
MBUNGE
wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), anatarajia kuanza ziara ya
siku tano mkoani Kigoma, itakayomfikisha katika majimbo mbalimbali ya
uchaguzi mkoani Kigoma.
Katibu
wa mbunge huyo, Alex Kitumo alisema jana kuwa Zitto atawasili mkoani
Kigoma leo ambapo atapokewa Uwanja wa Ndege wa Kigoma kwa maandamano ya
wanachama na wapenzi wa mbunge huyo.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo, maandamano hayo ya wanachama na wapenzi wa
Chadema Mkoa wa Kigoma, yatamsindikiza mbunge huyo hadi eneo la Mwandiga
kwenye ngome yake Kuu ambapo atahutubia mkutano wa hadhara.
Ziara
hiyo ya Zitto, imeanza wakati mahasimu wake, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Willibrod Slaa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, wakifanya
ziara kama hizo, zinazoitwa za kuimarisha chama.
Tofauti
na jina la ziara hizo, kwamba ni za kuimarisha chama, viongozi hao wa
Chadema wamekuwa wakiuuza uamuzi wa Kamati Kuu ya Chama hicho wa kumvua
madaraka Zitto na wenzake.
Hata
hivyo, Kitumo hakusema kama Zitto naye atatumia ziara hiyo kupinga
akina Mbowe na Dk Slaa, lakini alisema siku inayofuatia, Zitto atakuwa
na mikutano miwili wilayani Kasulu ambako kabla ya mikutano hiyo ya
hadhara, atakuwa na kikao cha ndani na wazee wa Chadema wa wilaya hiyo
kabla jioni hajahutubia mkutano wa hadhara mjini Kasulu.
Ratiba
ya Mbunge huyo inaonesha kuwa baada ya mkutano wa Kasulu siku ya
Jumatatu, Zitto atafanya mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Mkongoro
Kigoma Vijijini jimboni kwake, mkutano ambao utatanguliwa na mkutano wa
wazee wa jimbo hilo pia.
Katibu
wa mbunge huyo alisema kuwa baada ya ratiba hiyo ya awali, watatoa
ratiba nyingine ya shughuli za mbunge huyo mkoani Kigoma ambayo pia
itazingatia majukumu yake mengine ya Kitaifa ya Mbunge huyo ambayo
hayakuwekwa wazi.
Waandishi
wa habari walitaka kujua kama Zitto anaruhusiwa kufanya mikutano maeneo
mengine tofauti na jimboni kwake, wakati amevuliwa nyadhifa zote za
chama kitaifa, lakini Katibu wa Mbunge alijibu kuwa Katiba ya Chadema
inamruhusu kufanya hivyo.
“Katiba
inampa mamlaka Zitto kama Mbunge ya kufanya shughuli ambazo atazifanya
za kuimarisha chama na kusaidia chama chake na ndiyo dhamira kuu ya
ziara hiyo,” alisema Kitumo.
Licha
ya habari za ndani kueleza kuwa ziara hiyo inalenga kufuta propaganda
zilizopandikizwa na Dk Slaa, Kitumo alikanusha jambo hilo na kusema kuwa
ziara hiyo haihusu lolote kuhusu aliyozungumza au kufanya Dk Slaa.
---Habari leo
---Habari leo
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro








Post a Comment
Post a Comment