Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linamng’ang’ania mfanyabiashara maarufu wa Wilaya ya Mvomero, Johnson Damian Mkude (39) akituhumiwa kumkata kichwa mdogo wake wa kuzaliwa, Mathias kisha kuondoka nacho kwenda kwa mganga kwa kile kilichodaiwa ni kufanyiwa dawa ili awe bilionea, mkasa wote huu hapa. Tukio hilo ambalo kwa sasa ndiyo gumzo mkoani hapa lilijiri usiku wa Agosti 3, mwaka huu katika mashamba ya Kata ya Mlali ambapo ndugu wa marehemu waliokuwa wakimsaka ndugu yao walifanikiwa kuona kiwiliwili Agosti 6, mwaka huu.
MWILI WAZIKWA KATIKA SHAMBA LA MTU
Mwandishi wetu alifika eneo la tukio na kushuhudia kiwiliwili kikiwa kimeharibika vibaya. Ilibidi baba wa marehemu, mzee Damian Mathias Mkude (63) amwombe mmiliki wa shamba hilo lililopo kwenye Kijiji cha Mbalala, Kata ya Mlali kumzika mwanaye hapo ambapo alikubali.
BABA WA MAREHEMU
Akizungumzia tukio hilo kwa uchungu, baba wa marehemu mzee Mkude alisema:”Mwezi mmoja kabla ya tukio, Johnson alinichonganisha na Mathias, nakiri hadi marehemu anakufa nilikuwa sina uhusiano naye mzuri kutokana na maneno aliyoniambia kaka yake
Ofisa wa polisi akifafanua jambo kwa wananchi eneo la tukio.
“Lakini nilipomuuliza kuhusu hayo maneno, Mathias alikanusha, nikaamua kuyafanyia uchunguzi. Wakati naendelea na uchunguzi Agosti 3, mwaka huu, majira ya jioni, giza halijaingia niliwaona wanangu (Jonson na Mathias) wamepakizana kwenye bodaboda.
“Siku hiyohiyo, saa 5 usiku, mke wa Mathias, Revina Evarist akaja kwangu na kunijulisha kwamba mumewe hajarudi nyumbani na si kawaida yake kufika muda huo. Tulipompigia simu hakuwa hewani. Kwa vile nilimuona akiwa na kaka yake, nikampigia yeye lakini simu yake ilizimwa.
“Ilipofika saa 7 usiku tukaamua kwenda kwa kaka yake, tukamkuta. Nilipomuuliza mdogo wako yuko wapi akasema hajui. Akajiunga na sisi, tukaendelea kumtafuta mdogo wake kwa zaidi ya siku 2 bila mafanikio,” alisema mzee huyo.
Mke wa marehemu, Mathias, Revina Evarist akihuzunika kwa kumpoteza mumewe.
MAITI ILIVYOONEKANA
Mzee huyo akasema Agosti 6, mwaka huu alipata taarifa kwamba kuna maiti imeonekana kwenye mashamba ya Mlali.
“Nilishtuka sana kusikia hivyo, nikamtuma mkwe wangu, mume wa mtoto wangu mkubwa na mtoto wa dada yangu, Gasper Msimbe. Walisafari hadi Kata ya Mlali kushuhudia maiti hiyo.
“Walipofika waliikuta maiti haina kichwa lakini walimtambua kuwa ni Mathias kwa nguo na viatu. Walinijulisha haraka ambapo nilikwenda eneo la tukio. Nilipofika niliumia sana kushuhudia mwanangu asiyekuwa na hatia kauawa kikatili huku mwili wake uliokuwa hauna kichwa ukitoa harufu kali kwa kuharibika.”
Revina Evarist akilia kwa uchungu.
BAADA YA MAZISHI
“Sasa kilichonishangaza ni kwamba, baada ya mazishi kule shambani, zimesikika tetesi kuwa, Johnson ndiye aliyemchinja mdogo wake na kutoweka na kichwa kwa imani za kishirikina ili awe tajiri mkubwa.
“Nikaambiwa anashikiliwa kwenye Kituo cha Polisi Mzumbe (kabla ya kupelekwa mkoa). Nilikwenda, nikamkuta amewekwa chini ya ulinzi huku akiwa na hirizi alizokamatwa nazo akiwa kwa mganga wa kienyeji eneo la Sangasanga, Mvomero.”
BABA AOMBA KICHWA CHA MWANAYE
“Pale kituoni, polisi walinitaka nimsalimie lakini nikakataa mpaka arudishe kichwa cha mdogo wake. Tena naliomba jeshi la polisi kumbana Johnson ili kama kweli amechukua kichwa cha mdogo wake akirudishe nikizike hapa nyumbani Kijiji cha Nyandila,” alisema mzee huyo.
Diwani wa Kata ya Nyandila (Chadema), Peter Joseph Zengwe.
MKE WA MTUHUMIWA AZUNGUMZIA KUFUNGA NDOA
Uwazi lilifika nyumbani kwa Johnson ambapo mke wa mtuhumiwa, Mchilo Peter (33) alikiri mumewe kuswekwa mahabusu akituhumiwa kumkata kichwa mdogo wake.
Alipotakiwa kueleza chochote kuhusu tukio hilo, mwanamke huyo alisema kwa mafumbo:
“Huko ni kukosa elimu, kwa nini mganga akudanganye. Kama ni gari mbona yeye hana, mume nimeanza kuishi naye tangu mwaka 2000, namwambia tufunge ndoa hataki, Jumapili kusali hataki, yuko bize kusaka pesa.
“Siku ya tukio kachukua pesa zote ndani zaidi ya shilingi laki 7. Leo baada ya njaa kuwa kali nimeamua kufungua duka licha ya kupokea vitisho kwamba kuna kundi la watu linataka kuvamia duka kwa lengo la kuchoma moto kama hawatapewa kichwa cha Mathias,” alisema mama huyo.
Alipoulizwa kuhusu mali wanazomiliki, alisema wana nyumba, duka na nguruwe wawili.
MTUHUMIWA ALIJULIKANAJE?
Kwa mujibu wa Diwani wa Kata ya Nyandila (Chadema), Peter Joseph Zengwe, Agosti 15, mwaka huu baada ya mauaji hayo kutokea, vijana wawili, Amos na Mohamed Chali walikamatwa na polisi wakidaiwa kuhusika na mauaji hayo.
Marehemu Mathias enzi za uhai wake.
“Siku chache baada ya mauaji hayo, Amos na Mohamed Chali walifuja pesa kwa kunywa pombe kupita kiasi ambapo mmoja aliropoka kilabuni kwamba walilipwa fedha nyingi kwa kumuua Mathias.
“Baada ya majigambo hayo, watu wakatoa taarifa polisi na wahusika wakakamatwa na ndiyo waliomtaja Johnson,” alisema diwani huyo.
MGANGA AINGIA MITINI
Uwazi lilifanikiwa kufika Sangasanga kwa mganga huyo na kuambiwa kuwa alikimbia kwa kutumia mlango wa nyuma baada ya polisi kufika kwa ajili ya kumkamata.
MATUMIZI YA KICHWA
Habari zilizoenea kwenye kijiji alichokuwa akiishi marehemu Mathias zinadai kwamba, mganga huyo ambaye jina halikujulikana mara moja, alimwambia mtuhumiwa kuwa, angekifanyia dawa kichwa hicho ambapo angekiweka dukani ili kuvuta wateja wengi kwa siku, hivyo ndani ya mwaka mmoja tu angekuwa bilionea.
Credit GPL
Like ukurasa wetu wa facebook ili habari ziwe zinakuijia punde tu zinapoweka kwenye mtandao huu bonyeza hapa
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment