Mwigizaji Wema Sepetu amewataka watu wanomsakama kwa maneno waache apumzike kufanya hivyo kwani yeye ni binadamu kama ilivyo kwa wengine na anaumia kama wanavyoumia wengine.
Wema ambaye alikuwa akizungumzia ujumbe aliouandika hivi karibuni katika mtandao wa Instagram kuhusu kutopata mtoto, anasema kuna watu hawajali maumivu yake ndiyo maana kila kukicha wanamkashifu.
“Watu hao hawawezi kutafuta jema langu na kunisifu, kazi yao kunisanifu na kunikashifu kwa vitu wasivyovifahamu wala kuwa na ukweli navyo.Nimevumilia mengi namna sasa imetosha,” anasisitiza dada huyo aliyewahi kuwa Miss Tanzania na kuongeza kuwa kwa sababu hiyo, hivi sasa hasomi magazeti ya aina yoyote akiogopa kuharibu ‘hali ya hewa ya siku’ husika, kwani watu hawajali wanaandika chochote bila kufikiria madhara gani.
Akizungumzia tuhuma za kuwalipa fedha waandishi wa habari ili aandikwe kwa lengo la kupata ‘Kiki’ mwanadada huyo anasema hayana ukweli wowote na kuongeza kuwa kama kuna anayefanya hivyo hana akili.
Anasema haoni sababu ya kutoa fedha ili aandikwe ilhali kuna watu kazi yao ni kuangalia anafanya nini na kumuandika, ingawa amekiri kuwa anawafahamu baadhi ya waandishi kama binadamu.
Anasema watu wakimuona yupo karibu na watu hao wanaamini anawapa fedha wamuandike, kwa lengo la kumpaisha jina lake.
“Niliwahi kuwa mrembo mkubwa tu, natambulika na watu wengi, mwigizaji, naendesha kipindi katika runinga, kwa kila hali lazima nitaandikwa tu, lakini siyo kwa kuwapa watu fedha ili wanichafue eti... nakuza jina , hapana jina langu ni kubwa tayari, ” anasema Wema.
Mkali huyo wa filamu ikiwamo ile inayosubiriwa kwa hamu ya ‘Day after Death’ aliyoigiza na mwigizaji mahiri wa nchini Ghana, Van Vicker, anasema anahitaji kuwa na wakati wake binafsi, lakini kutokana na kuwa na jina hana hiyo nafasi kwani kila anachokifanya kinafuatiliwa na jamii, hivyo katika hali kama hiyo hakuna haja ya kulipa fedha aandikwe.
Kuhusu siasa Wema anasema yeye ni shabiki mkubwa wa CCM, ingawa kuna baadhi ya vitu vinamkera na inabidi vifanyiwe kazi ili kujiimarisha.
Anasema anaupenda utendaji wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete kutokana na vitu vingi alivyofanya katika kipindi cha miaka 10 aliyokuwa madarakani na ingekuwa amri yake angerudi tena.
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment