ASKARI Polisi watatu kati yao wawili wenye cheo cha Sajini na mwingine
Koplo wa Jeshi la Polisi mkoani Morogoro, wamefukuzwa kazi baada ya
kufikishwa mahakama ya Kijeshi wakituhumiwa kushirikiana na raia
kumbambikia mfanyabiashara fuvu la kichwa cha binadamu.
Wakati hayo yakijiri mkoani Morogoro, kwa upande wa Arusha, polisi
aliyekufuzwa kazi hivi karibuni kwa tuhuma za kukutwa akisafirisha bangi
magunia 18, ametoroka mikononi mwa polisi wakati akipekuliwa nyumbani
kwake, nje kidogo ya Jiji la Arusha kabla ya kufikishwa mahakama ya
kiraia.
Kwa upande wa askari wanaodaiwa kutumia fuvu kubambikia kesi,
wamefikishwa katika mahakama ya kiraia, wakidaiwa kumbambikia
mfanyabiashara Samson Mwita kwa kutumia fuvu wakitaka wapewe fedha suala
hilo lisifikishwe polisi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, aliwataja
askari hao ni D 4807 Sajini Sadick, D 4344 Sajini Mohammed wote kutoka
Kituo cha Polisi Dakawa, wilayani Mvomero na E 3861 Koplo Nula wa Kituo
cha Polisi Dumila, wilayani Kilosa.
Askari hao walifikishwa mahakamani wakiwa na mshirika wao Rashid Ally au
Sharifu Hassan (47) mkazi wa Mbagala, Dar es Salaam na kesi yao
imepangwa kutajwa Juni 3, mwaka huu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa akisimulia tukio hilo lilitokea Mei 7, mwaka
huu saa 12 :30 asubuhi katika mtaa wa Mgudeni, Kata ya Dumila, wilayani
Kilosa, alisema askari hao watatu na raia huyo walikula njama ya utapeli
kwa kumbambikizia mfanyabiashara maarufu kwa jina la ‘Mula’, fuvu
linalosadikiwa kuwa la kichwa cha binadamu.
Hata hivyo alisema, askari hao walijipangia wenyewe kazi bila ya idhini
ya wakuu wao na kwa kushirikiana na raia huyo waliamua kufanya vitendo
vinavyokwenda kinyume na maadili ya kazi ya kutaka kujipatia fedha kwa
njia ya kubambikiza kosa mtu mwingine.
Hata hivyo alisema, uchunguzi bado unaendelea ili kubaini mtandao wa
matapeli wanaoshirikiana na askari wa jeshi hilo na akawaomba wananchi
kuendelea kushirikiana na Polisi kwa kutoa taarifa na kuwafichua
wahalifu na askari wanaokwenda kinyume na utendaji wao wa kazi.
Hata hivyo, ilidaiwa kuwa askari hao walimwambia mfanyabiashara huyo
awapatie Sh milioni 25 kumaliza suala hilo kitu ambacho Mwita alikipinga
na kuwataka kulifikisha suala hilo Kituo Kikuu cha Polisi Morogoro.
Polisi wa Arusha Akizungumzia kutoroka kwa Koplo Edward aliyekamatwa
mkoani Kilimanjaro akisafirisha bangi, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Arusha, Liberatus Sabas alisema baada ya kufikishwa mahakama ya kijeshi
ilikuwa afikishwe katika mahakama ya kiraia kujibu mashitaka hayo.
Kamanda alisema alitoroka wakati akipekuliwa nyumbani kwake na Ofisa wa
polisi aliyekuwa akisimamia upekuzi huo, Inspekta Isack Manoni anahojiwa
kuhusiana na kadhia hiyo.
Edward akiwa na mwenzake mwenye namba G.2434 Pc George walikamatwa Mei
18 mwaka huu saa 5 maeneo ya Himo wakiwa na magunia 18 ndani ya gari la
Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) la Mkoa wa Arusha lenye namba za
usajili PT 2025 Toyota Land Cruiser wakitoka Arusha kwenda Holili
mpakani mwa Kenya.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa polisi wa Mkoa wa
Arusha, Liberatus Sabas alisema askari hao walishafukuzwa kazi na hatua
za kuwafikisha katika mahakama za kiraia zilikuwa zikiendelea kwa kosa
la kufanya biashara haramu ya bangi.
Sabas alisema askari hao walipelekwa nyumbani kwao eneo la Mrombo nje
kidogo ya jiji la Arusha, kwa ajili ya upekuzi ndipo Edward alitoroka na
kuwakimbia polisi ambao hawakufanikiwa kumkamata.
source:networked
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro







Post a Comment
Post a Comment