Hivi
karibuni nimeshuhudia kusambazwa kwa taarifa mbalimbali kupitia ujumbe
mfupi wa simu (sms) na mitandao ya jamii zikinihusisha na tuhuma
mbalimbali.
Napenda kuufahamisha umma
kwamba taarifa zote zilizotolewa kupitia njia hizo ni za uongo, chuki,
na uzushi. Kilichonisikitisha sana ni kuona kuwa uzushi huo unachochea
kuifarakanisha jamii yetu kwa misingi ya ukabila jambo ambalo ni hatari
kwa umoja na mshikamano ambao Tanzania tumejitahidi sana kuujenga, na
mtu yeyote anayediriki kuleta uchochezi wa kikabila hastahili kuwa
kiongozi wa ngazi yoyote katika taifa letu.
Mimi ni miongoni mwa
Watanzania walio mstari wa mbele wanaomuunga mkono Mhe. Dkt Jakaya
Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika
kusisitiza kuwa rasilimali za asili zilizopo nchini ni mali ya
Watanzania na ni lazima wawe wamiliki wakuu wa rasilimali hizo ikiwa ni
pamoja na gesi asilia. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,
aliwahi kusema mwaka 1974 katika andiko lake la “Ujamaa ni imani” ukurasa wa 31, kwamba: “madini au mafuta yalio chini ya ardhi, n.k. vitu hivi ni mirathi ya wananchi wote”.
Katika miaka ya hivi karibuni
dhana hii ya Watanzania kuwezeshwa na kumiliki uchumi wa nchi yao
imetambuliwa na Serikali na Chama tawala kama ifuatavyo:
Sera ya Taifa ya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 inasema kwamba:
- Aya ya 1.5 TAFSIRI YA WANANCHI
“Walengwa wa Sera ya
Uwezeshaji ni Wananchi. Makampuni ya Wananchi ni yale ambayo
yamesajiliwa Tanzania ambayo walengwa wanamiliki asilimia isiyopungua
hamsini ya hisa zote za makampuni hayo. Sera ya Uwezeshaji itajumuisha
wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyakazi na wafanyabiashara katika sekta
mbalimbali na makundi mengine.”
- Aya ya 3.1 DIRA
“Uwezeshaji wa
wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi ni sehemu ya
Dira ya maendeleo ya Taifa kufikia mwaka 2025. Kufikia wakati huo,
sehemu kubwa ya uchumi wa Tanzania inatarajiwa kumilikiwa na Watanzania
wenyewe.
- Aya ya 4.1.2 TAMKO LA SERA
“Jitihada za kuwawezesha
wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi nchini ni muhimu
ziendane na ukuaji wa uchumi unaojumuisha na kunufaisha Watanzania
wengi, kuongeza vipato vyao pamoja na kuinua hali zao za maisha.”
Nayo Sheria ya Taifa ya Uwezeshaji Kiuchumi ya mwaka 2004 (National Economic Empowerment Act, 2004) katika utangulizi inasema:
“Economic empowerment is a
central means for bringing about economic growth and social justice
among our people that is necessary for the promotion of peace,
tranquility and social stability that has characterized our society.”
Tafsiri yake ni kama ifuatavyo:
“Uwezeshaji wa Wananchi
kiuchumi ni njia kuu ya kukuza uchumi na kuleta haki miongoni mwa jamii,
mambo ambayo ni ya lazima katika kudumisha amani, utulivu na
mshikamano, ambayo ni tunu ya asili ya jamii yetu.”
Chama tawala, CCM katika “Mwelekeo wa Sera za CCM katika miaka ya 2010 hadi 2020” kimetamka kwamba:
- Aya ya 84 UWEZESHAJI WA WANANCHI KIUCHUMI
‘’Chama Cha Mapinduzi katika
sera zake za msingi kama zilivyoainishwa katika Mwelekeo wa Sera za CCM
katika Miaka ya Tisini na Mwelekeo wa Sera za CCM katika miaka
2000-2010, kimetamka bayana kwamba, mkakati mkuu wa uwezeshaji wa
kiuchumi wa wananchi ni ule unaohakikisha kwamba wananchi wenyewe
wanamiliki na kuendesha uchumi wa nchi yetu ama mmoja mmoja, kwa kupitia
vyama vyao huru vya ushirika wa aina mbalimbali au kwa kupitia
makampuni ya wananchi ya ubia ambamo maelfu ya wananchi watanunua hisa”
- Aya ya 103
“Wakati umefika wa kuweka
mazingira bora ya upendeleo kwa Watanzania, kama inavyofanyika katika
nyanja za kimataifa kwa mfano katika utoaji wa kandarasi za ujenzi,
manunuzi n.k. Kuwapendelea Watanzania katika ajira na biashara nchini ni
njia mojawapo ya kuwawezesha kiuchumi.”
Kwa msingi huo nimekuwa
nikiishawishi Serikali kutekeleza sera na sheria ya uwezeshaji ili
kuwashirikisha Watanzania kikamilifu katika uchumi wa Taifa, na kwa sasa
hasa katika uchumi wa gesi asilia, ili kudumisha amani na utulivu
katika nchi yetu.
Jitihada zangu zimekuwa
zikipingwa na kiongozi wa moja za Wizara za Serikali na amekuwa akitumia
mbinu na visingizio mbalimbali. Naamini kwamba usambazwaji wa uzushi
unaofanyika sasa ni mwendelezo wa mbinu hizo chafu. Mtanzania yeyote
hastahili kuwa kwenye uongozi katika ngazi yoyote kwa staili ya kudharau
na kutukana Watanzania akidhani kwamba kwa kufanya hivyo atajijengea
umaarufu. Jambo ambalo Watanzania wengi wanajiuliza ni kwamba ujeuri
tunaoushuhudia unatokana na ulevi wa madaraka au ulevi wa fedha ama
vyote viwili?
Rai yangu kwa Watanzania ni
kupuuza uzushi unaosambazwa, na kwamba wasikubali kuondolewa kwenye hoja
ya msingi ya kutaka kujua namna serikali yao itakavyotekeleza sera na
sheria ya uwezeshaji ili kuhakikisha kuwa inawashirikisha katika
mchakato mzima wa uchumi wa gesi asilia, kuanzia hatua ya utafutaji na
uchimbaji (up-stream) hadi uchakataji na usambazaji (midstream and
downstream).
Na kwa wale wanaotumiwa na
kiongozi huyo ningependa kuwasihi wawe na uzalendo na mapenzi kwa nchi
yao na wakatae kutumiwa kwenye mambo ya uongo yasiyo na tija kwa taifa
letu.
Kinachonipa faraja katika
juhudi zangu za kutetea maslahi ya Watanzania ni maneno ya Mhe. Rais
Dkt. Kikwete aliyoyasema mnamo mwaka 2009 kwamba:
“Midomo ya Wanadamu imeumbiwa
kusema na wakati mwingine wanasema wanachokifikiria wao hata kama huo
siyo ukweli, lakini watauamini, wataueneza uongo huo na watakuhukumu kwa
uongo wao.”
Dkt Reginald Mengi
28 Mei, 2014
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment