Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This


TAMKO LA UMOJA WA MATAWI YA WANACHADEMA MKOA WA MWANZA DHIDI YA UAMUZI  HARAMU WA KAMATI KUU YA CHADEMA.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

UTANGULIZI

Ndugu wanahabari, mbele yenu ni muunganiko wa wawakilishi wa matawi 189 ya chama cha demokrasia na maendeleo mkoa wa mwanza. Umoja huu wa matawi unawajumuisha wajumbe kutoka majimbo yote ya mkoa wa mwanza.

Hivyo katika kikao chetu tulichoketi tarehe 30.nov 2013 kuanzia saa nne asubuhi mpaka saa tisa kasorobo, pamoja na mambo mengine tumeazimia kuanzisha umoja huu wa wanachama.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba viongozi wetu wanaotuwakilisha kwenye vikao vya maamuzi kama  vile wilaya, mkoa na taifa wamekuwa waoga na wameshindwa kuwakilisha mawazo yetu tuliyowatuma badala yake wengi wao wamekubali kuwa vibaraka wa kile kinachoitwa CHADEMA KASKAZ

Kutokana na ukweli kwamba msingi wa chama chetu na chama kingine chochote kile cha siasa, uimara na uhai wake unatokana na uwepo wa misingi na matawi ya chama, hivyo sisi wanachama wa matawi haya 189 tumeamua kuunganisha nguvu zetu kutetea chama chetu na kuhakikisha haki, heshima, katiba na maadili ya chama vinafuatwa bila ya kuogopana wala kuoneana haya.

Umoja huu umeonelea ni vyema kuutaarifu umma wa watanzania na wapenzi na wanachama wa chadema mambo kadhaa yafuatayo
Kwamba:-

Chadema ni chama cha siasa kinachopaswa kuendeshwa kwa misingi ya kufuata taratibu, kanuni na katiba yake na si vinginevyo. Lakini badala yake kwasasa kumeibuka ombwe kubwa kwa viongozi wetu wa juu kujitwalia mamlaka ya chama kinyume na matakwa ya katiba ya chama chetu hususan katika kutoa haki sawa kwa viongozi na wanachama wa chama chetu.
 
 Kumekuwepo na upendeleo wa hali ya juu sana kwa wale wanao amini kuwa ndani ya chama hawawaungi mkono hivyo kupelekea kuwaadhibu kama ndio kinga yao ya kuendelea kuongoza bila kuhojiwa au kukosolewa.

Sababu zilizotolewa na kamati kuu hazikubaliki

Maamuzi ya kamati kuu ya tarehe 20-21 /11/2013 ya kuwavua uongozi Mh: Zitto Zuberi Kabwe, Dr. Kitila Mkumbo na Ndg Samson Mwigamba, kumeonyesha dhahiri si woga tu wa Demokrasia bali ni unafki na Uzandiki wa hali ya juu sana kwa viongozi wetu kuikwepa Demokrasia kwa kisingizio cha kusaliti na uhaini ndani ya chama.
 
 Katiba yetu imeweka wazi Ibara ya 6 Kifungu cha 3 kipengele cha 6. (a – f) Mamlaka za nidhamu na uwajibishaji ndani ya chama. Kulikuwa na haraka gani ya kufanya maamuzi bila kufuata taratibu hizi kwa viongozi hawa? 

Tuonavyo sisi baadhi ya wanachama huo ni umangi meza na udhalilishaji wa kibaguzi ndani ya chama kwa viongozi wetu waliotumia nguvu zao na akili nyingi sana kukijenga chama.

Sababu kubwa ya kuandamwa kwa viongozi hawa ni

1.    Kutaka kujua mapato na matumizi ya fedha za chama zinazotokana na Ruzuku ya fedha za serikali.
 
2.    Michango ya wanachama na wapenzi kwenye mikutano ya wazi.
 
3.    Harambee  za M4C Mwanza, Arusha na Dar es saalam.
 
4.    Kutaka kujua taratibu za manunuzi ya rasilimali ya chama namna walivyopatikana wazabuni wa kusambaza bendera na kadi za chama, magari na pikipiki ambapo ununuzi wake ni wa mashaka makubwa.
 
5.    Kutaka kuona usawa wa kimadaraka kwa viongozi wote bila ubaguzi wa aina yoyote kuanzia ngazi ya chini mpaka Taifa kinyume na ilivyo sasa hasa makao makuu ya chama ambapo ukanda na ubaguzi wa hali ya juu umetawala.

Kushamiri kwa migogoro

Mwenyekiti na katibu mkuu wameshindwa kutatua migogoro ya viongozi na wanachama kutoka mikoani kwa njia sahihi za vikao na kwa wakati hivyo kutoa mwanya kwa viongozi na wanachama kutumia njia ya mitandao ya kijamii tukiongozwa na katibu mkuu mwenyewe kujitokeza mara kwa mara kwenye mitandao hiyo hiyo kwa madai ya kutolea ufafanuzi wa mambo mbalimbali yahusuyo maswala ya chama ilihali akijua kufanya hivyo ni usaliti mkubwa kwa chama chake.

Njia hiyo ya nje ya vikao ilipelekea migogoro mikubwa sana hususan mkoa wetu wa Mwanza na kupelekea kupoteza Halmashauri ya Jiji la Mwanza kutokana na kufukuzwa kwa baadhi ya madiwani, kuvunjwa uongozi wa mkoa na wabunge kuwa juu ya chama na kutumia nafasi zao kupanga safu za uongozi wanao uona watawatumikia wao na si chama hivyo kusababisha mifarakano mikubwa ndani ya chama na kupelekea kuvuliwa uongozi kwa viongozi mbalimbali katika mkoa wetu kwa maamuzi yasiyo zingatia utafiti na uhalisia wa kweli ndani ya chama.

Mwenyekiti na katibu mkuu wamekuwa vinara wa kuvunja katiba Mfano:
Kitendo cha kutoa muongozo nje na matakwa ya katiba juu ya kuwapata wawakilishi kwenye vyombo vya maamuzi kama wabunge kwamba wanaohitaji kugombea 2015 waandike barua makao makuu na wao ndio watatoa wagombea kinyume na katiba ya chama Ibara 7.2.13 inayotoa taratibu ya kuwapata wagombea.

Huo ni uvunjaji wa katiba na ubakaji wa demekrasia ndani ya chama. Sidhani kama kuna uhaini zaidi ya huu .Swali la kujiuliza hapa, Je, kama leo sisi Chadema hatuheshimu katiba yetu tuliyoitunga sisi wenyewe itakuwaje siku tukikabidhiwa nchi yenye watu wenye mawazo na mtizamo tofauti na sisi?. Hatutaki kuamini kama nchi hii inaweza kugeuka uwanja wa maopambano ya kivita.

Tunataka kujua hatua gani zilizochukualiwa dhidi ya Mbunge wa Arusha Mjini Mh: Godbless Lema kumkashfu kiongozi wa chama Mh: Zitto Zuberi Kabwe kuwa ni mnafiki na Mzandiki kwenye mitandao ya kijamii .

Pia tunataka kujua hatua gani zilizochukuliwa na chama dhidi ya Bw Henry Kilewo kwa kuweka  waraka unaoitwa ripoti ya siri inayomhusu Zitto. 

Chadema  makao makuu kupitia kwa mkurugenzi wa habari na uenezi wa chama ilikana mbele ya vyombo vya habari kuwa  haihusiki na waraka huo , lakini  Bw Kilewo ambaye pia ni kiongozi wa chama ngazi ya mkoa wa Kinondoni aliuweka waraka huo  kwenye Blog yake ilihali akijua kufanya hivyo ni kinyume na kanuni za viongozi wa chama kuhusu maadili ya viongozi kanuni ya 10.

Tunataka kuona nguvu iliyotumika kuwaadhibu Mh: Zitto na wenzake kwa kuandaa waraka ujulikanao kama mkakati wa mabadiliko 2013  inatumika kwa hawa waliotumia njia chafu ya kuandaa waraka wa kumchafua zitto ambao chama kinawajua na baadhi yao tumewaweka humu kwenye tamko letu.
  
Matwakwa  yetu:
1.Mwekiti na katibu mkuu wajiuzulu mara moja ili kupisha uchunguzi wa mapato na matumizi ya fedha za chama ambazo zinatokana na kodi za wavuja jasho wananchi .

2.M/kiti na katibu mkuu watoe ufafanuzi juu ya kuvunja katiba kwa kuondoa kipengele cha ukomo wa uongozi ndani ya chama .Kutangaza uchaguzi huku mkiwaondoa washindani wenu ni uwoga na ubakaji wa Demokrasia.

Hitimisho:
Tunataka maamuzi haya HARAMU yaliyofanywa na kamati kuu yabatilishwe na mchakato wa kuwavua viongozi hawa nyazifa zao ufuate taratibu na kanuni kwa mujibu wa katiba.

Tofauti na hapo tarehe 4/12/2013 tutaungana na wapigania Demokrasia kote nchini kufanya maandamano yasiyokuwa na ukomo mpaka uongozi uliopo  utoke madarakani.

Baada ya tarehe hiyo tunataka mhakikishe mnawahamisha wabunge vibaraka wote wa chadema mkoa wa mwanza.

Mchukueni  Wenje mkamtafutie jimbo Moshi na Highness Kiwia mkamtafutie  jimbo HAI na MACHAME.Hii ardhi ya kanda ya ziwa sio saizi yao na tunataka waondoke mara moja. Kinyume na hapo tutawaondoa huku wakishuhudia kwa macho yao.

Pia tunamuagiza Mbowe na Slaa wasithubutu kukanyaga ardhi hii ya kanda ya ziwa ikiwa bado hawajajiuzulu ama kubadili maamuzi yao HARAMU haraka iwezekanavyo. Hatuna sababu ya kuendelea kuwa watumwa wa fikra ndani ya chama chetu.

ROBERT E. GWANCHELE
Mwenyekiti wa umoja wa Matawi ya CHADEMA mkoa wa MWANZA
Mwenyekiti wa Vijana KANDA YA CHAMA ZIWA MAGHARIBI
Mjumbe kamati Tendaji wilaya  ya ILEMELA
0757 084776

Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala,

Hifadhi blog hii kwenye simu yako ili upate habari zote kwa urahisi zaidi

Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
http://www.facebook.com/kibonajoro

Post a Comment

 
Top