Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Wiki moja baada ya kuandikwa habari
kuhusu hatari ya kupata magonjwa, ikiwemo
kipindupindu inayowakabili wakazi
wanaoishi karibu na dampo la Pugu
Kinyamwezi na hatua ya kula kwenye
chandarua walioianzisha kupunguza kero ya
inzi, uongozi wa Jiji la Dar es Salaam
umezungumzia hali hiyo.
Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson
Kabwe amekiri kuwepo kwa tatizo la hatari
ya magonjwa kwa wakazi hao, lakini
amesema wakazi hao ni wavamizi wa eneo la
kutupa takataka kwa kuwa walilikuta dampo
wakati wakijenga eneo hilo hivyo wanapaswa
kuondoka.
Alisema kutokana na kuvamia eneo hilo,
adha wanazopata, wamejitakia wenyewe na
kuwaeleza kuwa dawa ya kumaliza adha hizo
ni kuondoka kama walivyoelekezwa na
Serikali mara nyingi kupitia viongozi
mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano, Dk Mohammed Gharib
Bilal.
"Wale ni wavamizi wa eneo la kutupa taka,
dawa ya mvamizi si kulalamika kwamba yupo
hatarini kupata magonjwa, ni kuchukua
hatua kukabiliana na tatizo hilo ikiwemo
kuondoka eneo hilo, serikali ilishawataka
mara nyingi waondoke lakini ndio tabia zetu
wananchi, hawataki kuchukua hatua hiyo,"
alisema Kabwe alipozungumza na gazeti hili
Ijumaa.
Alipoulizwa muda waliopewa wakazi hao
kuondoka, Kabwe alisema serikali kwa
kutambua kuwa wale ni wanadamu kama
wengine, wamepewa muda mrefu wa
kuondoka taratibu na kutaka wengine
wasiendelee kujenga eneo hilo lakini bado
hakuna waliochukua hatua hiyo.
Kabwe alisema masuala ya siasa pia
yanaingilia suala hilo, jambo linaloweka
ugumu kuchukua hatua na kuongeza kuwa
yanayoendelea Pugu ni kama yaliyotokea
Jangwani ambako pamoja na wakazi hao
kukumbwa na mafuriko na hata wengine
kupoteza maisha, waling'ang'ania kuishi
eneo hilo pamoja na kutengewa eneo la
Mabwepande, Kinondoni jijini humo.
Hata hivyo, Kabwe alipoulizwa kwanini
wakazi hao wa dampo la Pugu Kinyamwezi
lililopo wilayani Ilala wasitengewe na wao
eneo, alisema wakazi wa Jangwani kupewa
Mabwepande ilikuwa ni huruma ya Serikali
na kueleza kwamba, si kila wakati Serikali
itafanya huruma kama huo.
Kuhusu hali ya inzi na miundombinu mibovu
ya dampo hilo, Kabwe alisema kwa wiki mbili
sasa wamekuwa wakipiga dawa na hata siku
alipozungumza na mwandishi, Ijumaa
iliyopita, walipiga dawa.
Akizungumzia mpango wa kulifanya dampo
hilo kuwa la kisasa, Kabwe alikiri kweli kuwa
miundombinu ya dampo hilo haiko vizuri na
kueleza kuwa, mpango wa Serikali ni
kuliboresha unaendelea. Hata hivyo
hakutaka kueleza hatua ilikofikia zaidi ya
kudai mchakato uanendelea.
Miongoni mwa malalamiko ya wakazi hao ni
ahadi ya serikali kuwa dampo hilo lingekuwa
la kisasa, likizungushiwa ukuta, kuwekewa
dawa ya kuzuia madhara kwa binadamu.
Tofauti na hayo, dampo hilo liko wazi,
lililojaa nzi na wadudu wengine wa hatari, na
mvua zinaponyesha, maji machafu hutiririka
kwenye makazi ya watu.
Hivi karibuni mwandishi alifika katika
dampo hilo na kubaini kuwa, wakazi waishio
karibu na eneo hilo katika harakati za
kujikinga na maradhi na usumbufu
wanaoupata wa nzi majumbani, wamegundua
mbinu mpya za kukabiliana na tatizo hilo na
sasa familia zinakula chakula ndani ya
vyandarua.
Familia hizo hulazimika kufunga chandarua
ama sebuleni au barazani na baba, mama,
watoto na wanafamilia wengine huingia
ndani yake na kuzuia vizuri mianya ya nzi
kuingia kwa kuweka mawe ama mbao na
kisha hupata ahueni ya kula bila kuandamwa
na nzi.
Hata hivyo, pamoja na ugunduzi huo uliotoa
nafuu kwa kuwapunguzia maradhi, hali za
afya kwao bado ni tete kutokana na harufu
kali ya kemikali na taka zinazotupwa katika
dampo hilo pamoja na hatari ya kupata
saratani kutokana na moshi unaofuka mara
kwa mara.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo
waliozungumza na gazeti hili katika makazi
yao umbali wa kutengwa na barabara
inayoingiza magari yanayotupa taka eneo
hilo, walilalamikia hali hiyo na kueleza kuwa
wameamua kugundua mbinu hiyo ili
kunusuru afya zao.
Maua Hamis (22), mkazi wa Mtaa wa
Kichangani Majohe, alisema watoto katika
familia wamekuwa wakiugua vifua, matumbo
ya kuhara, mafua na malaria kila kukicha
kutokana na madhara ya dampo hilo na
familia takribani zote, sasa wanalazimika
kununua vyandarua zaidi ya viwili kwa ajili
ya matumizi hayo.
"Hapa kwetu 'neti' (chandarua) hazina kazi
ya kuzuia mbu tu usiku au mchana, bali
tunazo zaidi ya mbili na familia nyingi
tunazitumia kwa chakula pia, tunazifunga
kwa kamba ama misumari ukutani sebuleni
ama barazani na tunaweka mawe, vipande
vya miti au mbao kwa chini ili nzi wasiingie
kisha tunaingia wote haraka haraka na
kuanza kula tukiwa ndani ya neti," alisema
Maua.
Alisema mara zote wanapotaka kula iwe chai,
mlo wa mchana ama usiku wanalazimika
kufanya hivyo kwa kuwa jambo la ajabu ni
kwamba nzi hao hawalali hata usiku ni
wasumbuu kama wanavyofanya mchana.
Mwandishi akiwa eneo la tukio, alishuhudia
wingi wa nzi hao katika bustani za mboga
katika makazi ya watu, kwenye magudulia ya
maji, ukutani na walikuwa wakitua na
kuruka kwa wingi kwa watu, akiwemo
mwandishi wa habari hizi. Awali waandishi
walipofika eneo hilo na kuvuta hewa,
walianza kuumwa matumbo na vichwa.
Watoto walionekana pembezoni mwa dampo
wakicheza huku nzi wakiwa midomoni, puani
na maeneo mengine ya mwili, maji machafu
kutoka katika dampo yakiwa yanapita na
kuingia katika makazi yao huku watoto hao
wakicheza kwenye maji hayo bila viatu.
Baadhi ya watu walionekana katikati ya
dampo wakiokota vyuma chakavu, chupa na
vifaa vingine bila vifaa vya kinga.
Moses Lucas, mkazi wa eneo hilo alidai hali
za afya kwa wakazi wa eneo hilo ni tete
kutokana na mazingira yaliyopo hasa nyakati
hizi za mvua na kuongeza kuwa, japo
wanakula kwenye chandarua lakini watoto
wanacheza kwenye maji machafu kutoka
katika dampo hilo.
Lucas alisema kumeundwa kamati ya
wananchi kushughulikia kero hizo, lakini
alidai serikali imekuwa ikiwapiga danadana
katika kushughulikia kero hizo ikiwemo
kuboresha dampo.
Baadhi ya watoto waliozungumza na
mwandishi, Rashid Abdallah (12) na Bariki
Massawe (11) walisema kwa nyakati tofauti
kuwa wanalazimika kufukuza nzi ndani kwa
muda wa nusu saa kabla ya kuweka neti na
kula chakula, pia moshi, harufu na maji
machafu yanahatarisha afya zao.

Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala,

Hifadhi blog hii kwenye simu yako ili upate habari zote kwa urahisi zaidi

Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
http://www.facebook.com/kibonajoro

Post a Comment

 
Top