hasemi
kuhusu habari za mbunge mmoja wa kike (CCM) ambaye ameandikikwa kwenye
magazeti pia kuwa ameiba kidani.
Alisema wizi huo nao unalichafua bunge pia na Mwigulu alipaswa kulilalamikia hilo kwa kuwa nao linawachafua wabunge.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Anna Abdallah, aliunga mkono kauli ya
Msabaha, akisema masuala hayo ya binafsi hayapaswi kujadiliwa bungeni.
Kwa upande wake Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Kabwe Zitto,
alisema Bunge linataratibu zake za namna gani ya kushughulikia masuala
kama hayo.
Alisema Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) ambayo yeye ni mwenyekiti
wake, imemwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
kufanya uchunguzi kuhusu suala hilo na kuwasilisha ripoti yake kwa
Spika.
Alisema kama Spika ataona kuwa inafaa taarifa hiyo iwekwe hadharani basi bunge litataarifiwa.
Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azan Zungu, alisema kuwa mwongozo huo utatolewa baadaye.
CHANZO: NIPASHE
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro







Post a Comment
Post a Comment