Hoja ya kumng’oa Spika Zziwa ilianza kuzungumzwa kwenye vyombo vya
habari vya Afrika Mashariki kwa wiki kadhaa sasa na hatimaye
kuwasilishwa jana na Mbunge Peter Mathuki kutoka Kenya kwa niaba ya
wenzake Shy-Rose Bhanji wa Tanzania, Nyiranilimo Odette wa Rwanda na
Hafsa Mossi kutoka Burundi.PICHA|MAKTABA
Arusha. Bunge la Afrika Mashariki (Eala) limeanza kuonekana kufanana na Bunge la Katiba linaloendelea mjini Dodoma.
Arusha. Bunge la Afrika Mashariki (Eala) limeanza kuonekana kufanana na Bunge la Katiba linaloendelea mjini Dodoma.
Bunge hilo jana limevunjika bila kujulikana
litakutana tena lini baada ya kuibuka mabishano ya kisheria kuhusu hoja
ya kutokuwa na imani na Spika, Margret Zziwa.
Hoja ya kumng’oa Spika Zziwa ilianza kuzungumzwa
kwenye vyombo vya habari vya Afrika Mashariki kwa wiki kadhaa sasa na
hatimaye kuwasilishwa jana na Mbunge Peter Mathuki kutoka Kenya kwa
niaba ya wenzake Shy-Rose Bhanji wa Tanzania, Nyiranilimo Odette wa
Rwanda na Hafsa Mossi kutoka Burundi.
Awali Bunge hilo linalopaswa kuanza vikao vyake
saa 8:00 mchana lilichelewa kuanza hadi Saa 9:44 alasiri baada ya
wabunge kugoma kuingia ukumbini walipobaini kuwa hoja ya kumng’oa Spika
haikuwa miongoni mwa shughuli za Bunge kwenye kikao cha jana.
Baada ya mashauriano ya muda mrefu kati ya ofisi
ya spika, Mwanasheria wa EAC, Wakili Wilbert Kaahwa na Katibu wa Bunge,
Kenneth Madete, Spika Zziwa alikubali hoja ya kumng’oa iongezwe kwenye
orodha ya shughuli za Bunge ndipo Mbunge Mathuki alipopewa fursa ya
kuwasilisha hoja.
Hata hivyo dakika moja tangu Mathuki alipoanza
kusoma maelezo ya hoja hiyo, Mbunge Fred Mukassa Mbidde aliinuka na
kuomba mwongozo wa Spika na alipopewa nafasi, alipinga hoja hiyo
kuwasilishwa na kujadiliwa kwa madai kuwa kuna kesi katika Mahakama ya
Afrika Mashariki (EACJ) inayohusiana na hoja hiyo.
Akifafanua Mbidde alisema kesi hiyo inaomba
mwongozo na ufafanuzi wa kisheria kuhusu kanuni ya 9 ya Bunge la EAC
inayoelekeza utaratibu wa kumwondoa madarakani Spika wa Eala iwapo
kutatokea haja ya kufanya hivyo.
Wakati Mbunge Mbidde akiwa bado amesimama huku
akiendelea kutoa hoja yake, Mbunge Joseph Ombasa kutoka Kenya aliinuka
na kumpinga mbunge mwenzake akisema anataka kulipotosha Bunge kwani
kifungu 38 (3) kinaruhusu Bunge hilo kujadili hoja yoyote yenye masilahi
ya umma wa EAC ikiwamo hilo la kumng’oa Spika.
Baada ya hoja ya Ombassa, Mwanasheria wa EAC,
Kaahwa alisimama kutoa ufafanuzi wa kisheria licha ya kukiri kuwapo kesi
mahakamani alisema tayari mahakama hiyo imetoa uamuzi mdogo kuwa shauri
hilo haliwezi kuzuia shughuli na mjadala wowote wenye nia ya kumwondoa
Spika madarakani
Hoja hiyo ya Mwanasheria ilimwibua tena Mbunge
Mbidde aliyehoji kwanini maelezo na ufafanuzi wa mwanasheria huyo
yanatoa mwelekeo wa ulipo msimamo wake kuhusu hoja iliyokuwa mbele ya
Bunge.
Katika hali iliyoashiria uwapo wa kimkakati kati
ya kiti cha Spika na Mbunge Mbidde, Spika Zziwa naye aliunga mkono hoja
ya mwanasheria kuonekana anaelemea upande unaotaka ang’olewe.
Kauli hiyo ilimwamsha kitini Mwanasheria Kaahwa
aliyemhakikishia Spika kuwa hoja yake inalenga kusaidia uendeshaji bora
wa Bunge na siyo kuegemea upande unaotaka kumng’oa.
Baada ya malumbano hayo, Mathuki alinyanyuka kwa nia ya
kuendelea na hoja yake lakini Spika hakumpa nafasi na badala yake akatoa
ushauri wa hoja hiyo kuondolewa kwenye shughuli za Bunge lakini wabunge
wengi wakapinga kwa kupaza sauti za hapana.
Hivyo, ghafla Spika Zziwa alisimama na kutangaza
kuliahirisha bunge kwa muda usiojulikana akitumia kifungu cha 82 cha
kanuni za bunge hilo kinachotoa mamlaka kwa Spika kufanya hivyo pale
panapotokea hali ya kutoelewana ndani ya bunge.
Akitoa msimamo wa nchi ya Uganda anakotoka Spika
Zziwa, Waziri wa Afrika Mashariki kutoka Uganda, Shem Bagaine alisema,
Serikali ya nchi hiyo haitaki kuingilia mchakato wa vikao na uamuzi wa
Bunge la EAC, bali inasubiri kuona hatima ya hoja hiyo.
“ Kama nchi hatutaki kuingilia mchakato wa vikao
vya bunge. Kama hoja ya kumng’oa Spika itafanikiwa basi tutapendekeza
jina la mgombea mwingine wa nafasi hiyo kwa sababu bado ni zamu ya
Uganda kushika wadhifa huo,” alisema
Wakati hali ikiwa hivyo, taarifa za uhakika
zilizopatikana kutoka miongoni mwa wabunge zinaeleza kuwa, Rais Yoweri
Mseveni wa Uganda aliwataka wabunge wa Eala kuahirisha hoja hiyo ili
kumpa fursa ya kuwasiliana na marais wenzake wa EAC.
Rais Museveni alikutana na baadhi ya wabunge kutoka Uganda mwishoni mwa wiki iliyopita.
>>>>>Mwananchi
<<<<<BOFYA HAPA ULIKE PAGE YETU KWA HABARI NYINGI ZAIDI >>>>>
>>>>>Mwananchi
<<<<<BOFYA HAPA ULIKE PAGE YETU KWA HABARI NYINGI ZAIDI >>>>>
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro







Post a Comment
Post a Comment