KIJANA Lalmohan Soren (17) amekata sehemu ya ulimi wake kwa wembe
kutokana na imani kali ya dini kwa Mungu wake wa Kihindu. Soren
aligundulika kukata sehemu ya ulimi wake nyakati za asubuhi alipokaa
ndani ya msikiti wa Mahedevgarha katika eneo la Dugda, Jharkhand ndipo
waumini walipoona damu imetapakaa sakafuni.
Waumini hao waliacha kusali na kuangalia zaidi ndipo wakakuta ulimi
huo upo ndani ya bakuli pembeni ya Soren aliyekuwa hawezi kuzungumza.
Sambamba na bakuli hilo waliona karatasi iliyoandikwa "nimeukata ulimi
wangu na kuutoa kama sadaka kwa Mungu Shiva".
"Tafadhali msiniondoe hapa msikitini, nataka nikae hapa miguuni kwa Mungu".
Soren alitoa sadaka ulimi wake kwa Mungu Shiva kwa lengo la
kumfurahisha na pia kutimiza ndoto zake. Kutokana na tukio hilo,
kiongozi wa msikiti huo alitaarifiwa na akafanikiwa kumshawishi Soren
akubali kupelekwa hospitali.
Madaktari walijaribu kuushona ulimi huo kwa lengo la kuurejesha
sehemu ulipokuwepo awali, lakini walishindwa na baada ya siku chache
Soren aliruhusiwa kutoka hospitalini.
Kwa sasa Soren yupo nyumbani na anaendelea kupona, lakini hawezi tena
kuzungumza na amekuwa akipewa chakula cha majimaji. Hata hivyo, Soren
mwenyewe hajutii kitendo alichokifanya na amekuwa akijivunia kwa ujasiri
na kumfurahisha Mungu Shiva.
Kutokana na kitendo hicho, familia yake imeshtushwa, lakini
imekubaliana na hali hiyo. Mama wa Soren anasema "mwanagu amekuwa
akijihusisha na mambo ya dini tangu akiwa mtoto".
"Amekuwa akipenda dini sana, lakini sikuamini kama ipo siku atakata
ulimi wake kumfurahisha mungu. Sijui kitakachotokea kwake lakini najua
hataweza tena kuzungumza vizuri. Maisha yake ya baadaye yatamtegemea
Mungu zaidi". Hata hivyo, mama huyo mwenye watoto wanne, ana uhakika
Soren atapata baraka.
"Mwanangu amejitolea ulimi wake kumfurahisha mungu hivyo tuna hakika
mungu atatimiza maombi yake yote na kumpa maisha mazuri", anasema mama
huyo. Watu wa eneo hilo wameshangazwa na jinsi vyombo vya habari
vilivyolichukulia suala hilo kwani wao wanaona ni kitu cha kawaida
kutokea. Jirani wa Soren, Manoj Sharma anasema;
"watu wa eneo hili ni washirikina sana na siku zote wanatekeleza
mambo ya ajabu. Mwaka 2011 kijana mmoja alijikata vidole viwili na kutoa
sadaka kwa Mungu katika msikiti huohuo, hivyo tukio hili si jipya
ingawa linaumiza nafsi za wengi."
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment