Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This
KWAKO
Miss Sitti Mtemvu mwakilishi wa Wilaya ya Temeke na sasa wewe ni Redds Miss Tanzania 2014.
Vipi uko poa? Raha ya ushindi unaionaje? Najua sasa hivi bado hujatulia, unatafakari kwa makini juu ya shilingi milioni 18 ulizokabidhiwa kama mshindi, tafakari mama, ndiyo muda wake.
Ukitaka kujua hali yangu, mimi ni mzima wa afya, namshukuru Mungu. Hongera kwa ushindi uliopata japo nimesikia kuna baadhi ya watu hawakukubaliana na matokeo.
Huo ndiyo ushindani, lazima kila mmoja awe na mtazamo wake lakini mwisho wa siku, hawakatazwi kusema na inawezekana pia wana hoja.
Moja kwa moja nikiachana na salamu, nataka kuzungumza na wewe kuhusiana na maisha yako baada ya huo ushindi wa kishindo ulioupata usiku wa Oktoba 10, mwaka huu ndani ya Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar.
Yawezekana uliwaza kabla au hukutarajia kushinda lakini tayari umeshatangazwa wewe ndiye mshindi. Swali langu la msingi kwako ni je, umejipangaje baada ya ushindi huo?Hautabaki historia ya mara moja na kusahaulika kama wenzako? Kumbukumbu inaonyesha wapo wenzako wengi waliopotea ndani ya muda mfupi tu baada ya ushindi.

Hatukuwasikia tena wakifanya mambo mbalimbali ya kijamii au kuanzisha taasisi mbalimbali ambazo zitamfanya azidi kuonekana muhimu katika jamii. Kutwaa ubingwa na kukaa kimya, kunapoteza maana kabisa ya ushindi.
Sijachelewa, taji ndiyo kwanza la motomoto. Weka mikakati yakinifu, jiwekee malengo ya taji lako na fedha ambazo umekabidhiwa. Wekeza katika miradi mbalimbali, wewe mwenyewe ni wakati wako wa kutumia fursa au vipaji mbalimbali ambavyo vinaweza kubebwa na taji lako, ukavionyesha na Watanzania wakakuunga mkono.
Nikirudi kwako Mkurugenzi wa Lino International Agency, Hashim Lundenga, hizi kasoro za sijui matokeo yamepangwa, mshindi alijijua kabla, mshindi kukosea maelekezo ya majibu na mambo mengine kwa nini viendelee kuwepo?

Kwenye interview yoyote duniani, mtu anapokosea maelekezo ya kujibu swali huwa inaaminika amefeli hata kama awe amejibu vizuri kwa kiasi gani? Sitti aliulizwa  na majaji kuwa atatumia lugha gani kujibu maswali ya papo kwa papo akasema atatumia Kingereza, alipojibu akatupia na Kifaransa je, hakufeli hapo?
Achana na yale mabango ya Sitti ambayo yalionekana yakionyesha kwamba ni mshindi pale ukumbini kabla ya kutangazwa, lakini vipi kuhusu lile gari la Hammer ambalo lilikuja maalum kwa ajili ya kumpokea mshindi, walijua kama atashinda nini? Lundenga wewe!!
Nafikiri ni wakati sasa wa kubadili gia katika sura nzima ya mashindano hayo kwani ninavyoona mimi, msisimko wake unaendelea kupungua siku hadi siku. Tunahitaji shindano hili liboreshwe ili tuwe tunampata mshindi atakayekwenda kuchuana na kushinda Miss World na siyo kila siku ziwe blablaa tu!
Wasalaam, Erick Evarist.
Bonyeza Hapa

Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala,

Hifadhi blog hii kwenye simu yako ili upate habari zote kwa urahisi zaidi

Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
http://www.facebook.com/kibonajoro

Post a Comment

 
Top