Katibu mkuu wizara ya mambo ya
nje wa Uganda, Balozi James Mugume, amesema kuwa Uganda haitishwi na
vikwazo ilivyowekewa na Marekani kama hatua ya kupinga sheria yake kali
kuhusu mapenzi ya jinsia moja.
Mwandishi wa BBC mjini Kampala, Isaac Mumena
anasema kuwa Balozi Mugume ameelezea kuwa serikali ya Uganda hata hivyo
itafanya mazungumzo na Marekani ili kufafanua hatua waliyochukua.
Serikali imesisitiza kuwa vikwazo hivyo
havitakuwa na athari kubwa kwa nchi hiyo na pia imekanusha madai ya
mashirika ya kijamii kuwa tayari sheria hiyo imechochea ongezeko la
dhuluma dhidi ya wapenzi wa jinsia moja.
Sheria hiyo iliyotiwa saini na Rais Yoweri
Museveni mwezi Februari inasema kuwa wanaopatikana na hatia mara mbili
ya kuhusika na mapenzi ya jinsia moja watafungwa maisha jela.
Sheria hiyo pia inaharamisha vitendo vya mapenzi
ya jinsia moja pamoja na kuwataka wananchi kuwashitaki watu wanaohusika
na vitendo vya mapenzi ya jinsia moja kwa maafisa wakuu.
Ikulu ya White house imelaani sheria hiyo ikisema kuwa inakwenda kinyume na uhusiano kati ya nchi hizo ikitoa wito wa sheria hiyo kufutuliwa mbali.
Waziri wa mambo ya nje John Kerry, amefananisha sheria hiyo na sheria za utawala wa zamani wa kinazzi nchini Ujerumani.
Chanzo bbc
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment