Dodoma/Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameagiza vyombo vya
dola kuwashughulikia kwa kuwapiga wale watakaokataa kutii amri wakati
wakifanya vitendo vya uvunjifu wa amani.
Akizungumza katika Kipindi cha Maswali ya Papo kwa Hapo kwa Waziri Mkuu,
bungeni Dodoma jana, Pinda alisema watu wanapokaidi wanajitakia
matatizo na vyombo vya dola.
Alisema hayo alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kilwa
Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu aliyeuliza: “Serikali ipo tayari kiasi
gani kubainisha na kuchukua hatua stahiki, badala ya kusakama makundi
fulani, tujue chanzo halisi cha vurugu hizi na matatizo haya na jinsi
gani vyombo vya dola vinavyoshughulikia kwa sababu yapo malalamiko
katika baadhi ya maeneo kama Mtwara kwamba wananchi wanapigwa na vyombo
vya dola?”
Waziri Mkuu alijibu: “Ni lilelile nililosema... mwishowe unaona anasema
vyombo vya dola vinapiga watu. Ukifanya fujo, umeambiwa usifanye hiki,
ukaamua kukaidi, utapigwa tu... hamna namna nyingine, maana wote
tukubaliane kwamba nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria.
“Sasa kama wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba ni imara zaidi... wewe
ndiyo jeuri zaidi watakupiga tu.... Mimi nasema muwapige tu, kwa sababu
hakuna namna nyingine... maana tumechoka.”
Pinda alisema Serikali imedhamiria kurejesha amani nchini ikiwamo mkoani
Mtwara na kuwataka Watanzania waiache Serikali ifanye kazi hiyo.
Alisema Serikali ina orodha ya watu wanaosemekana kuwa ni vyanzo vya
vurugu na matatizo yaliyotokea Mtwara na kushangaa wale wanaopinga
kukamatwa kwao.
“Lazima tuwakamate na kama katika kuwakamata watafanya jeuri, jeuri,
watapigwa tu kabla ya kupelekwa tunapotakiwa kuwapeleka, kwa sababu
hatuwezi kuendelea na hali hii, mkadhani kwamba tutafika tunapokwenda.
Nami nasema vyombo vya dola vijipange imara vihakikishe vinadhibiti hali
hii,” alisema.
Hata hivyo, jibu hilo lilipata upinzani wakati Mbunge wa Konde (CUF),
Khatibu Said Haji alipomwuliza Waziri Mkuu: “Hapo awali umetoa kauli
nzito ya kuliambia taifa hili kwamba wale raia wote, ambao watakaokuwa
wakaidi wapigwe tu na watapigwa tu; naomba ninukuu Katika Ibara ya 13 na
Kifungu cha 6B cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
“Ni marufuku kwa mtu yeyote aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kuteswa kama
mtu mwenye kosa, mpaka itakapothibitika anayo hatia kwa kutenda kosa
hilo.
“Pia ibara hiyohiyo Kifungu cha 6 E; kinasema ni marufuku kwa mtu
yoyote, kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazoweza
kumdhalilisha. Kwa kauli yako uliyoitoa huoni kwamba umevunja Katiba?”
Akijibu swali hilo, Pinda alisema ni lazima kutofautisha kati ya mtu
aliyekwishakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria... “Mimi
ninayemzungumza hapa ni mtu yule ambaye ameamua kufanya vitendo
hajakamatwa na ndiyo maana nilikwambia usiandamane... hapa mahali
hutakiwi kwenda wewe ukaamua kutumia mabavu kwa sababu mko wengi, ndiyo
maana nikasema, hawa watu tutashughulika nao hivyohivyo.”
Mbunge huyo hakuridhishwa na majibu hayo na kumtaka Waziri Mkuu kuyafuta.
Hata hivyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda aliingilia katika na kumweleza
mbunge huyo kuwa kila mtu alikuwa amemwelewa Waziri Mkuu na hakukuwa na
haja ya kuendelea na hoja hiyo.
Kabla ya swali lake la nyongeza, Mangungu aliuliza: “Ukisikiliza nyimbo
nyingi za taifa katika Afrika zinasema hekima, umoja na amani ndiyo ngao
zetu. Je, hali ambayo imejitokeza katika nchi yetu na matatizo
yaliyojitokeza Arusha na maeneo mengine kama Mtwara. Nini tamko la
Serikali?
Waziri Mkuu alijibu: “Swali lililoulizwa na Mheshimiwa Mangungu ni jambo
linalotugusa sisi wote. Suala la amani, ulinzi, utulivu ndiyo hasa tunu
ya kila nchi ingependa kuwa nayo. Ni kweli hivi karibuni kumejitokeza
vurugu za hapa na pale kwa hiyo angependa tuwaeleze Watanzania kama
Serikali tunafikiria tufanye nini.
Alisema ipo haja ya jukumu hilo kuachwa kwa viongozi wa kisiasa bila ya
kujali itikadi zao... “Yako mambo ambayo lazima tukubali kwamba ni
jukumu letu sisi wote na kila mmoja lazima azungumze lugha moja.
Ninyi wote ni mashahidi. Chadema waliposhinda hapa, wao walikuja
waziwazi, wakasema tutahakikisha nchi hii haitawaliki. Sasa, inawezekana
pengine ndiyo mwendelezo wa utekelezaji wa kauli hizo.
“La pili ni upande wa Serikali, lazima tuhakikishe kwamba wale wote
ambao kwa kweli wanajaribu kuvunja amani kwa namna yoyote ile, kazi
kubwa tuliyonayo ni kubanana, kupambana kwelikweli kwa njia zozote zile
zinazoonekana zinastahili.
“Sasa mimi ninaomba sana Watanzania, maana kila juhudi zinapoonekana
zinaelekea huko, unapata watu wengine wanajitokeza, unajua...unajua.
Acheni Serikali itimize wajibu wake kwa sababu jambo hili ni la msingi,
lazima tulilinde kwa nguvu zetu zote.
“Rai yangu kwa Watanzania kila mmoja ajue kwamba siku tukiingia katika
vurugu, hakuna mshindi. Wote tutaumia, sasa wote tuhakikishe hili jambo
tunalisimamia vizuri.”
Chadema waja juu
Akizungumzia kauli hiyo, Mkurugenzi Habari na Uenezi wa Chadema, John
Mnyika alisema: “Kauli ya Pinda inakiuka Katiba ya nchi na imethibitisha
kwamba matumizi mabaya ya vyombo vya dola na kusababisha mauaji ya raia
yana baraka za Serikali.”
Alisema kauli ya Pinda kama ilivyokuwa ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi zinatoa mwelekeo
kwamba mauaji ya Arusha yana baraka za Serikali.
Wanasheria wakerwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk
Hellen Kijo-Bisimba alisema Waziri Mkuu hakustahili kutoa kauli kama
hiyo.
Alisema Pinda hapaswi kuwa na jazba, bali anatakiwa kuwa na busara na
kuzungumza kwa kuzingatia sheria za nchi badala ya kutoa matamshi ambayo
siyo mwafaka kwa nchi inayoongozwa kwa kufuata sheria na taratibu.
Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Francis Stola alisema
kauli hiyo ya Waziri Mkuu, mbali ya kwenda kinyume cha Katiba na sheria
ya nchi, inaweza kuhatarisha amani.
Stola alisema matumizi ya nguvu kupita kiasi kudhibiti hali yoyote korofi hayaruhusiwi.
Chanzo - Gazeti la Mwananchi
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment