Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Profesa Mark Mwandosya amethibitisha kuwa sauti iliyosambaa mitandaoni akieleza mtazamo wake juu ya mwenendo mzima wa mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM, ni sauti yake halisi.
Kwa mujibu wa gazeti la Mtanzania lililoongea naye, Mwandosya amethibitisha hayo akiwa katika harakati za safari yake ya kuelekea nchini India.
Katika sauti inayosikika kwenye mitandao, Profesa Mwandosya anasikika akieleza kuwa Kamati ya Usalama na Maadili iliendesha mchakato huo kinyume cha katiba kwa kuwa walikuwa na majina matano hata kabla ya kufanya usaili wao.
“Majina hayo matano ni ya January Makamba, Amina Salum Ali, Asha Rose Migiro, Bernard Membe na John Magufuli. Kilichotokea ni kitu cha ajabu kwa sababu majina hayo yalishatoka kabla hata kikao cha maadili hajikatoka, kinaendelea kikao majina sisi tunayo,” anasikika Mwandosya.
“Wanasema haya ndiyo yatakwenda mpaka mwisho, mmenielewa eeh, mfuatilie sana, mwenyekiti alikuwa na majina yake mfukoni na Kamati ya Maadili, Kamati Ndogo ya Maadili ina majina yake,” aliendelea Mwandosya.
Mwandosya alitoa maoni yake pia kuhusu uchaguzi wa Magufuli, na kudai kuwa mgombea huyo haifahamu vizuri CCM kwa kuwa hakuwahi kushika nyadhifa yoyote ya maana ndani ya chama hicho.
“Ni rafiki yangu Magufuli, lakini hajawahi kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama, hajawahi kuwa mjumbe hata wa tawi, hajawahi kuwa Mwenyekiti hata wa wilaya, CCM haijui, lakini sasa ndiye atakuwa mwenyekiti wa Chama cha Mampinzi, ndivyo chama kinavyokwenda.”
Mwandosya alisika akiponda mwenendo mzima wa kikao cha Halmashauri kuu baada ya kuyapata majina matano kwamba hakikuwa na mvuto na kwamba hata mwenyekiti wa chama hicho alikuwa anajichanganya.
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment