Tangu
ugonjwa wa homa ya dengue uibuke mkoani Dar es Salaam na baadaye maeneo
mengine ya nchi, wananchi wamekuwa wakijiuliza maswali mengi yenye
utata ambayo sasa yamepata majibu ya wataalamu.
1. Kwa nini mbu wengine wakiwamo wanaoambukiza malaria hawawezi kuambukiza dengue?
Mtafiti
wa tabia za mbu kutoka Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI), Dk Nicholaus
Govela alisema mbu anayeambukiza homa ya dengue, Aedes Egypti, hawezi
kubeba vimelea vya malaria wala yule anayeambukiza malaria hawezi
kuambukiza dengue kutokana na maumbile yao.
Dk Govela alisema fiziolojia ya mwili wa mbu haiwezi kuruhusu Aedes Egypti kubeba virusi vya mbu mwingine.
“Ndiyo maana mbu hawezi kuambukiza Virusi vya Ukimwi,” alisema.
2. Kwa nini mbu wa dengue huuma mchana?
Dk Govela
alisema suala hilo bado linahitaji utafiti zaidi kwa sababu kati ya
aina tatu za mbu wanaosababisha dengue, hakuna utafiti uliofanyika kujua
tabia zao wote.
Aina hizo ni Aedes Egypti, Aedes Albokictus na Aedes Africaans.
Alibainisha
kuwa katika tafiti zinazofanyika, IHI iliwahi kubainika kuwa Aedes
African ambaye pia anaambukiza dengue huuma usiku.
Alisema
wengi wanamwelezea mbu huyu kwa kumlinganisha na tabia za mbu wa Japan,
China na America ya Kusini lakini inawezekana huyu aliyepo hapa ni mpya
tofauti na wa nchi za nje.
3. Je, dawa inayopulizwa inafaa kuwaangamiza?
Dk Govela
alisema inawezekana ndiyo au hapana, lazima hili pia lifanyiwe utafiti
kwa kuwa upo uwezekano wa mbu hawa kujenga usugu wa dawa kwa kuwa
wamekuwapo nchini kwa miaka mingi.
Alipongeza
uamuzi wa Serikali wa kupuliza dawa kwenye mabasi ya mikoani lakini
bado alihoji iwapo imefikiria udhibiti kuanzia katika viwanja vya ndege
na iwapo itawezekana kuzuia watu wanaokwenda mikoani wakiwa tayari
wameambukizwa.
4. Je, kuna watu wanaougua dengue bila kuonyesha dalili?
Mtafiti
huyo alisema wapo wanaougua bila kuonyesha dalili na wanaendelea
kuambukiza... “Hawa mara nyingi hawaendi hospitali lakini wanakuwa na
virusi mwilini,” alisema.
5. Kuna aina ngapi za virusi vya dengue?
Dk Govela
alisema zipo aina nne za virusi vinavyoambukiza dengue. Alivitaja kuwa
ni den 1, den2, den 3 na den 4. Hadi sasa, wanasayansi hawajaweza
kubaini ni virusi vya aina gani vinasababisha homa hiyo kwa Tanzania.
“Ndiyo maana tunahitaji kufanya tafiti zaidi,” alisema.
6. Je, juisi ya majani ya papai ni tiba ya dengue?
Ofisa wa Taaluma na Udhibiti wa Magonjwa wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Grace Saguti alisema haijathibitishwa kisayansi.
Dk Saguti
alisema ili tiba ikubalike, lazima ithibitishwe na hakuna namna mbadala
ya kuiruhusu itumike kabla ya kujua madhara na faida zake. Alisema
mpapai unaongeza vitamini A na hivyo kuimarisha kinga ya mwili, lakini
si kutibu virusi vya dengue ambavyo kwa asili yake havina dawa.
7.Mbu wa dengue wako Dar es Salaam pekee?
Mtaalamu
wa IHI alisema mbu huyo anaishi katika maeneo ya kitropiki, hivyo huenda
yupo hata katika mikoa mingine. Alisema kwa tabia, aedes africans
anafanana na mbu aina ya culex ambaye anapatikana katika mikoa mingine,
hivyo hata huyo anaweza kuwapo huko pia... “Lazima ufanyike utafiti ili
tujue iwapo mbu huyo hawezi kuzaliana katika mikoa mingine,” alisema.
8. Kwa nini aedes hupenda maji masafi yaliyotuama?
Dk Govela
alisema ni kutokana na asili ya maumbile yao. Mbu hao huamini maji
masafi yaliyotuama huwapa joto zaidi kwa ajili ya kutaga mayai.
“Lakini
si lazima wawe wanazaliana zaidi katika maji masafi kwa sababu wana
tabia ya kubadili tabia. Kwa mfano, anopheles wanaoeneza malaria nao
walipenda maji masafi awali, lakini kwa sasa wamebadilika wanazaliana
hata kwenye maji machafu,” alisema
9.Kwa nini wahudumu wa afya wanaathirika zaidi?
Daktari
Kiongozi na Mtaalamu wa Homa ya dengue, Mrisho Lupinda alisema nao ni
binadamu kama wengine na wanaishi maeneo hatarishi yenye mbu kama watu
wengine.
10. Kwa nini panadol pekee ndiyo inatibu dalili za dengue?
Dk
Lupinda alisema dawa nyingine za maumivu yaani Diclopar, Diclofenac na
Aspirini huingiliana na mfumo wa chembe hai nyeupe za damu na huweza
kusababisha chembe hizo kupungua mwilini. Dawa hizo huchochea
kutengeneza sumu ambayo huathiri baadhi ya ogani za mwili.
Ugonjwa wasambaa
Homa ya
dengue imesambaa katika maeneo mbalimbali nchini na kutoka Shinyanga,
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa, Fredrick Mlekwa amesema kumetokea
kifo cha mtoto aliyekuwa na dalili zote za ugonjwa huo.
Huko
Arusha, mkazi wa Maji ya Chai, Frank Nnko (30) amelazwa katika Hospitali
ya Mkoa ya Mount Meru akitokea Hospitali ya Wilaya ya Meru akiwa na
dalili za homa hiyo.
Zanzibar,
wagonjwa watatu wanaodhaniwa kuwa na homa ya dengue wamelazwa katika
Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja. Waziri wa Afya, Juma Duni Haji alisema
wagonjwa hao wana dalili za ugonjwa huo.
Mtu mmoja
amelazwa katika Hospitali ya Tumbi akiwa na dalili za dengue, akiwa na
maumivu ya kichwa na kutoka damu puani, Ofisa Habari wa Hospitali hiyo,
Gerald Chami alisema mgonjwa huyo mwenye umri wa miaka 30, alitokea
Mbezi Wilaya ya Kinondoni.
Credit: Mwananchi
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro







Post a Comment
Post a Comment