Mtoto Neema Joseph (2) akilia kutokana na maumivu makali ya jicho.
KWELI ni
zaidi ya mateso! Ukisema we unaumwa lakini unapata usingizi, kumbe
hujawaona wagonjwa wenyewe! Mtoto Neema Joseph (2) anateseka kwa
ugonjwa wa jicho ambalo limefumuka na kutoka nje huku likitoa harufu
kali na maumivu yasiyo na mfano,Mtoto huyo anayelia wakati wote
kutokana na maumivu, anaishi na mama yake mzazi, Annastazia Yohana (28)
kwenye Kijiji cha Bugomba, Kata ya Bulungwa wilayani Kahama, Shinyanga.
Akizungumza
huku akimwaga machozi kwa uzito wa tatizo la mwanaye, mama Neema
alisema hali yake ya maisha kiuchumi ni mbaya, hasa kufuatia kufiwa na
mumewe, Josephat miezi tisa baada ya kujifungua mtoto huyo huku akiwa
analea watoto wenginewawili.
SIKIA KILIO CHA MAMA NEEMA
“Tangu mume wangu afariki dunia nimekuwa na maisha ya shida, sina
msaada kwani hakuna ndugu wa mume wala wangu wenye hali nzuri ya maisha
na walio tayari kunisaidia kubeba mzigo wa maisha yangu.
“Hili
tatizo la jicho la mwanangu lilianza mwezi mmoja uliopita (Februari)
ambapo lilianza kwa kuwa jekundu huku likibubujika machozi mara kwa
mara.
“Alikuwa
akilifikicha kila wakati kitendo kilichoniasharia kuwa mwanangu anapata
mateso. Ndipo siku moja nilimpeleka Kituo cha Afya cha Kata.
Walimchunguza na kumpatia matibabu, lakini hali ndiyo ilizidi kuwa mbaya,” alisema mama Neema.
Alisema jicho lilianza kutokeza kwa nje na kutoa mwonekano wa
kutisha. Baadhi ya watu walimshauri ampeleke mtoto huyo kwenye Hospitali
ya Nkinga.
“Nilipopata
ushauri huo huku nikioneshwa mmoja wa wanakijiji ambaye mwanae alitibiwa
huko, nilimfuata mama yangu mzazi na kumuomba aniangalizie wanangu
wawili ambao mpaka sasa anao.
“Niliuza chakula changu chote cha akiba ili kupata pesa ya nauli na matibabu,” alisema mama wa mtoto huyo.
HOSPITALI KUBWA NDIYO WANAWEZA
Mama Neema aliendelea kuweka wazi kwamba, madaktari wa Hospitali ya
Nkinga walimfanyia uchunguzi mtoto wake na kusema tatizo lake linaweza
kutibiwa Hospitali ya
Kilimanjaro
Christian Medical Center (KCMC) iliyopo Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Alisema kwa kauli hiyo, alilazimika kurejea nyumbani na mwanae kwa vile
uwezo wa kufika huko hakuwa nao.
ASAKA FEDHA, AENDA KUSAKA TIBA ZAIDI
Mama Neema aliendelea kusema: “Hali ya mtoto ikazidi kuwa mbaya
zaidi. Sasa jicho lilizidi kutoka nje huku likiambatana na majimaji ya
njano na harufu kali. Alikuwa akilia sana kwa maumivu.
“Ilibidi
nisake fedha, nikampeleka Kahama mjini kuomba msaada wa matibabu. Kule
Kahama nilikutana na wanawake watatu ambao walinieleza nifike uwanja wa
michezo kuna madaktari wa saratani walioletwa na Shirika la Huheso
Foundation ambao walinikabidhi kwa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya
Kahama.”
MGANGA WA WILAYA AZUNGUMZA
Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Helen Yesaya
alikiri kumpokea mtoto huyo. Alisema alimpeleka kwa daktari wa macho ili
kumfanyia uchunguzi zaidi wa kubaini kama tatizo la jicho hilo ni
saratani au la!
“Hata
hivyo, kwa vyovyote itakavyokuwa ni budi mtoto huyu apelekwe Hospitali
ya Rufaa ya Bugando, Mwanza kwa ajili ya matibabu zaidi. Kama
unavyomuona, jicho limeoza, linatoa usaha, kwa kweli anahitaji
kusaidiwa,” alisema Dokta Helen huku akisikitika.
MAMA TENA
Akizungumzia taarifa hizo, mama wa mtoto huyo alisema hali yake
kiuchumi ni mbaya, uwezo wa kuishi jijini Mwanza wakati mwanae
akiendelea na matibabu hana, hivyo anawaomba Watanzania wamchangie fedha
ambazo anaamini zitakuwa msaada wa kupata tiba bora ya mtoto wake.
KUTOA NI MOYO
Kwa yeyote aliyeguswa na tatizo la mtoto Neema anaweza kumsaidia kwa
kuwasiliana na Shirika la Huheso Foundation la mjini Kahama kwa namba;
0753 444 840-Juma Mwesigwa, atawasiliana na mama Neema.
>>>>>GPL
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro







Post a Comment
Post a Comment