Ali Hassan Ali, Msomali
anayeishi katika kambi kubwa ya Dadaab huko kaskazini mashariki mwa
Kenya, amesema anahuzunishwa na kujiua kulikotokea hivi karibuni kwa
rafiki yake Mwethiopia na mwanakambi mwenziye wa muda mrefu.
Kijana
mdogo wa Kisomali aliyechafuka vumbi usoni akisubiri pamoja na
wakimbizi wengine kwenye kituo cha usajili katika kambi kubwa ya
wakimbizi ya Dadaab Agosti 2011. Hali ngumu ya maisha katika makambi na
msongo sugu umesababisha baadhi ya wakimbizi kujiua. [Tony Karumba/AFP]
Kila siku kwa kipindi cha miaka
mitano iliyopita, Ali, mwenye umri wa miaka 35, alisema yeye na rafiki
yake Abdi Aden Hussein walikuwa wakienda pamoja kila siku kuangalia mbao
za matangazo zinaorodhesha majina ya wakimbizi walioidhinishwa kwa
upataji wa makazi mapya.
Wanaume hao wawili walikuwa na
hakika kwamba siku moja maombi yao ya upataji wa makazi mapya
yatafikiwa, Ali alisema, lakini maombi ya Hussein yalikataliwa kabisa.
"Tulituma maombi pamoja kwa
ajili ya upataji wa makazi mapya. Huku nikisubiri kupata makazi mapya
huko Marekani, Abdi hakufanikiwa," aliiambia Sabahi.
Tarehe 9 Juni, Hussein, mwenye umri wa miaka 34, alijiua katika kambi ya Ifo I ya Daadab, Ali alisema.
Mahema
yamejaa katika viunga vya kambi ya wakimbizi ya Dagahaley katika kambi
kubwa ya wakimbizi ya Dadaab huko Kenya Julai 2011, katikati ya ukame na
njaa inayoua ambayo iliwalazimisha Wasomali wanaokadiriwa 1,300 kila
siku kuomba hifadhi nchini Kenya, kwa mujibu wa shirika la wakimbizi la
Umoja wa Mataifa. [Phil Moore/AFP]
Wale waliongizwa katika orodha
fupi kwa usaili kwa kawaida huwa na furaha sana kwa sababu maombi yao
kwa ajili ya upataji wa makazi mapya kwa hakika yanahakikishwa, Ali
alisema, lakini waombaji wanaokosa hutafuta njia ya mkato kwa
kuharibikiwa na kwamba wanazamisha huzuni zao kwenye madawa ya kulevya
au kujiua wenyewe.
Osman Yusuf Ahmed, mkimbizi wa
Kisomali mwenye umri wa miaka 39 ambaye ameishi katika kambi ya Hagadera
kwa miaka 17, aliiambia Sabahi kwamba kaka yake Musa alijiua mwezi
Disemba baada ya maombi yake kadhaa ya kupewa makazi mapya kutofanikiwa.
"Alikuwa na shauku kubwa na maisha ya
Ulaya kwa sababu ya hadithi za mafanikio ambazo zinavutia katika
makambi," Ahmed aliiambia Sabahi.
"Baada ya maombi ambayo
hayakufanikiwa, alijitenga. Katika matukio ya nyuma aliniambia kwamba
maisha hayana maana, lakini niliendelea kumtia moyo kwamba haukuwa
mwisho wa kila kitu," Ahmed alisema, lakini hakukuwa na mafanikio.
Yusuf Ali Elmi, Msomali mwenye
umri wa miaka 33 ambaye ameishi katika makambi ya wakimbizi nchini Kenya
tangu 1995, alisema mara kwa mara alifikiria kujiua kabla ya hatimaye
kuwa na sifa ya kupata makazi mapya Marekani mwezi Mei.
"Mawazo ya kukata tamaa yana
nguvu unapokuwa pekee yako au unapokosa mwelekeo," Elmi aliiambia
Sabahi. Kuelezana aliyoyapitia na hisia zake na wengine ndiko
kulikomfanya asubiri kwa muda mrefu, alisema.
Licha ya kushindwa kupata makazi
mapya, wakimbizi wengi wanakabiliwa na msongo mkubwa kutokana na hali
duni ya maisha na changamoto za maisha katika kambi zilizojaa, ambazo
zinawasababishia baadhi kujiua, alisema.
Idadi ya waliojiua haijulikani
Jitihada
za kupata takwimu rasmi za idadi ya waliojiua katika kambi za wakimbizi
Kenya hazikufanikiwa. Viongozi kutoka Shirika la Kimataifa la Uhamiaji
walikataa kujibu maombi ya mahojiano.
Ofisa wa Wilaya ya Dadaab
Bernard ole Kipury alikiri kwamba kujiua kumetokea katika kambi, lakini
katika matukio kadhaa, sababu ya kifo bado haijulikani, alisema.
"Jamii ya wakimbizi iko katika
tahadhari, na hata ambapo kujiua kuliko wazi kunafanywa, wanafamilia
wanasisitiza kwamba kichukuliwe kama kifo cha kawaida," aliiambia
Sabahi.
"Waathirika wengi wanazikwa hata
kabla mamlaka hazijafahamishwa. Tunapata taarifa muda mrefu baada ya
mazishi kufanyika, wakati hatuna lolote la kufanya," alisema.
Kuzuia tatizo la kujiua katika
kambi ya Dadaab na kambi nyingine na kusaidia wakimbizi kukabiliana na
hisia zao, mashirika ya wakimbizi yanapaswa kuingiza huduma za ushauri
wa kisaikolojia katika programu zao, alisema Edward M'Mutungi, mhadhiri
wa muda wa saikolojia katika Chuo Kikuu cha Daystar mjini Nairobi.
"Wakati wakimbizi wanapowasili
na wakati wanaishi katika kambi, wanapaswa kuhakikishiwa kwamba kila
kitu kitakuwa sawa na kupewa hisia za matumaini," aliiambia Sabahi.
"Kila mmoja, ikiwa ni pamoja na
wakimbizi, wanataka maisha mazuri. Mkimbizi ambaye wakati wote amekuwa
akifikiria vita nyumbani na siku zijazo utasababisha madhara wa kimwili
na akili. Ushauri unaweza kufanyika katika vikundi au kwa mtu
mmojammoja," alisema.
Kukabiliana na tabia ya mauaji,
wakimbizi wenyewe wameshauriana aina isiyo rasmi ya tiba ya vikundi,
alisema Moulid Ali Hassan, mkimbizi wa Somalia mwenye umri wa miaka 35
katika kambi ya Ifo.
Wakimbizi wameanzisha michezo
mbalimbali ya pamoja kambini, ambayo wameipa jina la utani la "kona za
msongo", alisema. Wakimbizi wasiofadhaika hukutana hapo kutoa matatizo
yao miongoni mwao wenyewe.
Wanaweza kukutana kuanzia
alfajiri hadi jioni wakizungumza kuhusu mada mbalimbali ikiwa ni pamoja
na fursa za kazi kambini, siasa nchini Somalia, matarajio ya kupata
makazi mapya, matatizo katika ndoa zao au ukiwa, alisema.
"Katika kona za msongo, mtu
anaruhusiwa kuzungumza kwa sauti ya juu, kunong'ona, kugumia, kulaani,
kuwia, kutapatapa, kuapa na kulia. Tunawafariji na kuwanasihi kila
mmoja," aliiambia Sabahi.
"Mwishoni, mtu huondoka mahali hapo akijisikia kwamba ameondoa baadhi ya machungu," alisema.
Chanzo: sabahionline.com
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment